Makala

KASHESHE: Wasafi kaa la moto

October 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na THOMAS MATIKO

MENEJA mpya wa Mbosso Khan wa WCB, kainua zake hata kabla hajaanza kazi kule.

Almah Bronix aliteuliwa kujaza pengo lake Sandra Brown baada ya meneja huyo kujikata akilalamikia malipo duni na kutumiwa vibaya pale WCB.

Hadi anaondoka, alikuwa amemsimamia Mbosso kwa kipindi cha mwaka mzima. Almah alipochukua majukumu, hata hakudumu zaidi ya mwezi mmoja.

Taarifa za uhakika tulizonasa ni kwamba aliamua kujitoa baada ya WCB kumshurutisha aachane na kazi za kampuni yake Bronix Entertainment na kujishughulisha kwa asilimia 100 na majukumu ya WCB.

“Ni jambo ambalo asingelikubali kwa sababu kajenga brandi yake kwa miaka sita na ndio sababu Diamond alipata kumjua na kumfuata ili kumsimamia Mbosso hivyo kumwambia aachane na biashara zake za pembeni, ilikuwa kama dharau. Isitoshe, kumsimamia Mbosso tu hakuwezi kumwingizia mkwanja anaoutengeneza kupitia Bronix Entertainment. Hii ndio sababu ya kujitoa,” chanzo chetu kimeeleza.

Safu hii ilipochonga na mmoja wa mabosi wakuu pale WCB Sallam Mendez, alikanusha lebo hiyo kuwahi kumteua Almah kuwa meneja wa Mbosso.

“Hilo halikuwahi kutokea sema yeye ndiye aliwahi kutangaza kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii. Tulimpa kazi kwa muda wa majaribio akashindwa, hatukuwa tumefikia hatua ya kumpa mkataba,” Sallam akasema.

Kinachoshangaza ni kwamba Almah kaondoka siku chache tu baada ya Harmonize naye kujitoa kwenye lebo hiyo inayoonekana kufanya vizuri.

Wengi waliojitoa WCB wamelalamikia malipo duni na kutumiwa vibaya.