Jinsi ya kuzuia saratani ya matiti
NA WANGU KANURI
Mwezi wa Oktoba katika kalenda ni mwezi ambao huangazia kwa kina saratani ya matiti. Hospitali nyingi huwarai watu kuzuru na kuchunguzwa iwapo seli zilizoko kwenye matiti yao zinakua na kujigawanya ipasavyo ama la.
Hospitali hizi hutenga siku kadhaa katika mwezi huu ili kuhakikisha kuwa idadi ya wanaougua kansa hii imepungua. Hata hivyo, matibabu ya kansa hii bado yanazidi kuwalemea waathiriwa kutokana na malipo ya juu.
Isitoshe, kupitia Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) changamoto kuu inayosababisha matokeo hafifu ya kuhakikisha kansa hii imezuiwa ni kutoigundua kansa hii miongoni mwa waathiriwa ikiwa haijaenea kwenye titi.
Saratani hii huwaathiri wanawake wengi ikilinganishwa na wanaume duniani. Takwimu kutoka WHO zimeratibu kuwa wanawake milioni 2.1 hupata kansa hii kila mwaka.
Kansa hii husababishwa na kuwepo kwa seli ambazo hazikui ipasavyo kwenye matiti. Seli hizi hujigawanya sana huku zikiongezeka na kuunda donge ambalo husababisha kansa ya matiti.
Hali kadhalika hizi ni njia ambazo mwanamke anaweza kuangaza ili ajue kama anauwezekano wa kuipata saratani hii ya matiti. Kwanza mwanamke ambaye ana kilo nyingi kupita kawaida haswa mwenye uzito wa mwili (BMI) u zaidi ya thelathini.
Pili, iwapo historia ya kifamilia inayoonyesha kuwa mama, dada ama mwana wa ukoo wako amewahi kuipata kansa hii japo hii si sababu kuu kwani kunao walio na kansa hii na hamna historia ya kansa hii kwa familia yao.
Tatu, mwanamke ambaye ana historia ya kansa hii ya matiti hata baada ya kutolewa titi moja, hilo titi lingine linaweza kuipata kansa hiyo. Nne, mwanamke mwenye historia ya ugonjwa wa matiti.
Tano, mwanamke mwenye kufanyiwa matibabu ya mionzi katika kifua chake akiwa mdogo au akiwa mtu mzima anaweza kuwa katika hatari ya kuipata kansa hii.
Isitoshe, mwanamke ambaye anampata mtoto wake wa kwanza akiwa na miaka zaidi ya thelathini yumo katika hatari ya kuipata kansa hii.
Saba kumeza dawa zinazoathiri homoni za mwili haswa zinazochanganya homoni ya estrojeni na projesteroni. Mwisho mwanamke mwenye uraibu wa bia anaweza kuongezea athari za kuipata kansa hii.
Hali kadhalika, wanawake wanaweza kuzuia kupata kansa hii kwa kuchunguzwa matiti kila mara na kumweleza daktari wajapohisi donge katika titi ama matiti yao. Pia hawafai kunywa pombe.
Unafaa kufanya mazoezi siku nyingi za wiki kwa muda usiopungua dakika thelathini. Hakikisha kuwa kilo zako ni nzuri kiafya. Punguza mafuta unayokula kila siku. Mwisho hakikisha unachokula ni chakula bora si bora chakula. Yaani, virutubishi vyote viwepo katika chakula chako.