Makala

Jumbe za vitisho zinavyomkosesha usingizi nyota wa ‘Mali Safi Chito’

Na LABAAN SHABAAN July 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KUNA nyakati anajiuliza maswali mengi bila majibu kwa nini alipinga ushauri wa baba yake.

Baba yake hakutaka ajishughulishe na usanii wa muziki kama njia ya kutega uchumi.

Tangu awe mwimbaji maarufu nchini mnamo Novemba 2023,  Bi Millicent Jerotich, 36, maarufu kwa jina Marakwet Daughter, amesumbuka sana.

Akifichua kuwa alifurahia umaarufu kutoka kwa wimbo ‘Mali Safi Chito’ uliomfanya kutambulika, furaha yake ya ghafla ilidumu kwa wiki mbili tu.

Tangu wakati huo, Marakwet Daughter huangalia nyuma kila wakati kwa hofu ya kushambuliwa.

“Siku hizi ni adimu sana nitoke nyumbani na aghalabu siwaambii mashabiki wangu kuhusu shughuli zangu za burudani nikiogopa mahasimu,” anafichua. “Nimetukanwa tangu Novemba mwaka jana: simu yangu ina jumbe nyingi za vitisho.”

Akizungumza na Taifa Leo kupitia njia ya simu, Bi Jerotich alisinasina akisikitikia maisha yake.

Kulingana naye, mara nyingi, amelazimika kuripoti katika vituo vya polisi ila hajasaidiwa.

“Imebidi nikabiliane na mahasimu hawa bila kuogopa baada ya polisi kunipuuza,” msanii huyu alilalama. “Baba yangu hunipigia simu kila siku kujua kama niko salama.”

Alitutumia moja ya jumbe zilizotishia maisha yake: Futa video mara moja la sivyo uchukuliwe hatua kali.”

Mtumiaji huyu wa mitandao ya kijamii alikuwa anatuma ujumbe kwa Bi Jerotich akimwelekeza kuondoa wimbo Konech Kalya (Kikwangwanga) kutoka kwenye mtandao wa YouTube.

Katika wimbo huu, inafahamika kuwa Marakwet Daughter haombi tu kwa ajili ya amani kati ya jamii zinazozozana za wafugaji kutoka jamii ndogo tofauti za Kalenjin, bali pia kwa nchi nzima.

Lakini wimbo huu ni chanzo cha uhasama kati yake na ‘mashabiki’ wake.

Jumbe za “Lala mahali pema peponi” ni miongoni mwa jumbe za vitisho ambazo amepokea kwa miezi kadhaa.

Aliripoti vitisho hivi katika kituo cha polisi cha Iten na ikanakiliwa katika kitabu cha matukio kwa nambari 20/12/04/23.

“Baadhi ya watu wanaonishambulia wanadai kuwa jamii yetu iliua watu wao wakati wa visa vya wizi wa mifugo,” anafichua.

Alivuma baada ya miaka 15 ya usanii

Ilichukua miaka 15 kwa juhudi za Marakwet Daughter kutamba kimuziki  kuzaa matunda.

Aliimba zaidi ya nyimbo 500 lakini alijulikana tu nyumbani na mashabiki wachache.

Mara tu alipozindua wimbo wa ‘Mali Safi Chito’, mwanamuziki huyu alivuma nchini na ughaibuni.

Kibao hiki sasa kimetazamwa mara milioni 12 katika mtandao wa YouTube.

Kimeibuka kuwa nyimbo pendwa na Wakenya wengi kwa sababu ya umuhimu wake wa kiutamaduni pamoja na mvuto.

Alitamani sana kuvuma katika tasnia ya sanaa, ila hakuwa tayari kwa kilimchomkuta.

Mapato ya muziki

Mwimbaji huyu alikuwa miongoni mwa waliopata pesa nyingi, akitia mkobani angalau Sh100,000 kutokana na malipo ya hivi majuzi ya mirahaba iliyotolewa na Chama cha Hakimiliki ya Muziki Kenya (MCSK).

Tangu wakati huo, amezindua nyimbo nyingi zinazofanya vizuri zaidi kuliko zile zilizotolewa kabla ya umaarufu wake.

Ni pamoja na: ‘No giving up’, ‘Hapana taka’, ‘Promise keeper’, ‘Run your race’ na ‘Sonko teta’.

“Umaarufu huu umeleta taabu nyingi maishani mwangu – sina uhakika wa usalama wangu,” anasema. “Ninatishwa karibu kila wiki. Mmoja wa walionitisha alisema, ‘Nimelipwa ili kukumaliza, lakini ikiwa hutanipa kitu, nitachukua hatua.’”

“Siku hizi, sitembei sana na nimekatisha uhusiano na marafiki wengine… Sikuwahi hata kufikiria kwamba watu hawatakuwa na furaha nikifanikiwa,” Bi Jerotich anaongeza.