Jinsi wanandoa wanavyoweza kusaidiana wanapofiwa na jamaa
MAAFA kama vile kifo cha mtoto, mzazi, ndugu, au hata marafiki wa karibu ni jambo ambalo haliwezi kuzuiliwa maishani.
Hata hivyo, athari zake kwa wanandoa mara nyingi huwa kubwa, hasa pale ambapo huzuni na uchungu yanageuka chanzo cha migogoro ndani ya ndoa.
Kifo huacha pengo lisiloweza kuzibwa kwa urahisi. Wengine hujikausha, wengine hulia kila wakati, huku wengine wakijaribu kuendelea na maisha kama kawaida.
Lakini kwa wanandoa, majonzi haya yakikosa kushughulikiwa kwa busara, yanaweza kuvuruga mawasiliano, upendo na hata kuwafanya mtengane.
Mtaalamu wa masuala ya ndoa, Loice Okello, anasema kwamba jambo la kwanza ni kukubali aliyekufa hatarudi tena na hivyo kuomboleza pamoja.
Wanandoa wanapaswa kujikumbusha kuwa wao ni timu moja. Badala ya kulaumiana au kujitenga, wakumbatiane na kutoa nafasi ya kuomboleza pamoja,” anasema.
Ni muhimu pia kuepuka kulazimisha mwenzako kusahau haraka kuwa alimpoteza mtu anayempenda iwe ni ndugu, jamaa au rafiki.
Wanandoa wanafaa kukumbuka kuwa kila mtu ana njia yake ya kushughulikia huzuni. Wengine wanahitaji muda zaidi, wengine wanatafuta ushauri wa kidini au wa kisaikolojia huku wengine wakiamua kujitenga kw muda.
Mke au mume anapaswa kuwa mvumilivu na kumpa mwenzake nafasi ya kujieleza bila kuhukumiwa.
Katika nyakati kama hizi, Loice anasema maombi, imani, na msaada wa kijamii huchukua nafasi muhimu.
“Familia na marafiki wanaweza kusaidia kwa maneno ya faraja, lakini ni jukumu la wanandoa kuhakikisha kuwa huzuni yao haiwataenganishi au kuleta mafaragano kati yao.”
Anaeleza kuwa baadhi ya wanandoa hupoteza mawasiliano baada ya maafa. Kuna ukimya, kutokuelewana, au hata kujitenga kimwili.
Hapa ndipo mazungumzo ya wazi yanahitajika zaidi. “Msemezane kuhusu hisia zenu, kuhusu kumbukumbu za yule aliyefariki, au namna mnavyohisi leo. Hata mazungumzo mafupi husaidia kupunguza machungu moyoni,” anaongeza Loice.
Kando na hayo, wanandoa pia wanaweza kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu.
Zaidi ya yote, wanandoa wanapaswa kukumbuka upendo uliowaleta pamoja. Kumbukumbu za pamoja, maombi, na kufanya mambo wanayopenda kwa pamoja kama kutembea, kusoma Biblia au kushiriki chakula cha jioni vinaweza kusaidia kurejesha amani.
Kumbuka kuwa kifo ni sehemu ya maisha, na hakipaswi kuwa mwisho wa upendo au wa ndoa.