Makala

Jinsi Papa Francis alijipalia makaa kwa kulegeza masharti ya kidini

Na CECIL ODONGO April 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

PAPA Francis ambaye aliaga dunia jana, alikuwa tofauti na watangulizi wake akionekana kulegeza baadhi ya masharti makali ya dini ya Katoliki.

Kwa muda ambao alikuwa Papa tangu 2013, alisafiri mara 47 akitembelea zaidi ya mataifa 65 nje ya Italia ambazo ni kilomita 465,000.

Ingawa hivyo, hakurejea kwao Argentina ambako alizaliwa.

Baada tu ya kuingia mamlakani, alikashifiwa na baadhi ya makadinali ambao hawakupendezwa na hatua yake ya kuwakaribisha mashoga ndani ya kanisa Katoliki.

Papa alisema kuwa ushoga haukuwa dhambi na akawaambia kuwa Mungu aliwapenda kisha akawakaribisha makanisani.

Alitekeleza mageuzi makubwa ndani ya Vatican ili kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na marekebisho kwenye mfumo wa matumizi ya fedha.

Alionekana kuwakera baadhi ya makadinali kwa kuwateua wanawake kwenye nyadhifa kadhaa za uongozi.

Ingawa hivyo, alikuwa na wakati mgumu sana kupambana na tatizo la dhuluma za ngono ndani ya kanisa hasa yaliyoshirikisha mapadri na watawa.

Kati ya mambo ambayo hayakupendeza baadhi ya makadinali ni hatua yake ya kuwaruhusu waliotalikiana na wale ambao walioana na hawana cheti cha ndoa kula sakramenti.

Katika sheria za Kikatoliki, waliotalikiana na hawana cheti ya kuthibitisha hilo, hawafai kula sakramenti kwa kuwa wanazingatiwa kama wazinifu.

Papa Francis alipinga hukumu ya kifo akisema haifai kutekelezwa kwa yeyote hata kama ametenda uhalifu wa aina gani. Alikemea kifungo cha maisha akisema hakifai na ni ufasiri tu wa hukumu ya kifo ambayo alisema ni haramu.

Ingawa Papa alipinga matumizi ya mbinu za kisasa za upangaji uzazi, aliwaambia Wakatoliki wasizaane kama ‘sungura’.

Mnamo 2018, Papa Francis aliwaruhusu maaskofu kutoka China waendelee kuhudumu hata kama hawakuidhinishwa na upapa hapo awali.

Pia atakumbuwa kwa kukataa kuidhinisha jaribio la maaskofu kutoka Amerika kumnyima Rais Joe Biden sakramenti kutokana na msimamo wake kuhusu uavyaji mimba.

Papa Francis alisema maaskofu wanastahili kuwa mapadri na si wanasiasa.

Alikashifiwa kwa kutosisitiza marufuku kuhusu uavyaji mimba kama watangulizi wake. Aliwaruhusu wanawake walioavya mimba kanisani.

Pia aliimarisha uhusiano wa Wakatoliki na Waislamu wa dhehebu za Sunni na Shiite huku akipigia upato amani, umoja na mazungumzo kusuluhisha tofauti za kidini.