KAULI YA MATUNDURA: Athari ya lugha za kigeni kwa Kiswahili
Na BITUGI MATUNDURA
MOJAWAPO ya vipengee muhimu ambavyo mwalimu na mwanafunzi wa isimujamii anahitajika kujua ni historia ya Kiswahili.
Katika kuangazia historia ya lugha hii muhimu ya Afrika Mashariki na Kati, mwalimu na mwanafunzi wake hawawezi kukwepa suala la jinsi Kiswahili kimeathiri na kuathiriwa na lugha nyingine.
Katika makala haya, ninaangazia jinsi wageni kutoka nje ya bara la Afrika walivyochangia katika kuathiri Kiswahili.
Athari ambazo hujitokeza wazi kwenye mada kama hii angalau huwa ni ya kileksikoni au msamiati.
Miongoni mwa wageni wa awali kabisa kuwasili katika pwani ya Afrika Mashariki walikuwa ni pamoja na Waajemi, Wafursi, Wamisri, Wachina na Waarabu.
Utafiti wa akiolojia au historia chimbo umeonyesha kwamba vyungu vya Wachina, maandishi ya Wamisri na hata athari za wageni wengine kwa wakazi wa pwani bado zingalipo.
Baadhi ya wageni hawa walipiga kambi na kuishi pwani ya Afrika Mashariki mapema mwaka 900 Baada Kristo.
Wageni hao ambao walihamia pwani ya Afrika Mashariki kwa sababu wanazozijua wao wenyewe waliishi katika eneo hilo na kufunga ndoa na wenyeji wa sehemu hizo.
Wanavyosema Chiraghddin Shihabuddina na Mathias Mnyampala katika ‘Historia ya Kiswahili’, wahamiaji hao walichangia katika kupanuka na kukua kwa miji ya mwambao ya Washwahili kama vile Pate, Lamu, Mombasa, Kilwa, Vumba, Pemba na Zanzibar.
Wajukuu wa Waarabu wengi pamoja na Waajemi chambilecho Abdalla Khalid walisahau lugha zao baada ya muda mrefu na kuanza kutumia Kiswahili.
Mezwa
Hali ambapo lugha za baadhi ya wahamiaji hao ‘ilimezwa’ na lugha ya wenyeji wa mwambao kimsingi ilitokana na uchahe wao.
Hata hivyo, Kiajemi au Washirazi kutoka Irani walipokeza Kiswahili maneno mengi ambayo yanapatikana katika lugha hii hadi wa leo.
Himaya ya Shirazi na makazi yao kuanzia Kisiwa cha Funzi kusini mwa pwani ya Kenya hadi Tanga na Bagamoyo nchini Tanzania ingali inatambulika ingawa si kwa njia ya kinaga ubaga hivi leo.
Washirazi walitofautishwa na wakazi wengine wenyeji wa pwani kama vile Wadigo na Wasegeju kwa sababu ya jinsi walivyoishi maisha yao kijumla.
Walitegemea uvuvi na kutumia lahaja ya kipekee ya Kiswahili iliyojulikana kama Chichifundi.
Washirazi waliathiri leksikoni ya Kiswahili katika mianda mbalimbali.
Mianda na nyanja hizo ni pamoja na utawala ambapo tunapata maneno kama vile jumbe, diwani, amir, waziri, serikali, shehe, akida na Sultan.
Katika mwanda wa biashara, Washirazi walichangia maneno kama vile tajir na bakshish ambayo yameswahilishwa na kuwa tajiri na bakshishi. Kwenye mwanda wa uchukuzi kwa vyombo vya majini tunapata maneno kama vile bandali,nanga, tezi na kadhalika.
Katika taaluma ya mimea, Washirazi walichangia maneno kama vile mbangi, mbilingani, mdengu, mgulabi, mharagwe, mpopo, mtambuu, mnansi, mdalasini na derabi.
Kuhusu vyakula, walichangia maneno kama birinzi, borohoa,gubiti, sambusa na siki.
Msamiati wa mavazi, mapambo na rangi waliochangia ni pamoja na lasi, seredani, utaji, urujuani, zari, zumaridi na rangi.
Aidha kwenye taaluma ya ujenzi walichangia maneno kama vile dari, boma,ghala, roshani. Maneno mengine ni pamoja na bahati, beluwa, usafidi, huruma, hoihoi, uhanithi, ushenzi, barabara miongoni mwa mengine.
Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka
Baruapepe ya mwandishi: [email protected]