Jinsi ya kulinda afya ya meno ya mtoto
NA WANGU KANURI
Ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha kuwa mtoto wake mchanga anaota meno inavyofaa. Hali kadhalika, sio watoto wengi wadogo huota meno inavyofaa.
Meno ya watoto kubadili rangi yake halisi ambayo ni nyeupe na kuwa rangi ya hudhurungi, kijani kibichi, manjano na wakati mwingine nyeusi huchangiwa na mambo kadha wa kadha.
Kwanza ni kutompiga mswaki mwana wako vyema. Ukoga ama ukipenda uchafu wa meno hubadilisha rangi ya meno ya mtoto wako na kuwa katika rangi ya manjano.
Pili, kumpa mtoto wako mchanga peremende nyingi na vinywaji vilivyo na sukari nyingi kama juisi na soda. Licha ya kuwa vitu hivi hubadilisha rangi ya meno, vinaweza sababisha mashimo katika meno ya mtoto.
Ni vyema kwa wazazi kujua kuwa vitamini zingine zitakazomfaa mwana wako kama madini ya ayoni zinaweza kuyafanya meno ya mwana wako kuwa na madoadoa meusi. Hata hivyo, usisite kumpa mtoto wako vitamini hii kwa kuhofia kuyaharibu meno yake.
Kutumia dawa ya meno iliyo na floridi nyingi. Floridi hii huharibu enameli ya mtoto wako. Tano, mtoto aliyezaliwa na ugonjwa wa ngozi unaoifanya ngozi ya mtoto kuwa ya rangi ya manjano (jaundice) ajapoota meno, meno yake huwa na rangi ya kijani kibichi ama manjano.
Mtoto anaweza kuwa na meno yasiyo na rangi nyeupe kutokana na enameli isiyodhabiti kwa sababu ya chembechembe za DNA alizopata kupitia wazazi wake. Mwisho, mtoto aliyepata majeraha ya meno na mishipa ya damu yake ikavunjika na kutoka damu anaweza iathiri enameli yake.
Isitoshe, mtoto anaweza ota meno yaliyo na rangi ya kijani kibichi ama manjano kwa sababu ya kuwepo na bilirubini nyingi ndani ya damu yake.
Unaweza kuzuia meno ya mtoto wako mchanga kuwa ya rangi nyingine bali na rangi nyeupe kwa; kwanza kuyapiga mswaki meno ya mtoto huyo mara mbili kwa siku.
Pili, kuosha ufizi na meno yake ukitumia pamba hata ingawa meno hayajachipuka bado. Kutompa mtoto wako peremende au vinywaji vilivyo na sukari nyingi.
Kumtembelea daktari baada ya miezi sita baada ya meno ya mtoto wako kuota. Iwapo madini ya ayoni ndiyo sababu ya mtoto wako kuwa na meno yasiyo na rangi nyeupe, hakikisha umepangusa ama kupiga mswaki meno ya mtoto wako baada ya kumpa mtoto wako vitamini hiyo.
Usikubali mtoto wako alale akiwa na chupa chake cha maziwa mdomoni kwani maziwa na sukari hukuza bakteria katika meno ya mtoto wako. Mwisho, tumia dawa ya meno iliyo na upungufu wa floridi mpaka wakati ambapo mwana wako atajua kutema dawa ya meno baada ya kumpiga mswaki.