Jepchirchir, Ngetich na Sawe kuwania kuwa mwanariadha bora duniani wa nje ya uwanja
MALKIA wa Olimpiki na dunia mbio za kilomita 42, Peres Jepchirchir pamoja na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya 10km, Agnes Ngetich watawania tuzo ya mwanariadha bora wa kike wa nje ya uwanja mwaka 2025 dhidi ya wapinzani kutoka Uholanzi, Ethiopia na Uhispania.
Shirikisho la Riadha Duniani limetoa orodha ya wawaniaji wa tuzo hiyo ya kifahari Oktoba 27, 2025, ambapo Jepchirchir anaonekana atapata ushindani mkali sana kutoka kwa mzawa wa Ethiopia, Sifan Hassan anayekimbilia Uholanzi.
Sifan alikamata nafasi ya tatu kwenye London Marathon nchini Uingereza mnamo Aprili 27 kabla ya kushinda Sydney Marathon nchini Australia hapo Agosti 31. London na Sydney ni sehemu ya ligi ya Marathon Kuu Duniani iliyo pia na Tokyo (Japan), Boston, Chicago na New York (Amerika), na Berlin (Ujerumani).
Mwaniaji mwingine wa tuzo ya mwanariadha bora duniani wa kike nje ya uwanja ni Tigst Assefa kutoka Ethiopia. Assefa alishinda London Marathon kwa rekodi mpya ya dunia ya saa 2:15:50 baada ya kufuta ile ya 2:16:16 ambayo Jepchirchir aliweka akitawala London Marathon 2024. Alikamata nafasi ya pili nyuma ya Jepchirchir kwenye Riadha za Dunia jijini Tokyo, Japan hapo Septemba 14.
Mhispania Maria Perez ametawala mashindano yake yote saba mwaka huu ya fani ya kutembea kwa haraka yakiwemo 35km na 20km kwenye Riadha za Dunia hapo Septemba 13 na Septemba 20, mtawalia.
Ng’etich alitwaa ubingwa wa Sirikwa Classic Cross Country mjini Eldoret mwezi Februari kabla ya kunyakua taji la Valencia Half Marathon nchini Uhispania kwa muda wa tatu-bora duniani katika 21km wa saa 1:03:08. Mshikilizi wa rekodi ya dunia ni Muethiopia Letesenbet Gidey (1:02:52). Ngetich anashikilia muda wa pili-bora wa 1:03:04 aliopata akimaliza nyuma ya Gidey wakati wa Valencia Half Marathon 2024.
Mbali na orodha ya wawaniaji wa kike, Shirikisho la Riadha Duniani pia limetangaza wanaume watakaowania kuwa mwanariadha bora wa nje ya uwanja ambayo inajumuisha Sabastian Sawe (Kenya), Alphonce Simbu (Tanzania), Yomif Kejelcha (Ethiopia), Caio Bonfim (Brazil) na Evan Dunfee (Canada).
Sawe ni bingwa wa marathon za London na Berlin, naye Simbu ni Mtanzania wa kwanza kunyakua dhahabu kwenye Riadha za Dunia. Simbu aliibuka mshindi wa 42km, nao Bonfim na Dunfee walitawala 20km na 35 za kutembea kwa haraka, mtawalia.
Mashabiki wana fursa ya kuchagua mwanariadha wampendaye kwa kupigia kura mwanariadha katika kurasa za jamii za Shirikisho la Riadha Dunia kutoka Oktoba 27 hadi Novemba 2, 2025.