JAMVI: ODM inavyotatizwa na upinzani katika vita vya ubunge ngomeni
NA MWANDISHI WETU
LICHA ya eneobunge la Ugenya kuwa ngome ya Orange Democratic Movement (ODM) imebainika kuwa chama hicho kinakabiliwa na kibarua kigumu katika kinyang’anyiro cha kuhifadhi kiti hicho.
Uchaguzi mdogo katika eneo-bunge hilo umeratibiwa kufanyika Aprili 5, mwaka huu. Hii ni baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha ushindi wa Chris Karani (ODM) katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017, ikisema uchaguzi huo haukuendeshwa kwa mujibu wa sheria.
Uamuzi huo ulilandana na ule uliotolewa na Mahakama Kuu na ile ya Rufaa kufuatia kesi iliyowsilishwa na aliyekuwa Mbunge wa Ugenya David Ochieng’.
Kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Karan aliibuka mshindi kwa kura 23, 765 akifuatwa kwa karibu na Bw Ochieng’ aliyetetea kiti hicho kwa chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG). Hii ina maana kuwa Ochieng’, ambaye alikuwa ameasi ODM baada ya Uchaguzi wa 2013, alishindwa kwa kura 283 pekee.
Ni kwa msingi huo ambapo wadadisi wanasema kuwa, ODM inayoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga inakabiliwa na kibarua kigumu kuhifadhi kiti hicho ikizingatiwa utendakazi wa Bw Karan haukuwa umewaridhisha wakazi wengi wa Ugenya.
Kwa msingi huo, baadhi ya wafuasi wa ODM walivunjwa moyo na hatua ya makao makuu ya chama hicho kumpa Bw Karan uteuzi wa moja kwa moja pasi na kuandaa kura ya maamuzi.
Hii ndiyo sababu iliyopelekea mfanyabiashara Daniel Juma Omondi, ambaye alikuwa akinuia kupambana na Bw Karan katika kura ya mchujo, aligura ODM na kuamua kushiriki uchaguzi huo mdogo kwa tiketi ya chama cha Grand Dream Development Party (GDDP).
Wengine wanaoshiriki katika uchaguzi huo mdogo ni Brian Omondi Onyango (Thirdways Alliance), Joseph Mburu Mbugua (National Vision Party) na William Sino ambaye ni mgombeaji huru.
Dkt Mathews Okanga anafananisha changamoto inayoikabili ODM katika uchaguzi mdgoo wa Ugenya na ile iliyoikabili Julai mwaka jana katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Migori ambapo nusra ipoteze kiti hicho kwa mgombea wa chama kisichomaarufu eneo hilo.
“Itakumbukwa nusra Seneta Ochillo Ayacko ashindwe na mwanasiasa limbukeni Eddy Ochieng sababu ikiwa ni hatua ya ODM kupuuza lalama za wafuasi wake, akiwemo Gavana Okoth Obado, na kumpa Bw Ayacko tiketi ya moja kwa moja,” akasema mchanganuzi huyo wa masuala ya siasa ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro.
Japo Bw Oketch, 27, ambaye aliwania kwa tiketi ya chama cha Federal Party of Kenya, alishindwa na Bw Ayacko, ushindi huo ulikuwa mwembamba zaidi, wa kura 24,757 pekee.
Mwanasiasa huyo limbukeni alizoa kura 62,209 dhidi ya kura 86,966 alizopata Bw Ayacko ambaye ni mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa ikizingatiwa kuwa amewahi kuhudumu kama Mbunge wa Rongo mbali na kushikilia nyadhifa kadhaa za uwaziri katika serikali zilizopita.
Kulingana na Dkt Okanga, ushindi mwembamba wa ODM katika uchaguzi mdogo wa useneta ulionyesha wazi kuwa wafuasi wengi wa chama hicho walimpigia Oketch kura kwa hasira kwamba Bw Ayacko alipewa tiketi ya moja kwa moja.
“Hali kama hiyo huenda ikashuhudiwa katika eneo-bunge la Ugenya ambapo huenda wapigakura wakawapigia kura wapinzani wa Bw Karan. Kinaya ni kwamba, huenda atakayefaidi sio Bw Omondi wa GDDP bali Bw Ochieng wa MDG ambaye rekodi yake ya maendeleo eneo hilo inashabikiwa na wengi,” anasema msomi huyo.
