Makala

KAULI YA MATUNDURA: Ni kweli neno ‘mzungumzishi’ halifai kwa maana ya‘spika’ lakini seneta Zani ana hoja

July 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BITUGI MATUNDURA

JUZI JUZI seneta maalumu, Dkt Agnes Zani, alimtaja Spika wa Bunge la Seneti Bw Ken Lusaka kuwa ‘mzungumzishi’ kwa maana ya spika ambao ni msamiati uliozoeleka.

Maseneta wengine, wakiongozwa na James Orengo walipinga vikali istilahi hiyo kwa misingi kwamba katika historia ya midahalo bungeni, dhana hiyo kamwe haijawahi kusikika.

Dkt Agnes Zani ni ‘Mswahili’ kindakindaki na binti ya walimu na waandishi mahashumu – Bwana Zachariah M. Zani na Teresa K. Zani.

Kadhalika, Dkt Zani ni msomi wa sosholojia ambaye alipata shahada yake ya uzamifu (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha Oxford mbali na kuwa mhadhiri wa vyuo vikuu kabla ya kujitoma katika siasa.

Kutokana na rai alizotoa, ninaweza kudai kwamba Dkt Zani alinivutia kuwili.

Kwanza, alionesha raghba ya kukitetea Kiswahili liwe liwalo. Pili, mkabala wake wa kutumia neno ‘mzungumzishi’ badala ya ‘spika’ ulinikumbusha mkabala wa mwanaleksikoni maarufu wa Kiswahili, marehemu Mzee Ahmad Sheikh Nabhany wa Mombasa wa ukuzaji wa Kiswahili mumo kwa mumo.

Nadharia ya Mzee Nabhany kuhusu upanuzi wa leksikoni ya Kiswahili ni kwamba; kabla ya kukopa na au kutohoa neno au msamiati kutoka lugha za kigeni, ni muhimu tupekuepekue katika lahaja za Kiswahili na lugha nyingine za Kibantu iwapo kuna neno au dhana inayoweza kutumiwa kuelezea neno au dhana tunayotaka kuikopa.

Nadharia ya Mzee Nabhany inalenga kuepuka ukopaji kiholela kwani kwa kuruhusu hili Kiswahili kinaweza kupoteza upekee wake.

Kwa hivyo, katika kusisitiza kwamba neno ‘mzungumzishi’ litumiwe badala ya ‘spika’, Dkt Zani ana hoja nzito ambayo inapaswa kuungwa mkono.

Lakini je, Kiswahili kina ufukara wa msamiati unaoweza kuchukua nafasi za ‘mzungumzishi’ na ‘spika’? Neno ‘spika’ limetoholewa kutokana na neno la Kiingereza Speaker.

Maana ya kileksika ya spika ni: Mtu anayeongoza majadiliano bungeni; mwenyekiti wa bunge au baraza la wawakilishi.

Msamiati mwingine wa Kiswahili sanifu unaoleta fahiwa inayokaribiana na ‘uspika’ ni ‘longa’ au ‘sogoa’.

Kwa hiyo, seneta Zani hangejipata matatani sana iwapo angependekeza kwamba spika aitwe ‘mlongaji’ au ‘sogoa’ badala ya ‘mzungumzishi’.

Hata hivyo, mdahalo wa seneta Zani na maseneta wengine unatutosa kwenye suala la upanuzi wa leksikoni katika lugha na njia zinazotumiwa na wanaleksikolojia katika kupanua msamiati wa lugha fulani.

Ikumbukwe kwamba lugha hukua kila uchao na hupanuka ili kukidhi haja za maswailiano ya kawaida na katika njanya maalumu.

Lugha hulazimika kupanua msamiati wake pale inapohitajika kushughulikia mawasiliano katika nyanja mpya ambazo awali zilikuwa hazishughulikiwi kwa lugha hiyo.

Hivi sasa, nyanja zinazozishinikiza lugha kupanua mawanda ya kimawasiliano ni maendeleo ya kasi katika sayansi na teknolojia.

Baadhi ya mikabala inayotumiwa katika kupanua leksikoni za lugha mbalimbali ulimwenguni ni pamoja na ‘ukopaji’ au utohozi, uhulutishaji, kubuni maneno mapya kwa kuangalia maumbile na utendakazi wa dhana au kifaa kinachohitaji neno au istilahi, kutumia vifupisho miongoni mwa njia nyingine.

Kwa hivyo, juhudi za Dkt Zani katika kupanua leksikoni ya Kiswahili hazipaswi kupingwa – bali kuungwa mkono. Ingawa hakutia fora katika mdahalo wa kutetea msamiati wake kilio chake na ari yake ya kukitetea Kiswahili ilionekana bayana.