Joho anavyootea ngome za Raila kwa urais 2022
Na DERICK LUVEGA
GAVANA Hassan Joho wa Mombasa sasa analenga kupata uungwaji mkono wa kisiasa katika maeneo ya Magharibi na Nyanza anapopania kuwania urais mnamo 2022.
Maeneo hayo yamekuwa ngome ya kisiasa ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga.
Gavana huyo, ambaye anahudumu kwa kipindi chake cha mwisho, ameanza ushirikiano wa karibu na wanasiasa kutoka maeneo hayo ambao walihudhuria hafla ya kumwapisha Bw Odinga kama “rais wa wananchi” mnamo Januari 30 mwaka uliopita.
Wanasiasa hao, ambapo wengi ni vijana, walisema kwamba wamebuni mkakati maalum utakaopelekea kubuniwa kwa chama kikubwa cha kisiasa watakachotumia kushiriki katika uchaguzi huo.
Wakitaja chama hicho kama cha vijana wenye ushujaa, walisema kuwa kaulimbiu yake itakuwa “Kumuunga Mkono Joho.”
Wanaounga mkono kauli hiyo walisema kwamba hawataki kuhusishwa na viongozi “waoga” ambao hawakuhudhuria hafla hiyo. Hata hivyo, hawakuwataja moja kwa moja.
Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, mwenzake wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula na Kalonzo Musyoka (Wiper) hawakuhudhuria uapishaji huo, wakisema kwamba hawakuamini kwamba hilo lingeleta mageuzi ya kisiasa. Viongozi walio katika kambi ya Bw Joho bado hawajawasamehea kwa kukwepa.
Bw Joho alizuru maeneo hayo mnamo Ijumaa na Jumamosi, akiwa ameandamana na baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Pwani.
Kwenye mikutano ya umma waliofanya katika maeneo ya Vihiga na Busia, viongozi hao walisema kwamba Bw Odinga tayari amemtayarisha Joho kutwaa nafasi yake wakati atastaafu kutoka siasani. Viongozi hao pia walikutana na Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o.
Na ingawa Bw Joho alionekana kupigia debe mwafaka wa makubaliano kati ya Rais Uhuru Kenuyatta na Bw Odinga, viongozi wengi waliohutubu walimpendekeza Joho kuwania urais ifikapo 2022.
Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko ndiye alikuwa wa kwanza kumpigia debe alipohutubu katika uwanja wa Mumboha, Luanda, Kaunti ya Vihiga.
“Kauli yetu ni kumuunga mkono Bw Joho na Muafaka wa Maridhiano kati ya mabw Kenyatta na Odinga. Maeneo ya Pwani na Magharibi yanapaswa kufanya kazi pamoja,” akasema Bi Mboko.
Mbunge Maalum, Bw Godfrey Osotsi na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna , waliapa kwamba viongozi vijana wataendesha ajenda yao bila kuwashirikisha viongozi waoga.
“Wiki hii tutaadhimisha mwaka mmoja tangu viongozi wengi, wakiwemo vinara wa NASA walikwepa hafla ya kumwapisha Bw Odinga kutokana na uoga,” akasema Bw Osotsi.
Katika ziara hiyo ya magharibi, Bw Joho alisisitiza kuwa muafaka uliopo utasaidia kuhakikisha usawa katika ugavi wa rasilmali nchini. Pia alitaja kuwa kura ya maamumizi itafanyika karibuni.
“Kutakuwa na kura ya maamuzi kubadilisha sheria kabla ya 2022. Tunataka mjitayarishe kwa sababu itasaidia sauti yenu ipate kusikika katika masuala ya kitaifa,” alinukuliwa kusema akiwa katika shule ya Wasichana ya Butula, Kaunti ya Busia, wakati wa kuchangisha pesa za kujenga bweni.
Wakati huo huo, alipongeza uteuzi wa Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i kuongoza kamati ya maendeleo ya baraza la mawaziri, akisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa siasa katika masuala ya maendeleo, na kutimiza malengo ya muafaka wa Machi 9 kati ya Rais na Bw Odinga.