JAMVI: Unafiki wa Ruto
Na CHARLES WASONGA
MASWALI yameibuliwa kuhusu sababu zinazochangia kupanda kwa umaarufu wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya huku umaarufu wa Rais Uhuru Kenyatta ukidorora katika eneo hilo ambalo ni ngome ya kisiasa ya kiongozi huyo wa kitaifa.
Hii ni licha ya kwamba kipengee cha 147 (1) cha Katiba ya sasa kinamtambua Naibu Rais kama “Msaidizi Mkuu wa Rais na atamsaidia (Rais) katika utekelezaji wa majukumu ya afisi yake.
Na kulingana na ibara ya 3 ya kipengee hicho, Naibu Rais anaweza kushikilia hatamu za uongozi wa nchi ikiwa “Rais hayuko au amelemewa kwa muda au wakati wowote ule ambapo rais ataamua.”
Itakumbukwa kwamba ni kwa msingi wa kipengee hichi cha Katiba ambapo mnamo Octoba 6, 2014 Rais Kenyatta,alimpokeza Dkt Ruto mamlaka ya uongozi wa nchini, kwa muda, alipoelekea katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) The Hague, Uholanzi kuhudhuria kesi kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu.
Lakini tangu mwaka jana, Rais amekuwa akilaumiwa kwa madhila yanayowakumba wakazi wa Mlima Kenya haswa katika nyanja ya kilimo, miundomsingi na biashara. Lakini lakini Dkt Ruto akishabikiwa kila anapazuru eneo hilo huku akisawiriwa kama “mwokozi wao.”
Wakati huu zaidi ya wabunge 30 kutokana kaunti za Murang’a, Nyeri, Kirinyaga, Embu, Tharaka Nithi, Meru, Nyandarua na Kiambu wanaunga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.
Hii ni kwa sababu, miongoni mwa sababu nyinginezo, wanamsawiri Dkt Ruto kama kiongozi ambaye atashughulikia changamoto zinazowakabiliwa wakulima wa kahawa, majani chai, viazi, mpunga, miraa na maziwa.
Mazao haya ndio nguzo kuu ya uchumi wa eneo la Mlima Kenya lakini katika miaka ya hivi karibu mapato kutoka kwayo yamepungua kwa kiasi kikubwa na kuwaacha wakulima wakiwa masikini.
Vilevile, Mlima Kenya pia wameelekeza kero zao kwa Rais Kenyatta kutokana na sera kali za serikali ambazo zimeathiri pakubwa biashara zao haswa wale wanaoagiza bidhaa kutoka nchi za nje. Miongoni mwa sera hizo ni kama zile zinazopiga marufuku uagizaji wa magari yaliyotumika kwa miaka mitano na zaidi.
Masuala haya ni miongoni mwa yale ambayo yalitawala mkutano wa viongozi wa eneo la Mlima Kenya ambao uliandaliwa katika Ikulu ya ndogo ya Sagana mwezi Novemba mwaka huu.
Lakini wadadisi wa masuala ya kisheria na uongozi wanasema kuwa japo wanasiasa na wakazi wa eneo la Mlima Kenya wanamsawiri Dkt Ruto kama ambaye atakayewaokoa kutokana na madhila yanayowazonga, yeye (Naibu Rais) pia anapasa kulaumiwa.
Tangu mwezi Machi mwaka jana, Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga walipozika tofauti zao kisiasa, Dkt Ruto amekuwa akikwepa hafla nyingi za uzinduzi wa miradi mikubwa ya serikali.
Kwa mfano, mwezi jana alikosa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Nairobi hadi Suswa, ulioongoza na Rais Kenyatta. Vilevile, wiki jana hakuwepo katika uzinduzi wa treni ya kusafirisha mizigo kutoka Nairobi hadi eneo la uwekezaji Naivasha.
Badala yake, alitumia wakati wake mwingi nyumbani kwake Sugoi kaunti ya Uasin Gishu, alipokea jumbe za wanasiasa kutoka sehemu mbalimbali kama kupigia debe azma yake ya kutaka kuingia Ikulu 2022.
Kulingana na Bw Barasa Nyukuri, ambaye ni mchanganuzi wa masuala kisiasa na uongozi, hatua ya Dkt Ruto kukwepa hafla kama hizo ni njama fiche ya kutaka kujiondoa kutoka kwa kivuli cha Rais Kenyatta, “haswa kuhusiana na miradi ambayo huenda ikafeli asiangukiwe na lawama.”
“Huu ni unafiki mkubwa ikizingatiwa kuwa yeye ni msaidizi mkuu wa Rais Kenyatta na anawajibika kwa mazuri na mabaya yanayojiri chini ya utawala wa Jubilee. Isitoshe, amekuwa akiwakumbusha Wakenya kwamba yeye ndiye naibu wa rais na ‘mtu wa mkono’ wa Bw Kenyatta,” anasema.
Kwa hivyo, kulingana na Bw Nyukuri, wakazi na wanasiasa wa eneo la Mlima Kenya wanafaa kuelekeza malalamishi yao, haswa, kuhusu kudorora kwa sekta kilimo, kwa Dkt Ruto.
“Katika miezi ya hivi karibu, Dkt Ruto amekuwa akizuru eneo Mlima Kenya kila mara kuongoza hafla za harambee na kuhudhuria ibada kadhaa makanisani. Swali ni je, mbona huwa hawamuulizi ziliko Sh3 bilioni zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu Juni 2019 kwa ajili ya kufufua sekta ya kahawa?” anauliza mtaalamu huyu.
Naye Profesa Edward Kisiang’ani anasema kuwa Dkt Ruto hafai kujitenga na kufeli kwa utekelezaji wa miradi yaliyoratibiwa na serikali ya Jubilee tangu 2013 akisema “ni unafiki kwake kujitia hamnazo kutokana na masuala kama hayo”.
“Hauwezi kutumia handisheki kati ya bosi wake Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kama kisingizio cha kujitenga na miradi mipango ya serikali ya Jubilee iliyofeli au inayoonekana kama yenye dosari machoni pa umma. Ni maendeleo gani atawaletea Wakenya 2022 ambayo ameshindwa kutekeleza wakati huu ambapo yeye ni naibu rais mwenye mamlaka?” akauliza msomi huyo ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Kwa mfano, ripoti iliyowasilishwa bungeni na Waziri Fedha, aliyesimamishwa kazi, Henry Rotich Desemba 2018, miradi ya Serikali Kuu inayokadiriwa kugharimu Sh366 bilioni imekwama tangu mwaka wa 2013.
Kulingana na ripoti baadhi miradi iliyokwama ni kama vile ujenzi wa barabara, mabwawa, umeme, unyunyiziaji mashamba maji na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Wajir, Tseikuru, Voi, Ikanga, Wagadud na Wilson.
Ujenzi wa viwanja vya michezo, kulingana na ripoti hiyo, pia umekwama, licha ya ahadi ya Dkt Ruto mnamo 2017 kuwa serikali ya Jubilee ingekamilisha ujenzi wa viwanja sita vya michezo ndani ya kipindi cha miezi sita.
Na majuzi ilifichuka kuwa mradi wa unyunyiziaji maji mashamba wa Galana-Kulalu iliyogharimu Sh17.5 bilioni na ule ya ununuzi wa vipakatalishi (iliyogharimu Sh24.5 bilioni) kwa wanafunzi wa darasa la kwanza, ilifeli kufikia malengo yao.