Jogoo wa jiji alivyozimwa, sasa ajikunyata
RICHARD MUNGUTI NA VALENTINE OBARA
GAVANA wa Nairobi Mike Sonko ni mashuhuri kwa makeke, kujipiga kifua na kutisha kila anayesimama kwenye mkondo wake.
Lakini jana alikuwa mtu tofauti akiwa amejikunyata katika Mahakama ya Milimani jijini Nairobi akionekana mwenye mawazo tele na mnyenyekevu.
Bw Sonko, ambaye amejizolea sifa kama mwanasiasa mwenye makeke yasiyo kifani na mahanjam, alifikishwa kortini muda mfupi baada ya saa mbili unusu asubuhi, akionekana kusononeka na mwenye uchovu bila vito vya dhahabu ambavyo hupenda kuvaa.
Alitulia tuli kizimbani alipokuwa akisomewa mashtaka 19 pamoja na washtakiwa wengine 25 ambao wote walikanusha madai ya ufujaji wa zaidi ya Sh381 milioni.
Ijapokuwa gavana huyo amezoea kuandamana na walinzi na makundi ya watu yakiwemo magenge ya vijana hasa wakati anapokumbwa na mikosi kama ya kuchunguzwa kisheria, jana mambo yalikuwa tofauti.
Polisi walishika doria nje ya Mahakama ya Milimani pamoja na barabara ya Jogoo Road inayoelekea mitaa ya Eastlands, ambapo Bw Sonko ana ufuasi mkubwa, kuzima jaribio lolote la vurugu wakati wa kesi hiyo.
Jumatatu, msafara wake ulikuwa wa polisi pekee kando na mawakili wake na wanasiasa wachache waliojitokeza kumtia moyo.
Vile vile, benchi gumu na chumba cha korti kilichofurika watu zilichukua mahala pa viti vya kifahari na vyumba vikubwa vilivyojaa hewa safi ambavyo gavana huyo hujisifia.
Licha ya mawakili wake kujaribu kumshawishi hakimu amwachilie kwa dhamana, iliamuliwa uamuzi apelekwe rumande hadi kesho atakapotoa uamuzi.
Hata hivyo, huenda akalala hospitalini kwa muda huo kwani Hakimu Douglas Ogoti aliamuru apelekwe hospitalini kuchunguzwa kimatibabu ili ibainike iwapo alivunjwa mbavu alipokuwa akikamatwa.
Alikuwa amedai kupata majeraha hayo wakati maafisa wa polisi waliomtia nguvuni walipompiga katika eneo la Voi mnamo Ijumaa. Bw Ogoti aliamuru ripoti ya hospitali iwasilishwe mahakamani.
Wakili Cecil Miller anayewakilisha Bw Sonko pamoja na zaidi ya mawakili wengine 10, aliwasilisha ripoti ya daktari aliyempima Bw Sonko mnamo Jumapili.
Madaktari wawili, Dkt Esther Nekesa Wafula na mwingine wa Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) walitoa ripoti sawa kwamba alikuwa na majeraha na alihitaji matibabu.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupitia kwa viongozi wa mashtaka James Kihara na Joseph Gitonga hawakupinga kuachiliwa kwa dhamana kwa washukiwa wengine isipokuwa Bw Sonko.
Bw Kihara pia aliomba mahakama izuie Bw Sonko na washukiwa wengine wanaofanya kazi katika Kaunti ya Nairobi kurudi afisini kwa vile watawatisha mashahidi.
“Sawa na jinsi mahakama ilivyowaamuru Magavana wa Samburu (Moses ole Kasaine) na Kiambu (Ferdinand Waititu Baba Yao) wasikanyange tena katika afisi zao, vivyo hivyo Sonko asirudi tena katika afisi yake,” Bw Kihara akaomba mahakama.
Ombi hilo lilipingwa vikali na mawakili zaidi ya 10 wanaomwakilisha Sonko wakiongozwa na Bw Miller. Wengine ni George Kithi, Maseneta Mutula Kilonzo Junior (Makueni), Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na Mbunge wa Makueni Daniel Maanzo.
Bw Kithi alisema Kaunti ya Nairobi haina naibu wa gavana anayeweza kuendeleza shughuli zake ikiwa Bw Sonko atazuiwa kuingia afisini kutekeleza majukumu yake.
“Naomba mahakama itofautishe kati ya kaunti za Samburu na Kiambu. Nairobi haina Naibu wa Gavana. Naibu wa zamani wa Sonko alijiuzulu,” akasema.
Mashtaka yalisema kwamba kati ya Mei 24, 2018 na Machi 28, 2019, washukiwa Sonko, Peter Mbugua Kariuki, Patrick Mwangangi, Wambua Ndaka, Andrew Nyasiego, Samuel Mwangi Ndung’u, Edwin Kariuki Murimi, Lawrence Mwangi Mukuru na wengine ikiwa ni pamoja na makampuni ya Hardi Enterprises Limited na Toddy Civil Engineers, ROG Security Limited, Web Tribe Limited na Yiro Enterprises ambayo mkurugenzi wake Fredrick Odhiambo almaarufu Fred Oyugi, walishiriki ufisadi.
Inadaiwa Bw Sonko alipokea katika akaunti alizofungua kwa majina yake kwenye Benki ya Equity zaidi ya Sh20 milioni kati ya Sh381 milioni zilizofujwa, akijua zimepatikana kwa njia isiyo halali.