MakalaSiasa

JAMVI: Wandani wa UhuRuto wasajili vyama vipya

May 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

MGAWANYIKO wa kisiasa unaokikumba Chama cha Jubilee (JP) umezua hofu kubwa miongoni mwa waandani wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Dkt William Ruto, ambapo baadhi yao wameanza harakati za kusajili vyama tofauti vya kisiasa.

Kufikia sasa, vyama vipya karibu 30 vya kisiasa vimesajiliwa, huku ikibainika kuwa wengi waliovisajili ni baadhi ya viongozi walio katika Jubilee.

Kulingana na orodha iliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu, baadhi ya vyama ambavyo tayari vimesajiliwa ni Party of Economic Democracy, Transformational National Alliance (TNA), Golden Alliance Party, National Rebirth Party, Kenya Democracy for Change, Digital Kenya Party, Democratic Action Party of Kenya, National Reconstruction Alliance kati ya vingine.

Tayari, mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria amejitokeza wazi kueleza kuwa ndiye aliyesajili chama cha TNA, lengo lake kuu likiwa kuipa Mlima Kenya “sauti mbadala” kwenye uchaguzi wa 2022.

“Jubilee ni kama imesambaratika kwa sasa. Lengo langu ni kuhakikisha kuwa Mlima Kenya ina chama na sauti yake huru ielekeapo 2022,” asema Bw Kuria.

Mbunge huyo amesisitiza kuwa hatabadilisha wazo lake licha ya kukosolewa vikali na baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoka ukanda wa Mlima Kenya.

Duru zinaeleza kuwa wanasiasa wengi ambao wamesajili vyama hivyo wamewatumia washirika wao, kama njia moja ya kutotaka kujulikana mapema.

“Vyama vingi vimesajiliwa na wanasiasa ambao wanahofia kwamba JP itasambaratika hivi karibuni kutokana na mivutano ya kisiasa inayoendelea kati ya wandani wa Rais Kenyatta na Dkt Ruto,” akasema afisa mmoja ambaye hakutaka kutajwa.

Duru pia zinaeleza kuwa wengi ambao wamesajili vyama hivyo ni wanasiasa waliopoteza nyadhifa zao kutokana na shughuli tata za uteuzi zilizovikumba vyama vya Jubilee na ODM.

Kulingana na Bi Nderitu, afisi yake ilianza kupokea maombi ya usajili wa vyama hivyo baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti.

“Tunatarajia kupokea maombi ya vyama zaidi vya kisiasa. Wale wanaomba kutuma maombi lazima wazingatie kanuni zinazohitajika kabla ya chama chao kusajiliwa,” akasema, kwenye mahojiano.

Kulingana na wachanganuzi wa kisiasa, mkondo huo ni hatari kwa mustakabali wa mabw Uhuru na Ruto, kwani unaashiria kuwa msingi wa Jubilee tayari umetikisika.

Kulingana Dkt Njoki Mwangi, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, hilo pia linaashiria kuwa Rais Kenyatta atakuwa na muda mgumu sana kisiasa katika kipindi chake cha pili, ikiwa hatatangaza hadharani mwelekeo atakaochukua katika uchaguzi wa 2022.

“Kilicho dhahiri ni kuwa Rais Kenyatta mwenyewe ndiye wa kulaumiwa kutokana na migawanyiko inayoshuhudiwa katika Jubilee. Sababu kuu ni kuwa licha ya kushinikizwa na baadhi ya wabunge kueleza kiwazi ikiwa ‘atarudisha mkono’ kwa kumuunga Ruto mnamo 2022, amebaki kimya,” asema mchanganuzi huyo.

Wachanganuzi wanasema kuwa dalili kuhusu mwelekeo huo zilianza baada ya malalamishi yaliyoandama shughuli za uteuzi wa Jubilee mnamo 2017, ambapo baadhi ya wanasiasa maarufu walidai kunyang’anywa tiketi licha ya kuibuka washindi.

Miongoni mwa waliodai ‘kunyang’anywa’ ushindi wao ni aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo, mwaniaji wa ugavana katika Kaunti ya Uasin Gishu Zedekiah Buzeki, wabunge wa zamani Ndung’u Gethenji (Tetu), Kabando wa Kabando (Mukurwe-ini), aliyekuwa Seneta wa Murang’a Kembi Gitura kati ya wengine.

Wanasiasa wengi walimlaumu Dkt Ruto kwa kuingilia mchakato huo, kwani ndiye aliyekuwa msimamizi mkuu wa shughuli hizo kutoka makao makuu ya chama hicho, jijini Nairobi.

Kama kile kilichoonekana kuwa ‘kisasi’ kwa madai hayo, baadhi ya wanasiasa hao walibuni Chama cha Wananiaji Huru Kenya (KICA), ambapo wengi wao walijaribu kutetea nyadhifa zao lakini wakashindwa.

Kulingana na mchanganuzi Oscar Plato, hiyo ndiyo ilikuwa dalili ya kwanza kuwa hali haingekuwa shwari katika chama hicho.

“Hali inazidi kutokota Jubilee. Kwanza, Rais Kenyatta hajafanikiwa kuwatuliza wanasiasa ambao walihisi kunyang’anywa ushindi wao kwenye uteuzi wa 2017. Kama kiongozi wa chama, vilevile anaonekana kushindwa kuzima migawanyiko inayojitokeza kati ya mirengo ya ‘Tanga Tanga’ na ‘Kieleweke’,” asema Bw Plato, akitabiri kuwa huenda hali ikawa mbaya zaidi.

Kulingana na baadhi ya wabunge wa Jubilee waliozungumza na ‘Jamvi la Siasa,’ kiini kingine cha migawanyiko inayoshuhudiwa inatokana na hatua ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto kutoitisha mikutano ya chama, kama ilivyo kawaida kwa vyama vingine vya kisiasa.

“Tumekuwa tukiwashinikiza Rais Kenyatta na Dkt Ruto kuitisha mkutano wa chama, ili kuzima baadhi ya migawanyiko inayoendelea kushuhudiwa. Hata hivyo, hakuna anayeonekana kuzingatia kauli zetu,” akasema mbunge mmoja ambaye hakutaka kutajwa.

Awali, Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen, alikuwa amesema kuwa mkutano wa pamoja kati ya viongozi wote waliochaguliwa ndiyo ingekuwa njia ya pekee ambapo umoja katika chama hicho ungerejeshwa.

Wachanganuzi pia wanaeleza kuwa mojawapo ya misukumo ya kubuniwa kwa vyama hivyo vipya ni hatua ya utawala wa Jubilee “kutowashukuru” wale waliokubali kuvunja vyama vyao 2017 ili kuipa nguvu Jubilee.

Tayari, baadhi ya viongozi wa vyama vikuu vya kisiasa kama Musalia Mudavadi (Amani), Moses Wetang’ula (Ford-Kenya), Charity Ngilu (Narc) wameapa kutovunja vyama vyao hata ikiwa watapewa nyadhifa kuu serikalini.

Wachanganuzi wanasema ni lazima Rais Kenyatta adhibiti umoja wa Jubilee, la sivyo huenda ikasambaratika kabisa hata kabla ya 2022.