KAULI YA MATUNDURA: Kanuni za Kudumu za Bunge hazitasaidia sana ikiwa Baraza la Kiswahili la Kenya halitaundwa
Na BITUGI MATUNDURA
MNAMO Novemba 12, 2020, kwenye hafla ya Hotuba ya Rais Kwa Taifa, Rais Uhuru Kenyatta alizindua tafsiri ya Kiswahili ya Kanuni za Kudumi za Bunge kutimiza mahitaji ya Katiba ya Kenya ya mwaka 2010.
Kwa mujibu wa Katiba hiyo, Kiswahili ni lugha ya taifa na rasmi – sambamba na Kiingereza. Hatua ya uzinduzi huo ilipiga jeki mambo mawili.
Kwanza, ilionesha kwamba Kiswahili kinaendelea kukuzwa Kimakusudi nchini Kenya. Kwa muda mrefu, lugha hii imeachwa ijitafutie mkondo wake. Pili, uzinduzi huo utakivusha Kiswahili hadi ng’ambo ya pili katika kuhakikisha kwamba suala la Sera ya Lugha nchini Kenya – hususan kiutekelezaji linatiliwa maanani. Kwa nini? Kwa sababu masuala ya maendeleo na ustawishaji wa lugha yanafungamana mno na siasa.
Licha ya kuisherehekea hatua hii, ni muhimu kukumbuka kwamba Kenya bado haina Baraza la Kiswahili la Kenya (BAKIKE). Je, kuna faida gani kuwa na Baraza la Kiswahili nchini Kenya? Tangu 1967, Tanzania imekuwa na vyombo vingi vinavyofadhiliwa na serikali. Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) liliundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 27 ya mwaka 1967. Kutokana na sheria hiyo, Baraza hilo linaratibu na kusimamia asasi zote na mawakala wote wanaokuza Kiswahili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Majukumu yake kama yalivyofafanuliwa na Sheria hiyo ni pamoja na: Kuratibu na kusimamia maendeleo ya Kiswahili nchini Tanzania, kushirikiana na vyombo vingine nchini humo vinavyojihusisha na maendeleo ya Kiswahili na kuratibu shughuli zao, kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli rasmi na za kawaida na kushirikiana na mamlaka zinazohusika zinazohusika kuthibitisha tafsiri sanifu za istilahi.
Majukumu mengine ni pamoja na kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa serikali, mashirika ya serikali na yasiyo ya serikali na asasi nyingine, kuchapisha jarida au toleo linalohusu lugha na fasihi ya Kiswahili, kushirikiana na mashirika ya kitaifa, asasi na watu binafsi, kufuatilia, kushauri na kusimamia shughuli zinazolenga kukuza Kiswahili na kushirikiana na mashirika mengine ya kitaifa na kimataifa kusimamia utafiti unaohusu Kiswahili nchini Tanzania.
Vilevile, Baraza hilo hutoa ushauri kwa waandishi na wachapishaji ili watumie Kiswahili fasaha mbali na kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuidhinisha vitabu vinavyotumika shuleni na vyuoni kabla havijachapishwa.
Muundo wa kiutawala wa BAKITA ni kwamba, kuna idara tano; nazo ni idara ya uhariri na uchapishaji, Idara ya Lugha na Fasihi, Tafsiri na Ukalimani, Istilahi na Kamusi na Idara ya Uhusiano. Idara hizi zote hufanya kazi kwa ushirikiano. Idara ya Istilahi na Kamusi kwa mfano hufanya utafiti wa istilahi zinazotakiwa kusanifiwa na Kamati ya Kusanifu Lugha (KAKULU). Idara hii pia huandaa orodha ya istilahi zinazosanifiwa na KAKULU na kuidhinishwa na Baraza, kuandaa istilahi sanifu kwa ajili ya kuchapishwa katika matoleo ya Tafsiri Sanifu na kufuatilia matumizi yake, kuandaa Kamusi kwa matumizi ya asasi, shule na watu wa aina mbalimbali na vilevile kutoa ufafanuzi wa istilahi kwa wanaoihitaji.
Nchini Kenya, shughuli ya kubuni, kusanifisha, kusawazisha na kusambaza istilahi mpya za Kiswahili limeachiwa watu binafsi na vyombo vya habari. BAKIKE hivyo basi itatoa mwongozo katika maendeleo ya Kiswahili.