KAULI YA MATUNDURA: Aina za udhibiti wa maandishi ya kazi za fasihi unaoathiri uandishi na waandishi
Na BITUGI MATUNDURA
JUMA lililopita niliangazia suala la udhibiti wa maandishi (censorship).
Hii ni sifa ya kuyadhibiti maandishi ya kifasihi inayohusishwa na tawala za kimabavu ambazo zinaubana uhuru wa kimaandishi na kusoma. Katika historia ya maendeleo ya fasihi, kuna vitabu vingi ambavyo vimewahi kupigwa marufuku kutokana na sababu za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kimaadili na au kidini.
Riwaya ya kiusasaleo ya Salman Rushdie ya ‘The Satanic Verses’ ilipigwa marufuku kwa sababu za kidini.
Riwaya ya Rosa Mistika (E. Kezilahabi) ilipigwa marufuku nchini Tanzania katika miaka ya 1970s pamoja na Jando na Unyago (J. Mamuya) na novela za D. Maillu kwa sababu zilizodaiwa kuwa za kimaadili.
Kuna mbinu mbalimbali zinazotumiwa na mamlaka na vyombo vya dola katika kutekeleza sera ya udhibiti wa maandishi.
Katika makala haya, tunaangazia takriban aina mbalimbali za udhibiti. Kuzuia ni mbinu itumiwayo ili maandishi yasichapishwe. Kuzuia husitisha maandishi ambayo yanaonekana au kuaminika hayafai kufikia umma au hadhira ya wasomaji. Aidha serikali au kundi fulani linalotetea au kudumisha maslahi fulani hutekeleza aina ya pili ya udhibiti. Aina hii ya udhibiti wa maandishi mara nyingi huhusu afisi au asasi fulani ya serikali, kundi la kidini huwa na mamlaka lenye kumiliki vyombo vya habari au mashirika ya uchapishaji.
Vilevile, kuna mbinu ya kuharibu: Aina hii ya udhibiti huhusu kuharibu vitabu na maandishi mengine kabla au baada ya kuchapishwa ili kuzuia vitabu au maandishi hayo kufikia umma au kuchapishwa upya. Hili hutekelezwa kwa kuteketeza maandishi au kuchanachana kazi husika. Mbinu hii iliwahi kutumiwa na serikali ya Kenya dhidi ya Kampuni ya Uchapishaji ya East African Educational Publishers iliyokuwa inataka kutoa kitabu cha Ngugi wa Thiong’o kiitwacho ‘Matigari ma Njiruungi’ (1987).
Usimbaji (Encryption) pia ni mtindo wa udhibiti ambapo maandishi hudhamiriwa kufikia hadhira au kundi fulani la wasomaji wachache, hasa kwa kubadilisha lugha na kufanya maandishi kuwa magumu kusomeka au kuchochea kimakusudi hamu ya kutosoma kwa kundi fulani nje ya lile linalolengwa na maandishi husika. Kwa mfano, vitabu vingi vya zamani na majarida kuhusu taaluma ya utabibu viliandikwa kwa Kilatini. Ingawa hili lilifanywa kwa sababu kadha, mojawapo ya maelezo ya kimsingi kuhusu hali hiyo ilikuwa ni kuyafanya maandishi hayo yasiwafikie watu wengi, bali kuhakikisha kwamba ni watu wachache waliochukuliwa kuwa wa hadhi na viwango fulani vya elimu ndio wangeweza kusoma maandishi hayo.
Katika uhawilishaji (omission), sehemu au maelezo fulani katika kazi fulani ya kifasihi ambayo yanafikiriwa kuwa hayafai huondolewa kabla ya kazi fulani kuchapishwa. Mbinu hii mara nyingi huweza kuathiri matini asilia. Mbinu hii huruhusu tu kuondolewa kwa kiasi fulani cha matini kwa msingi kwamba kuondoa sehemu kubwa ya matini kunaweza kufanya kazi au maandishi kutoweza kusomeka kwa sababu ya kuvurugika.
Halikadhalika utakasaji ni aina ya udhibiti inayohusu kuacha nje au ‘kutakasa’ matini si tu kwa kuondoa, bali pia kubadilisha maneno, sentensi au sehemu, aya au hata sura za matini iliyokwisha kuchapishwa. Hivi majuzi, kitabu kinachoitwa ‘Blood Ties’ kilichoandikwa na mwandishi wa Afrika Kusini, Zimkitha Mlanzeli kiliondolewa kwenye maduka ya Text Book Centre jijini Nairobi mnamo Septemba, 2019 kwa madai kwamba kilitumia lugha ‘chafu’.
Udhibiti wa kiubunifu huhusisha uandishi upya matini na wadhibiti wenyewe na kubadilisha matini kabisa kiasi kwamba wadhibiti wanaweza kuwa waandishi wenza.
Kuna pia udhibiti wa kutoa kwa orodha ya kupiga marufuku.