MakalaSiasa

JAMVI: Tuhuma za ufisadi huenda zikaathiri utendakazi wa Chebukati

March 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine maswali yameibuliwa kuhusu iwapo mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati na makamishna wenzake wawili wamehitimu kimaadili kuweza kusimamia shughuli za tume hizo zitakazogharimu pesa nyingi.

Shughuli hizo ni kama vile uanishaji upya wa mipaka, chaguzi ndogo katika maeneo bunge ya Ugenya, Embakasi Kusini na Wajir Magharibi, kura ya maamuzi na uchaguzi mkuu ujao mnamo 2022.

Hii ni baada ya Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) kupendekeza kwamba Bw Chebukati na makamishna Boya Molu na Abdi Guliye waondoke afisini ili wachunguzwe na kushtakiwa kuhusiana na utoaji zabuni za thamani Sh9.3 bilioni kinyume cha sheria wakati wa uchaguzi mkuu wa 2017.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, inakubaliana na ufichuzi wa Mkaguzi Mkuu wa Matumizi ya Pesa za Serikali Edward Ouko, kwenye ripoti yake, kwamba huenda Sh4.6 bilioni zilipotea katika sakata ya utoaji zabuni.

Miongoni mwa zabuni hizo ni ile ya ununuzi wa mitambo ya kielektroniki (KIEMs Kits) iliyotumika katika uchaguzi huo na marudio ya kura ya urais wa Oktoba 26,2019 iliyogharimu Sh6.3 bilioni.

Na licha ya hayo, Spika wa Bunge la Kitaifa ameamuru kuondolewa kwa sehemu ya ripoti ya PAC inayopendekeza kutimuliwa Bw Chebukati na wenzake, wadadisi wakisema tayari watu hao wamepakwa tope la ufisadi.

“Bw Chebukati na wenzake wamekosa heshima mbele ya umma kwa kuhusishwa na sakata ya ufisadi iliyopelekea Wakenya walipaushuru kupoteza mabilioni ya fedha wakati wa uchaguzi uliopita. Na licha ya Bw Muturi kuonekana kuwanusuru kwa kuzima pendekezo la PAC kwamba waondoke afisini, hawastahili kuendelea kushikilia wadhifa kwani hawajatimiza hitaji la Sura ya sita ya Katiba,” akasema James Mwamu, akisema hali hiyo itayeyusha zaida imani ya Wakenya kwa utendakazi wa IEBC.

Bw Mwamu ambaye ni wakili mtajika, anaongeza kuwa kando na ripoti ya kamati ya PAC, ripoti ya awali iliyotolewa na Mkaguzi Mkuu Bw Ouko pia iliwahusishwa makamishna hao, pamoja na wenzao waliojiuzulu mwaka jana, na sakata hiyo hali ambayo inafanya agizo la Muturi kutoweza kuwatakasa makamishna hao.

“Sawa na ripoti ya PAC, Bw Ouko pia anapendekeza kuwa Chebukati na wenzake pamoja na maafisa wa afisi kuu wachunguzwe na asasi husika kama vile EACC na DCI kufuatia kupotea kwa pesa za umma. Tofauti ni kwamba ripoti ya Mkaguzi Mkuu haijapendekeza waondoke afisini,” anaeleza Bw Mwamu ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

Kwa mfano, ripoti ya PAC ilidai kuwa kampuni ya mawakili ya Cootow and Associates ambayo ilianzishwa na Bw Chebukati, ilipewa zabuni ya na IEBC kwa idhini ya mwenyekiti huyo na wenzake, pasina utaratibu wa kisheria kufuatwa. Hata hivyo, alipofika mbele ya kamati hiyo Desemba 2018,, mwenyekiti huyo alijiondoa kama mshirika wa kampuni hiyo pindi alipoteuliwa kwa wadhifa huo mapema 2017, na kwamba hafai kuhusishwa nayo.

Kando na Chebukati, Molu na Guliye, ripoti hiyo pia inapendekeza makamishna waliojiuzulu Aprili 20, 2018; Consolata Maina, Margaret Mwachanya na Paul Kurgat wachunguzwe kwa lengo la kushtakiwa kwa kushiriki njama ya uidhinishwaji wa zabuni kinyume cha sheria hatua iliyosababisha kupotea kwa pesa za umma.

Shoka la kamati ya PAC pia ilielekezwa kwa aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa zamani Ezra Chiloba, kaimu afisa mkuu mtendaji Marjan Hussien, Praxedes Tororey (Mkurugenzi wa idara ya sheria) na James Muhati (mkurugenzi wa ICT).

Hata hivyo, ripoti hiyo iliporatibiwa kujadiliwa bungeni Jumatano wiki jana, kiongozi wa wengi Aden Duale alipinga pendekezo la kuondolewa kwa makamishna wa sasa afisini, akisema linakiuka Katiba.

“Mapendekezo ya kamati hii yatakiuka katiba ikiwa yatapitishwa. Vilevile, yataleta matokeo mabaya kwa sababu hakutakuwa na tume ambayo inaweza kusimamia chaguzi ndogo endapo zitatokea.

Isitoshe, kupitishwa kwa ripoti hii ya PAC kutaathiri chaguzi ndogo katika maeneo ya bunge ya Ugenya, Embakasi Kusini na Wajir Magharibi ambayo tayari zimetangazwa,” akasema Bw Duale ambaye pia ni Mbunge wa Garissa Mjini.

Kulingana na Mbunge huyo, kuondolewa kwa makamishna wa IEBC kunafaa kufuata mwongozo uliowekwa katika kipengee cha 251 cha Katiba. Kipengee hicho pia kimetoa sababu ambazo zinaweza kusababisha hatua hiyo kuchukuliwa dhidi ya wanachama wa tume za kikatiba na afisi huru.

Baadhi ya sababu hizo ni ukiukaji wa katiba, mienendo mibaya, kulemaa kiakili, kushindwa kutekeleza majukumu ya afisi na endapo wanachama watatangazwa kuwa wamefilisika.

Hata hivyo, Bw Wandayi na wabunge; Otiende Amollo (Rarieda) na Junet Mohamed (Suna Mashariki) walipinga kauli ya Duale na uamuzi wa Spika Muturi wakisema, pendekezo la PAC lililenga kuanzisha mchakato wa kuwaondoa watatu hao “kwa mujibu wa hitaji la Katiba”.

“Kamati hii inafahamu hitaji la kipengee cha 251 cha Katiba. Kwa hivyo, ripoti yake sio ombi la kutaka makamishna hao waondolewe afisini bali msingi wa hatua. Kwa hivyo, pingamizi la Duale halikuwa na mantiki yoyote,” akasema Bw Wandayi.

Dkt Amollo anasema kuzimwa kwa pendekezo ya kamati hiyo, ni sawa na kuhujumu wajibu wake (PAC) wa kikatiba kuhusu suala lenye umuhimu mkubwa kwa Wakenya.