Makala

KAULI YA MATUNDURA: Kasumba kuwa Wapwani wanafahamu Kiswa­hili zaidi kuliko wenzao wa bara imepitwa na wakati

March 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 5

Na BITUNGI MATUNDURA

MAKALA yangu, ‘Waswahili wa Bara: Je, wasomi wa pwani ‘wamepokonywa’ lugha ya Kiswahili na wenzao kutoka bara?’ (Taifa Leo, Oktoba 22, 2009) yaliibua mdahalo baina yangu na msomi na rafiki yangu – Dkt Hamisi Babusa wa Chuo Kikuu cha Kenyatta. 

Makala hayo yalichochewa na matukio ya mwaka huo kwenye maonesho ya kimataifa ya Vitabu ambayo huandaliwa kila mwaka na Chama cha Wachapishaji wa Vitabu cha Kenya (KPA).

Maonesho hayo yalifikia kilele chake kwa sherehe ya kuwatuza waandishi bora wa fasihi – Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta (sasa Text Book Centre Jomo Kenyatta Literature Prize).

Katika kategoria zote za tuzo hiyo zilizowaniwa, vitabu vingi vilivyowa­silishwa na wachapishaji kushindania tuzo hiyo ya kifahari na ya kuhusudi­wa nchini Kenya na Afrika Masha­riki na Kati kwa jumla vilikuwa vya waandishi kutoba bara.

Kwa muda mrefu kumekuwepo na kasumba kwamba watu wa bara ‘hawakimudu Kiswahili’ wanapolin­ganishwa na wenzao kutoka pwani.

“Ingawa uandishi wa fasihi ya Kiswahili ulianza zaidi ya miaka 200 iliyopita wakati Said Abdulla Al Nassir alipoandika Al Inkishafi na Mwanakupona kuandika Utendi wa Mwanakupona ambazo ni kazi zinazoheshimika kisanaa kote ulim­wenguni, inaonekana kwamba watu wa bara wanatoa mchango mkubwa katika fasihi kuliko wenzo wa Pwani,” anasema Prof John Kobia, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Chuka.

Rai ya Prof Kobia huenda ina uk­weli fulani hasa tukiegemea matokeo ya jinsi kazi za Kiswahili zilizowasil­ishwa kung’ang’ania Tuzo ya Jomo Kenyatta ya mwaka huo kwenye katego­ria mbalimbalimbali.

Katika kategoria ya fasihi ya watu wazima, Prof Kyallo Wamitila aliibuka mwandishi bora zaidi kwa riwaya yake Unaitwa Nani? (Vide Muwa). Alifuatiwa na Prof Mwenda Mbatiah kwa kazi yake Vipanya vya Maabara (Jomo Kenyatta).

Wa tatu bora katika kategoria hiyo alikuwa Abu Omar Marjan aliyeandika riwaya ya Kala Tufaha (Phoenix).

 

Kutoka bara

Hawa wote ni waandishi na wasomi wa Kiswhili kutoka bara. Katika kategoria ya fasihi ya wa­toto, Prof Ken Walibora aliibuka kuwa mwandishi bora zaidi kwa kitabu chake Kisasi Hapana (Oxford University Press), akafuatwa na Bitugi Matundura na novela yake, Sitaki Iwe Siri (Longhorn).

Kazi ya Bw A­tibu Bakari, Ngoma za Uchawi (Kenya Literature Bureau) ndiyo iliibuka ya tatu kwenye kategoria ya fasihi ya watoto. Hawa wote pia ni waandishi wa barani.

Mshindi wa pekee kutoka pwani alikuwa ni Prof Sheilla Ryanga am­baye novella yake Dago wa Munje ilishinda nafasi ya kwanza kwenye kategoria ya fasihi kwa vijana.

“Labda itakuwa si haki kamwe kutu­mia kigezo cha utunzi pekee kufikia kauli kama hiyo – kuna na vigezo vingine vingi kwa mfano kuangalia idadi ya wasomi na watunzi wa fasihi kwa Kiswahili na maeneo wanakotoka,”akasema Prof Kobia.

