Jinsi unyunyiziaji maji utaisaidia Kenya mwongo ujao
NA RICHARD MAOSI
Maeneo kame nchini yanaweza kugeuzwa kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula cha kutosha hasa mahindi na mboga, Kenya inapolenga kutimiza ruwaza ya 2030, mojawapo ya ajenda zake kuu ikiwa ni kuzalisha chakula cha kutosha kwa raia milioni 50.
Mabadiliko ya hali ya anga yanayoambatana na ukame usiweka kutabirika ikiwa ndio changamoto kuu, inayowakumba wakulima waliowekeza katika kilimo biashara, miongoni mwa matatizo mengine kama vile miundo misingi duni na kero la mfumuko wa bei ya bidhaa katika masoko.
Mashirika ya kibinafsi pamoja na serikali yanaweza kujizatiti na kuwekeza kwenye miundo misingi ili kuhakikisha kuwa kilimo cha unyunyiaji kinazidi kunawiri, mashinani na maeneo kame.
Akilimali ilipata fursa ya kuzuru Rubi Ranch inayopatikana katika eneo la Naivasha zaidi ya kilomita 60 kutoka kaunti ya Nakuru, ambapo tulikutana na Moses Nduati mtaalam wa kilimo, ambaye alitufichulia namna ya kuongeza mazao kupitia kilimo cha unyunyizaji, katika maeneo ambayo ukame ni jambo la kawaida.
Anasimamia mradi wa kukuza zao aina ya Brocolli , aina ya mboga ambayo kwa mbali utafikiri ni sukumawiki.Anasema kuwa zao la Brocolli linaendelea kupata umaarufu humu nchini, kwanza kutokana na manufaa yake kiafya.
Anasema kuwa zao la Brocolli ni mojawapo ya mazao yanayohitaji maji kwa wingi ili kuhakikisha kuwa vichwa vya aina hii ya mboga maalum vinafikishiwa virutubishi kwa wakati.
Pili wakulima wengi wamenza kuchapukia ukuzaji wa mboga hizi kwa wingi, kwa sababu bei yake ni nzuri sokoni ambapo kichwa kimoja kinaweza kumpatia mkulima shilingi 50 hivyo basi akapata faida ya 25.
Aliongezea kuwa ni kwa sababu hiyo Rubi Ranch iliamua kuwekeza pakubwa kwenye kilimo cha unyunyizaji, kukuza mimea pamoja na kupulizia dawa bila matatizo.
Aliongezea kuwa Brocolli ni aina ya mazao yanayohitaji eneo lenye baridi na angalau saa sita zenye jua, lakini kutokana na unyunyizaji inawezekana kutekeleza haya endapo mpanzi atazingatia mahitaji ya mmea.
Maeneo meng nchini yanayokuza Brocolli yakiwa ni pamoja na eneo la Magharibi mwa Kenya, Bonde la Ufa na eneo la kati ambapo mvua na rutuba ni ya kutosha.
Anasema kuwa siku hizi katika maeneo mengi mvua sio jambo la kutegemewa hivyo basi wakulima waliowekeza katika kilimo biashara, wanahitaji kujihami na njia mwafaka za kujiongezea kipato ili kujiinua kimaisha.
“Kwanza nchi itakuwa katika nafasi nzuri ya kujizalishia chakula cha kutosha bila kuagizia kutoka kwenye mataifa ya nje,” akasema.
Pili kilimo cha unyunyizaji kitasaidia kupambana na changamoto zinazotokana na uhaba wa maji mara kwa mara.
Nduati anasema viungani mwa mji wa Naivasha ni mojawapo ya maeneo yanayopokea mvua haba, na kwa sababu hiyo wakulima wengi wamekuwa wakikadiria hasara kubwa msimu wa kuvuna, mimea yao inapokauka.
Kila msimu wa kuvuna Rubi Ranch ina uwezo wa kupeleka mazao mengi sokoni kiwango cha hadi tani 50 kila msimu, kutokana na kilimo cha unyunyizaji ambacho kimepiga jeki hatua ya kuzalisha mazao.
Nduati anaamini kuwa kilimo cha unyunyizaji kitawafaa wakulima wadogo ambao huzalisha chakula kama vile mboga, kwa ajili ya matumizi ya kila siku bila kutegemea msimu wa mvua mabo wakati mwingine huchelewa.
Aidha unyunyiizaji unaweza kumsaidia mkulima kukabiliana na swala la mmomonyoko wa udongo kwa sababu mkulima anaweza kutumia mfumo wa drip irrigation, ambao ni maji kidogo tu yanayoufikia kila mmea kwa wakati mmoja.
“Kilimo cha mboga na matunda kinaweza kusaidia wakulima wengi kupigana na umaskini kwa kukuza kipato cha familia na kuyaboresha mazingira,”akasema.
Kulingana naye kilimo cha kunyunyiza kinaweza kumsaidia mkulima akatumia sehemu ya ardhi ambayo haiwezi kutumika kwa sababu ya ukosefu wa madini muhimu mchangani na uhaba wa rutuba.
Tatu anasema kuwa kilimo cha unyunyizaji kina manufaa mengi hasa kwa wakulima wanaoendesha kilimo cha miwa, pamba, majani chai na kahawa, ikizingatiwa kuwa wanaweza kusafirisha mazao yao ulaya na kujipatia kipato kizuri baada ya muda mfupi.
Wakati mwingine maji yanayotumika kunyunyizia mimea maji yanaweza kutumika kuzalisha nishati ya kawi ya umeme, inayofahamika kama Hydro Electric Power kwa wakulima wanaoendesha ukulima wa kunyunyiza katika vipande vikubwa vya ardhi.
Pia Nduati anaongezea kuwa unyunyizaji unaweza kuongezea katika hazina ya maji yanayopatikana kwenye ardhi yasije yakapotea ila yatumike kwa manufaa ya baadae, mbali na kuongeza nafasi ya ajira kwa watu wengi wanaofanya kazi kwenye mashamba ya wawekezaji wa kibinafsi kuendesha shughuli mbalimbali.
“Baadhi yao huajiriwa kuendesha mitambo, kupulizia mimea dawa, kupanda, kuvuna ,kupalilia na kusafirisha mimea sokoni,”aliongezea.