KAULI YA MATUNDURA: Mazingira ya kisiasa na kiuchumi katika riwaya ya 'Haini' yake Shafi Adam Shafi
Na BITUGI MATUNDURA
HII ni awamu ya nne ya makala kuhusu riwaya ya ‘Haini’ iliyoandikwa na Shafi Adam Shafi.
Mnamo 1982, mtaalamu Farouk Topan alidai kwamba watunzi muhimu wa riwaya ya Kiswahili walikuwa ni Mohamed Suleiman Mohamed na Euphrase Kezilahabi.
Zaidi ya miongo mitatu, madai ya Topan hayana mashiko tena kwa sababu tangu miaka hiyo tumeshuhudia waandishi wengi wa riwaya ya Kiswahili wakijitokeza na kuandika sana.
Mpaka sasa, tuna wanariwaya wapevu kama akina Shafi Adam Shafi, Mwenda Mbatiah, John Habwe, Kyallo Wamitila, S.A. Mohamed, Ken Walibora, Omar Babu miongoni mwa wengine.
Tulivyokwisha kutaja, riwaya ya ‘Haini’ ni mojawapo wa riwaya za mwandishi Shafi Adam Shafi.
Riwaya za mwandishi huyu: ‘Kasri ya Mwinyi Fuad’ (1978) na Kuli (1979), zinaakisi kwa kiasi kikubwa maudhui ya mapinduzi kisiwani Zanzibar yaliyotokea mnamo mwaka wa 1964.
Mapinduzi haya yaliondolea mbali utawala wa Kisultani na kubadili kwa kiasi kikubwa, mfumo wa uzalishaji mali visiwani humo. ‘Haini’ pia inaakisi tukio la kihistoria; kuuawa kwa Rais wa Zanzibar Abeid Amri Karume mnamo mwaka wa 1972.
Kufuatia mauaji hayo, watu wengi wasiokuwa na hatia walisakwa wakakamatwa na kutiwa gerezani kwa kutuhumiwa kuwa mahaini.
Mwandishi amelitumia tukio hilo kuwa kiini cha kuyachunguza matatizo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya nchi za Kiafrika baada ya uhuru. Maudhui yanayotawala katika kazi nyingi za waandishi wa Zanzibar kipindi hicho – mathalan Mohamed Suleimani Mohamed, Said Ahmed Mohamed ni ya kimapinduzi. Katika mapinduzi haya, utawala wa Sultani uling’olewa mamlakani na Waafrika walio wengi wakashika hatamu za uongozi.
Zanzibar ikawa Jamhuri chini ya uongozi wa Amri Abeid Karume. Katika ‘Haini’, mwandishi anamulika historia hii ya Zanzibar kutoka mbali anaposawiri sifa za Chopra, mwendesha mashtaka wa serikali. Anasema: “Jinsi alivyokuwa bingwa wa kazi yake hiyo, aliaminiwa sana na mahasimu wote watatu waliokitawala kisiwa cha Zanzibar.”
Wakati wa Elizabeth wa pili aliaminiwa sana na watawala wa Kiingereza na utiifu wake kwa watawala hao ukawa ni wa kupigiwa mfano. Sultani na wafuasi wake walipofanikiwa kuundoa utawala wa Elizabeth wa pili na kuweka utawala wao, nao pia wakawa na imani kubwa na Chopra wakamfanya kuwa ndiye mshauri wao mkuu wa mambo ya kisheria […] wakwezi na wakulima walipokuja juu wakamtimua Sultani na wafuasi wake kwa mapanga na mashoka na Kigogo akashika usukani wa kuiongoza nchi, Kigogo hakumwona mwanasheria aliyekuwa na kipawa kumshinda Chopra, akambandika cheo cha mwanasheria mkuu wa serikali.” (uk 230 – 231) Amri Abeid Karume aliuawa mnamo mwaka 1972.
Taifa la Zanzibar likashuhudia kilele cha ukiukaji wa haki za kibinadamu katika kile watawala walichokiita ‘usakaji wa mahaini’, wauaji wa Karume. Watu wengi waliteswa, wengi wakauwawa na wengi walifungwa gerezani kwa shutuma za kushiriki mauaji ya Karume.
Taifa likawa kama gereza. Hili ndilo tukio ambalo mwandishi analimulika katika ‘Haini’.
Riwaya ya ‘Haini’ inatufungulia milango ya mazingira yaliyojaa hofu na wasiwasi. Raia wanasakwa, kukamatwa na kutiwa gerezani kwa kosa ambalo wengi wao hawalifahamu.
Sehemu kubwa ya riwaya hii, inasimulia matukio ya gerezani ambamo Hamza pamoja na watuhumiwa wengine wamerundikwa, kuteswa, kuthakilishwa na kutendewa unyama wa kila aina. Hamza na wenzake hawana budi kuumia huku wakiwa hawajui hatima yao.
Wanateswa ili wakiri kwamba walihusika. Baadhi yao hawana budi kufanya hivyo ili kuokoa roho zao. Mkadam, Haramia, Mpakani, Sumbu, Marzuku, Vingosho, Zarkani, Pwacha na Kuchi wanakiri kuhusika kwao. Wanatungiwa visa na ushahidi wa uwongo wa kuwahusisha wale wengine.