Mtaalamu huyu wakati huo alihisi kwamba, kasumba kuwa wapwani wanakifahamu Kiswa­hili zaidi kuliko wenzao kutoka bara imepitwa na wakati na wala haina mashiko yoyote.

“Kiswahili si mali ya mtu – ni lugha ya mawasiliano, ni raslimali muhimu ya Kenya na Afrika Masha­riki. Kwa hivyo, kuanza kuibuka na imani na mawazo kwamba watu wa maeneo fulani ndio magunge katika Kiswa­hili kuliko wenzao ni kupotosha mambo,”akaongeza Prof Kobia.

Hata hivyo, mwanataaluma huyu alikiri kwamba wataalamu wengi wanaokichangamkia Kiswahili ni kutoka bara. “Kwa kila kikao cha wasomi kumi wa Kiswahili nchini Kenya, aghalabu saba ni kutoka bara,”akadai Prof Kobia.

Prof Kobia alidai kuwa kasumba hii ilivuka mipaka kiasi cha kuwa­fanya Wakenya waamini kwamba Watanzania wanakifahamu Kiswahili sana kuliko Wakenya.

Hali hii ilikita mizizi kwenye mfumo wetu wa elimu ambapo kazi za kifasihi za waandishi kutoka Tanzania ‘zilipendelewa’ zikilin­ganishwa na za waandishi wa nchi hii.

 

Kazi hazikutathminiwa

Ingawa waandishi muhimu nchini kwa Kiswahili kama vile Jay Kitsao, Chacha Nyaigotti Chacha, Katama Mkangi na Alamin Mazrui waliandika kwa Kiswahili sanifu – Kiunguja ambacho pia kinatumiwa na waandishi wa Tanzania, kazi zao hazikuthaminiwa sana,”akasema.

Vitabu vya waandishi kutoka Tanzania vilivyotahiniwa katika mfumo wa elimu nchini kwa muda mrefu ni pamoja na Kinjeketile na Mashetani vya Ebrahim Hussein, Duniani Kuna Watu, Kisima cha Giningi, Siri ya Sifuri, Mzimu wa Watu wa Kale na Mwana wa Yungi Hulewa vya marehemu Muhammad Said Abdulla, Kusadikika, Kufikirika, Utubora Mkulima na Maisha yangu Na Baada ya Miaka Hamsini vya Shaaban Robert.

Vingine vilikuwa ni Kiu na Nyota ya Rehema vya Moham­med Suleiman Mohamed na ‘Sikate Tamaa cha S.A. Mohamed miongoni mwa tungo nyingine za mwandishi huyu. Mhadhiri na mwandishi maarufu wa tamthilia wa Chuo Kikuu Kenyatta Dkt Timothy Moriasi Arege ana maoni tofauti kuhusu suala hili.

“Nafikiri huenda ikawachukua waandishi kutoka bara muda mrefu kutunga kazi zinazofumbata maz­ingira halisi ya Uswahilini – afanyavyo Said Ahmed Mohamed. Isitoshe, watunzi wengi hujipata wamekuwa waandishi wa ‘masafa ma­fupi’ kwa sababu hawachoti wala kuteka hadithi zao katika mazingira maa­lum wanayoyaelewa, ndiposa waandishi wa Tanzania wanatupiku,”anasema.

 

Uandishi bila mpango

Dkt Arege pia anahisi kwamba waandishi wengi wa Kenya – kutoka bara na pwani wanapapia uandishi bila mpango labda kwa sababu ya misukumo mingine tofauti kuliko kuandika sanaa kwa minajili ya sanaa. “Kunapokuwa na misukomo ya kikapitalisti na kushindana kuhusu ni mwandishi gani anayechapisha kazi ny­ingi kuliko mwingine, kuna uwezekano mkubwa wa kuathiri viwango vya fasihi na sanaa kwa jumla,”anasema.

