Makala

Jinsi maisha ya kujiachilia ya madereva wa matrela inavyolemaza vita dhidi ya ukimwi

Na MARY WANGARI November 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

DHANA potovu miongoni mwa madereva wa trela nchini huenda ikahujumu manufaa yanayotokana na mpango wa watu kujipima binafsi virusi vya ukimwi, inasema ripoti mpya.

Kulingana na wanasayansi, madereva Wakenya wa matrela wanasheheni dhana kuwa hatima ya mwanadamu haiwezi kuepukika, hisia kuwa hawana udhibiti wa maisha au afya yao na hali ya kukata tamaa inayoweza kuathiri manufaa yanayotokana na mikakati ya kujipima binafsi HIV (HIVST).

Haya yalijiri baada ya wataalam kugundua kuwa viwango vya kujipima virusi miongoni mwa madereva wa matrela kutoka Kenya, vilishuka katika muda wa miezi sita pekee baada ya kupanda mwanzoni mipango ya HIVST ilipoanzishwa.

Wanasayansi walianzisha utafiti uliokusudiwa kubaini kiini cha vipimo hivyo kushuka, wakitumia mfumo maalum wa Imani kuhusu Afya, kupima vigezo kama vile dhana ya kukubali matokeo ya hatima.

Data iliashiria kuwepo uhusiano mkubwa kati ya dhana ya kujiachilia kwa hatima na mikakati ya kuimarisha vipimo vya HIV vinavyofanywa na mtu binafsi.

Kulingana na wataalam, watu wanaoshikilia dhana kuwa binadamu hawezi kuepuka hatima yake, wana viwango vya chini vya vipimo vya HIV.

Walio na kiwango cha chini kuhusu mtazamo huo, waliashiria kuwa na viwango vya juu vya vipimo vya HIV.

“Ni muhimu kuwepo mikakati ya kisaikolojia na kijamii ili kuangazia mitazamo hasi kwa madhumuni ya kuimarisha manufaa ya vipimo vya watu binafsi kuhusu HIV miongoni mwa waendeshaji matrela Wakenya,” wanasema wataalam.

Wanasema utafiti huu umeangazia umuhimu wa,” kuelewa vizingiti vya kisaikolojia katika utekelezaji wa miradi ya afya miongoni mwa wanajamii wanaokabiliwa na hatari zaidi ya kuambukizwa HIV.”

Aidha, wataalam wanahoji kuwa utafiti umefichua masuala tata yanayoathiri tabia ya kujipima virusi vya ukimwi miongoni mwa wanajamii wanaochangia sehemu kubwa ya mzigo wa HIV.

Wizara ya Afya inaeleza HIVST kama mchakato ambapo mtu hujipima mwenyewe HIV kwa kutumia chembechembe za damu au kutoka mdomoni kama vile mate.

Kando na kuhimiza vipimo vya HIV kwa wanajamii wanaokabiliwa na hatari zaidi ya kuambukizwa gonjwa hilo, HIVST huwapa nafasi, watu ambao kwa kawaida hawangediriki kupimwa, kujipima kisiri na kupata matokeo halisi.

Awali, HIVST ilidhamiriwa kuimarisha vipimo na kuanza mapema matibabu kwa wanaougua HIV.

Ujumuishaji wa HIV kwenye mbinu anuai za matibabu ya kuzuia maambukizi (PrEP) ikiwemo tembe za kumeza na pete zinazowekwa ukeni, ni miongoni mwa mikakati inayokusudiwa kuzuia maambukizi mapya ya HIV.

Aidha, wataalam wanatafiti jinsi ya kutumia HIVST na aina mpya ya PrEP, (inayohusisha kudungwa sindano mara mbili kwa mwaka kila baada ya miezi sita) kama nyenzo ya kupiga vita maambukizi mapya.

Julai mwaka huu, Shirika la Afya Duniani lilitoa mwongozo na kutoa wito kwa mataifa kupanua matumizi ya HIVST PrEP katika juhudi za kuangamzia ukimwi.