Jinsi juhudi zote za Tuju kuokoa mali ya Sh4.2 bilioni zilivyosambaratika kortini
MALI ya thamani kubwa ya aliyekuwa Waziri Raphael Tuju itapigwa mnada baada ya Mahakama ya Juu kuruhusu benki moja kuipigia kengele kuvutia wateja baada ya kushindwa kulipa mkopo wa Sh4.5 bilioni.
Bw Tuju ambaye amekuwa na bidii ya mchwa kuokoa mali yake aligonga mwamba Ijumaa baada ya mahakama ya upeo kuruhusu Benki ya East African Development Bank(EADB) kuuza hoteli yake ya kifahari iliyoko mtaani Karen Nairobi.
Bw Tuju amepambana kufa kupona kwa miaka zaidi ya 10 kuokoa mali yake kwa kuwasilisha kesi kuanzia mahakama kuu, mahakama ya rufaa na hatimaye mahakama ya juu.
Kilele cha malumbano haya ya kisheria kilifikiwa pale majaji watano wa mahakama ya juu walipojiondoa kwenye kesi hiyo na kuacha mwanasiasa huyo apambane na hali yake.
Majaji hao watano wa mahakama ya upeo walijiondoa kwenye kesi hiyo walisema maagizo ya Mahakama ya Rufaa kwamba mali ya Bw Tuju yasalie tu.
Hivyo basi majaji hao wa mahakama ya upeo walidumisha uamuzi wa Mahakama ya Rufaa uliotolewa Aprili 2023, na kutupilia mbali rufaa ya Bw Tuju kuzuia kutekelezwa kwa uamuzi ulioiruhusu Benki ya EADB kuuza hoteli yake waziri huyo wa zamani.
Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu na Majaji Mohammed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u na William Ouko walijiondoa katika kesi wakisema kwamba wameshutumiwa kwa upendeleo.
‘Kwa hivyo, kila mmoja wetu anajiondoa katika kusikiliza na kutoa uamuzi wa rufaa iliyowasilishwa Aprili 26 2023,’ mahakama ilisema.
Majaji hao walisema ‘walishawishika vikali kwamba kuendelea kushiriki kwetu ‘ katika kesi hiyo hakutatimiza matakwa ya haki, angalau kwa maoni ya Bw Tuju.
Uamuzi huo unakuja siku chache baada ya Kampuni ya Garam Investments Auctioneers kuweka mnadani hoteli iliyo mtaani Karen, mali ya waziri huyo wa zamani.
Kampuni hiyo ya madalali iliweka notisi ya kuuza hoteli hiyo katika tangazo magazetini.
Hii ilikuwa baada ya jaribio lake la kusitisha uuzaji huo, akiteta kuwa hajawahi kupewa notisi ya kisheria chini ya kifungu cha 90 cha Sheria ya Ardhi, kutupiliwa mbali na jaji wa Mahakama Kuu Njoki Mwangi.
Bw Tuju pia alikuwa amepinga notisi ya kuuza mali yake akiteta kuwa benki hiyo ilikuwa ikitaka kurejesha Sh4.5 bilioni, kiasi ambacho kimepita kiasi halisi kwa sababu ya riba.
Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Chama cha Jubilee alienda katika Mahakama Kuu 2023 kusitisha uuzaji huo na pia kupinga uamuzi wa mahakama ya Uingereza, ambao uliidhinishwa na Mahakama Kuu mnamo Februari 2020.
Na baada ya kuruhusiwa kupinga uamuzi wa mahakama ya rufaa, Bw Tuju aliwasilisha ombi la kuwasilisha ushahidi mpya uliopatikana kutoka kwa afisa wa benki, ambao unadaiwa kuunga mkono kesi yake kuhusu mkopo huo uliozua mzozo.
Hata hivyo, ombi hilo lilikataliwa na Bw Tuju akaomba majaji kusitisha kesi hiyo akisema amewasilisha malalamishi katika Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kuhusu jinsi walivyoshughulikia kesi hiyo.
Katika ombi hilo, Bw Tuju na Dari Ltd walishutumu mahakama kwa kushughulikia maombi hayo kwa njia ambayo iliwafanya waamini kwamba majaji walikuwa wamepanga uamuzi watakatoa katika kesi hiyo.
Waziri huyo wa zamani alidai kwamba majaji walikuwa wamepuuza masuala na taratibu ambazo ni muhimu katika rufaa yake.
Katika mzozo huo, kampuni zake za Dari Ltd na SAM Company Ltd zilichukua mkopo mwaka 2015 ili kustawisha na kupanua biashara yake ambayo korti iliamua hakulipa kulingana na masharti.