“Waandishi wazuri ni wale wa­naochomoa kazi ambazo zinatoa mchango unaohisika katika taaluma ya fasihi,”anasema. Anatoa mchango wa Chinua Achebe, ambaye riwaya yake, Things Fall Apart ni kazi kuntu ambayo itazungumziwa kwa muda mrefu.

Katika ulingo wa Kiswahili, Dkt Ar­ege anamtaja Mohammed Suleiman Mohamed aliyeandika kazi tatu pekee mathalan Kiu, Nyota ya Neema na mkusanyo wa hadithi fupi, Kicheko cha Ushindi.

“Angalau utakuwa mtovu wa fa­dhila iwapo utataja waandishi wa­zuri wa fasihi ya Kiswahili bila kumtaja huyu,” Dkt Arege. Baada ya kusoma makala yangu, Dkt Babusa aliniandikia barua pepe iliyosoma hivi:

“Hujambo Bwana Bitugi, Mimi nilisoma makala yako leo na ningependa kupinga maoni yako kuwa waandishi au wasomi wa bara wamewapokonya Kiswahili wasomi wa pwani.

 

Uandishi ni kipawa

Kabla ya kufikia msimamo huo ningependa utazame vigezo kadhaa. Uandishi ni kipawa na haimaanishi kuwa ukiwa Mswahili basi waweza kuandika chochote. Pili, ingawa uandishi ni kipawa, kipawa chenyewe chahitaji kukuzwa kwa usomi.

Najua unafahamu vyema kuwa usomi hasa ndio huleta maendeleo kwa eneo lenye usomi huo. Je unajua kuwa watu wa pwani walibaguliwa kiusomi tangu uhuru hadi miaka ya 2000 hivi?

Tazama vizuri: Nieleze kwa mfano ni shule gani ya kitaifa (sekondari) iliyojengwa pwani? Hakuna. Shule zota za kitaifa zimejengwa na kustawishwa bara, wabara wakafaidi masomo ya kiwango cha juu.

Tatu nieleze iwapo eneo la pwani lilikuwa na chuo kikuu chochote kabla ya miaka hii ya 2000. Kulikuwa hakuna. Lakini kulikuwa na vyuo vikuu Nairobi, Central, Kisumu, Nakuru lakini Mombasa ni hivi karibuni ndipo vyuo vinatutumka kutuletea elimu.

 

Fursa

Sitaki kusema kuwa Wapwani hawajasoma lakini mambo kama hayo ndiyo yaliowafungua (akili) wabara mapema na wengi wakakimbilia elimu ambayo ilikuwa milangoni pao. Iwapo wapwani wangepewa nafasi na fursa kama walivyopewa wabara tangu uhuru ulipojiri, kungeibuka waandishi wengi sana.

Kwa hivyo, ni vyema kulinganisha vitu au watu wawili walio na uwezo au nafasi sawa. Maeneo ya pwani na bara hayakuwa na zikuna na nafasi au fursa sawa kabisa. Kwa hayo machache ninegependa kupinga maoni yako. sina mengi asante sana.

Mimi natoka pwani na nawajua vizuri wapwani. Hamisi Babusa. Nami nilimjibu mwalimu Babusa hivi: “Sijambo Shekhe – hofu kwako tu. Asante kwa maoni yako na nafikiri unayosema ni kweli.

Ni furaha kwamba wakati mwingine maandishi yangu yanazua mjadala. Hiyo ndiyo raha yangu kwa sababu mimi ni ‘mchokozi sana’. Ndio hulka yangu lakini huwa sinuii kumuudhi yeyote.

Nilitarajia kwamba ungeandika rejoinder kwenye Taifa Leo maanake ingetoa mchango zaidi kuliko inavyotoa unaponiandikia mimi.” Hata baada ya kumwelekeza Mwalimu Babusa jinsi ambavyo angeandika makala kwa mhariri wa Taifa Leo kuonesha wazi maoni na msimamo wake kuhusu madai yangu ya kuwalinganisha watunzi wa fasihi wa Pwani na Bara, hakulivalia njuga suala hilo. Alighairi.