Na ODM inaonekana kufahamu fika kuwa haitapata ushindi kwa urahisi licha ya chama hicho kuwa na umaarufu mkubwa katika eneo hilo. Hii ndiyo maana juzi Seneta wa Siaya James Orengo alisema chama hicho kitatumia nguvu, rasilimali na mikakati yake yote kuhakikisha kuwa kimehifadhi kiti hicho.
Mwanasiasa huyo, ambaye amewahi kuwa mbunge wa eneo hilo kwa mihula kadhaa, aidha alibashiri kuwa ushindi utawezeshwa na muafaka kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, kufuatia hatua ya chama hicho tawala kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.
“Kwa moyo wa handisheki, baadhi ya viongozi wa Jubilee wataungana nasi kumpigia debe mgombeaji wetu, kama walivyofanya wakati wa uchaguzi mdogo wa useneta wa Migori,” Bw Orengo akaongeza.
Mbali na hayo, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna ametangaza kuwa uongozi wa chama hicho umewaamuru wabunge, maseneta, magavana na madiwani wake kushiriki katika uchaguzi huo mdogo.
“Tuna imani kwamba tutahifadhi kiti hiki kwa sababu ni chetu, sawa na kile cha Embakasi Kusini. Kiongozi wetu ametoa amri kuwa kila kiongozi aliyechaguliwa kwa tiketi ya ODM ajumuike na wengine kumpigia mheshimiwa Karan,” akasema.
Mkakati mwingine ambao unatumiwa na viongozi wa ODM kuwavutia wapigakura upande wa mgombeaji wao ni kumsawiri Bw Ochieng’ kuwa “mradi” wa Naibu Rais William Ruto.
Lengo hapa ni kuwafanya wapiga kura waamini kuwa kimsingi, uchaguzi huo mdogo ni jukwaa la mieleka ya kisiasa kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto. ODM ilitumia mbinu kama hii katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Migori, ilipodaiwa kuwa Bw Oketch alikuwa kikaragosi cha Naibu Rais.
Lakini kupitia msemaji wake David Mugonyi, Dkt Ruto alipuuzilia mbali madai hayo akisema hana wakati wa kuingilia “masuala ya ndani ya watu ambao tuliwashinda katika uchaguzi mkuu uliopita”.
“Chama hiki kinapaswa kukoma kuingiza jina la Naibu Rais katika uchaguzi huo ili kujifunika aibu baada ya kufeli katika uendeshaji wa masuala yake,” akasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.
Bw Ochieng’ naye amepinga madai yaliyoibuliwa na ODM kwamba yeye ni mwandani wa Dkt Ruto akisema hizo ni porojo zinazoenezwa na wapinzani wake ili kumchafulia jina.
“Umewahi kuniona katika mikutano ya Ruto?. Hizi ni propaganda zinazoendeshwa na wapinzani wangu ambao wameingiwa baridi kwa hofu kuwa nitawashinda,” akaambia meza ya Jamvi kwa njia ya simu.
Lakini Bw Martin Andati anakitazama kinyang’anyiro cha Ugenya kama mtihani mgumu wa kisiasa kwa Bw Orengo kuhusiana na ndoto yake ya kuwania Ugavana wa Siaya 2022.
“Japo ni kweli kushindwa kwa Bw Karan kutakuwa pigo kwa azma ya urais ya Bw Odinga, yule ambaye atapoteza zaidi ni Bw Orengo ambaye anaunia kuwania ugavana wa Siaya. Hii ni kwa sababu Ugenya ni kwake nyumbani na wema huanza nyumbani,” akasema.
Kulingana na mchanganuzi huyo wa kisiasa, itakuwa vigumu kwa ODM kupata uungwaji mkono kutoka maeneo bunge mengine ya Siaya endapo, kwa bahati mbaya, chama hicho kitangushwa katika uchaguzi huo mdogo.
“Kwa hivyo, matokeo ya uchaguzi huu mdogo yatabaini mustakabali wa Orengo kisiasa mnamo 2022,” anakariri Bw Andati.