• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Jinsi wahubiri wanavyovuka mipaka kwa jina la kukemea pepo

Jinsi wahubiri wanavyovuka mipaka kwa jina la kukemea pepo

NA WANDERI KAMAU

KUIBUKA kwa video ya mhubiri Danson Gichuhi almaarufu ‘Askofu Yohanna’ akimpapasa mwanamke kwa njia tata akidai ‘kumtoa mapepo’ aliyokuwa nayo, kumeibua kumbukumbu kuhusu jinsi ambavyo baadhi ya wahubiri nchini wamekuwa wakivuka mipaka, kwa kisingizio cha kupunga pepo kutoka kwa waumini.

Video hiyo ilizua maswali na hisia mseto nchini, huku Wakenya wengi wakijitokeza kulaani hatua ya mhubiri huyo, wakidai kwamba alimkosea heshima mshirika huyo.

Watu wengi walijitokeza na kuwarai wananchi kutoenda makanisani mwao vivi hivi tu, bila kufahamu kuhusu ikiwa wanatapeliwa kwa kisingizio cha kufanyiwa miujiza

Hata hivyo, mhubiri huyo alijitokeza hadharani na kujitetea kwamba “hivyo ndivyo amekuwa akiwaombea na kuwaokoa washirika wake”.

Mbinu nyingine ambayo wahubiri wamelaumiwa kwa kuitumia, ni kupanga njama na baadhi ya washirika wao kujifanya wamepona baada ya kuwaombea, ili kuwavutia wafuasi wengi zaidi.

Hili liliibuka mnamo 2011, wakati Pasta (marehemu) Michael Njoroge wa kanisa la Fire Gospel Ministries, alijipata pabaya, baada ya mwanamke mmoja kujitokeza na kudai kwamba hakumlipa baada ya kujifanya alipona baada ya kumwombea. Mwanamke huyo, alijitambulisha kama Esther Mwende.

“Namdai Bw Njoroge Sh2,000 tulizoagana angenilipa, baada ya kuwadanganya watu kwamba nilipona baada yake kuniombea. Nimeamua kujitokeza kufichua mbinu anazotumia kuwapumbaza watu  kwani hakunilipa pesa zangu,” akasema mwanamke huyo kabla ya kuaga dunia.

Wahubiri wengine wamekuwa wakilaumiwa kwa kutumia vipindi vya redio na televisheni kupeperusha shuhuda za uwongo za watu wanaodai kupona baada ya kuombewa.

Inadaiwa kuwa baadhi ya wahubiri huwa wana studio zao, ambazo huzitumia kutayarishia vipindi hivyo na shuhuda hizo za uwongo.

Miongoni mwa wale ambao wamefichuliwa kwa kutumia mbinu hiyo ni ‘Nabii’ Victor Kanyari.

Kwenye makala ya kipekuzi yaliyofanywa na shirika moja la habari miaka kadhaa iliyopita, ilifichuka jinsi mhubiri huyo alivyokuwa akitumia baadhi ya washirika wake kwa kurekodi shuhuda za uongo kwenye studio zilizokuwa katika kanisa lake.

Soma Pia: Kanyari: Maisha magumu yalinisukumu kuambia waumini kupanda mbegu ya 310

Licha ya ufichuzi huo, Bw Kanyari alionekana kutojali, badala yake akitaja habari hizo kama “zilizolenga kumharibia jina lake”.

Kando na hayo, wahubiri wengine wamekuwa wakilaumiwa kwa kuwalazimisha wafuasi wao kununua “mafuta ya uponyaji” kwa kutoa kiwango cha juu cha pesa.

Madai hayo yamekuwa yakihusishwa na baadhi ya makanisa yaliyo katika maeneo ya mijini, hasa jijini Nairobi.

Zaidi ya hayo, wahubiri wengine wamehusishwa na sakata za kuwaangusha washirika wao wanapowaombea, ili kuonekana kama kwamba “wameanguka kutokana na nguvu za maombi yao”

Kulingana na wadadisi, mielekeo hiyo inafaa kuizindua serikali kuanza mchakato mkali wa kuhakikisha kuwa makanisa yote yaliyo nchini yamesajiliwa.

  • Tags

You can share this post!

Elimu, kilimo kutengewa fedha zaidi kwenye bajeti ijayo

Zari asema hajaingiza mdudu kwa penzi la Mondi na Zuchu

T L