Kaa chonjo watoto wasitekwe na sigara za kielektroniki msimu huu wa Sikukuu
ONYO limetolewa kwa wazazi kuwa watoto wao wanaweza kujiingiza katika matumizi hatari ya sigara za kielektroniki ambazo zinazidi kuongezeka ulimwenguni.
Sigara hizi zina mvuke wenye nikotini na ni hatari kwa watoto, asema mtaalamu wa malezi dijitali Simon Mwangi.
Idadi ya watoto wanaolazwa hospitalini kwa sababu ya kuvuta mvuke wa nikotini inaendelea kuongezeka na kutia wasiwasi.
“Hii imefanya wasimamizi wa huduma za afya katika baadhi ya nchi kupinga vikali kampuni za e-cig zinazovumisha bidhaa hizi zilizoongezwa ladha msimu huu wa Krismasi ili kuvutia vijana,” asema.
Tayari Uingereza imetangaza kuwa mwaka ujao itaweka sheria ya kupiga marufuku baadhi ya bidhaa hizo.
Kati ya Aprili na Oktoba mwaka huu, watoto 31 walio nchini ya miaka 18 walilazwa hospitalini Uingereza wakiugua maradhi yanayosababishwa na uvutaji mvuke kutoka bidhaa hizi.
Sigara za kielektroniki zinaweza kusababisha uharibifu wa mapafu na kumletea mtumiaji ugonjwa wa nimonia.
Isitoshe, wataalamu wanasema matumizi ya nikotini kwa wingi huleta kizunguzungu na kutapika.Tafiti zinaonyesha kwamba takriban asilimia saba ya watoto walio na umri wa chini ya miaka 18 — milioni moja — wanavuta au wanajifunza kuvuta sigara za e-cig kwa sababu wana uwezo wa kuzipata.
Mkurugenzi wa matibabu wa Shirika la Kitaifa la Afya Uingereza, Profesa Sir Stephen Powis, akizungumza na gazeti la The Sun alisema:
“Inatisha kulaza zaidi ya watoto na vijana 30 hospitalini kwa zaidi ya miezi saba. Sasa kampuni zinazouza sigara za kielektroniki zinatoa ofa za Krismasi. Zinaweza kuvutia hata watoto wenye umri mdogo ambao wataishia kuzinunua mzazi asipokuwa chonjo.”
Vapes – zinavyojulikana sigara hizo kwa lugha ya mtaa – ni zana muhimu ya kuwasaidia watu wazima waache kuvuta sigara, lakini hazipaswi kutumiwa na watoto walio chini ya miaka 18.
“Hakuna manufaa yoyote ya bidhaa hizo. Madhara yake ni mabaya mno kwa afya ya vijana,” anasisitiza mjuzi wa malezi dijitali Mwangi.