Kampuni ya Wave360 yatajwa kuwa bora katika kukuza vipaji vya wanarika
WAVE 360 Africa imetajwa kuwa miongoni mwa kampuni bora katika kukuza vipaji vya wanafunzi wa vyuo vikuu na kuwaunganisha na mashirika ya kuajiri.
Katika hafla ya kipekee iliyofanyika Nairobi Oktoba 4, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Zedekiah Mukoya alitajwa kuwa bora katika kutoa mafunzo na kuwaunganisha vijana hasa wa vyuo vikuu na mashirika ya kuajiri katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Bw Mukoya pia alihusishwa na mafanikio makubwa yaliyoibadilisha kampuni hiyo na kuwa moja ya mashirika yenye ushawishi mkubwa katika masoko na mawasiliano, ikiaminika na mashirika ya kimataifa, makampuni makuu ya kibiashara na taasisi zinazolenga vijana.
Katika mwaka mmoja uliopita, kampuni hiyo imekuwa ikifanya miradi ya kijamii ikijumuisha uhamasishaji wa jamii kuhusu masuala ya afya kwa ushirikiano na mashirika yasiyo ya kiserikali, pamoja na miradi ya mawasiliano ya kidijitali inayohusiana na Centers for Disease Control and Prevention (CDC).
Bw Mukoya pia ameshiriki kwenye kampeni za kupeleka misaada ya kibinadamu katika nchi zinazokumbwa na ukosefu wa amani kama vile Haiti.

“Malengo yetu ni kujenga uhusiano wa kibiashara, kujenga vipaji, kuunda kizazi cha vijana kinachoweza kujitegemea, na kuongeza uelewa miongoni mwao. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, tumeweza kutembelea vyuo zaidi ya 30 na taasisi za TVET, tukiwafikia wanafunzi zaidi ya 100,000,” alisema Mukoya.
Oktoba mwaka jana, kampuni hiyo ilizindua mpango wa kikuza vipaji vya wanafunzi wa vyuo vikuu na kuwaunganisha na mashirika ya kuajiri.
Kampuni hiyo pia inatoa mafunzo kwa wanavyuo kuhusu umuhimu wa ‘kujiuza’ na kujenga uhusiano mwanafunzi anapokuwa shuleni ili akihitimu mchakato wa kutafuta ajira usiwe mzigo.
Zaidi ya 6000 kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Oktoba 5, 2024 walikutana katika Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta University of Agriculture and Technology (JKUAT) kushiriki katika mpango wa kukuza vipaji na kuwaunganisha na mashirika mbalimbali.
Kwa utaalamu wa mikakati ya masoko ya “Below the Line” (BTL) na “Above the Line” (ATL), kampuni ya Wave 360 Africa inalenga kuunda mazingira jumuishi ya kibiashara yanayonuia kuleta uhusiano halisi na kuweka maslahi ya wanafunzi mbele.
Hadi sasa, Wave360 Africa imefanya kazi na zaidi ya taasisi 30 na kushirikiana na kampuni zaidi ya 40, na hivi majuzi imezindua rasmi huduma zake nchini Uganda.
“Kuwahusisha vijana kunaweza kuchochea uvumbuzi wa kisanii na kuleta suluhu ya kudumu kwani vijana wetu wataweza kujitegemea,” akaongeza Bw Mukoya.