Makala

KAULI YA MATUNDURA: Ni kweli Nyerere alikuwa tapeli wa tafsiri za tungo za William Shakespeare?

October 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BITUGI MATUNDURA

KATIKA ulimwengu wa taaluma, aghalabu huibuka mtu mmoja katika kizazi kizima ambaye mchango wake huwashangaza na kuwafanya watu wengi waajabie michango ya watu hao.

Nchini Uingereza, watu bado wanaajabia upeo wa tungo za mwanatamthilia William Shakespeare ambaye taathira ya tamthilia zake ingali inaonekana takriban mpaka sasa zaidi ya miaka 400 tangu alipoishi, na kutunga na kufa. Shakespeare yadaiwa alitunga tamthilia 36.

Huku Afrika Mashariki, wataalamu wa Kiswahili wanadadisi iwapo Muyaka bin Hajji Al- Ghassaniy ndiye aliyetunga mashairi yote yanayodaiwa kuwa yake.

Je, mbona ni Muyaka pekee aliyetukuka ilihali kulikuwa na malenga wengi wakiwemo kina Ali Koti ambao walitunga katika mazingira sawa na Muyaka?

Kuna uwezekano kwamba baadhi ya mashairi yaliyokwisha kupigwa muhuri kuwa kayatunga Muyaka ni ya akina Ali Koti? Mnamo mwaka 2000, msomi Prof Tigiti Sengo wa Tanzania aliibuka na madai ya kushangaza kuhusu Hayati Rais Julius Kambarage Nyerere na tafsiri ya tungo za William Shakespeare kwa lugha ya Kiswahili.

Katika mojawapo ya mihadhara yake minne ya umma katika Chuo Kikuu cha Egerton, Prof Sengo aliishangaza hadhira yake kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa tapeli na mwongo kuhusu tafsiri ya tungo hizo. Alidai kwamba tungo ‘za Shakespeare’ ambazo zimewahi kuzua mtafaruku na mjadala kuhusu mtunzi wake halisi – Mabepari wa Venisi, Juliasi Kaizari na Makbeth – ambazo yadaiwa zilitafsiriwa na Julius Nyerere – kwa hakika zilikuwa tafsiri zilizofanywa na Abdillahi Nassir.

Kwa mujibu wa Sengo, ‘wizi’ huu ulitekelezwa kwa kupanga na kula njama na kampuni ya uchapishaji ya Oxford University Press. Chambacho Tigiti Sengo, baada ya kulipachika jina la Julius Nyerere kimakusudi kuwa yeye ndiye mtafsiri, waliweka jina la mfasiri halisi; Abdilahi Nassir, kuwa ndiye mhariri.

Sengo alidai kwamba mambo hayakukomea hapo. Alidai kuwa baadhi ya kazi zilizoandikwa katika Kiswahili na kuaminika kuwa za Mwalimu Nyerere pia ni za ‘wizi’.

Kwa hiyo, Prof Sengo alisema kwamba sifa alizopewa Mwalimu Nyerere ambaye ndiye Mwanzilishi wa Taifa la Tanzania kuhusu ufanisi huo zilikuwa si za haki.

Anadai kwamba mwelekeo wa Nyerere kuhusu Kiswahili haukuwa na ukereketwa wa haja na kwamba alichofanya Nyerere ni kukidaka Kiswahili kwa manufaa yake kisiasa.

Sengo alidai kwamba kuna Watanzania ambao walikikumbatia na kukikuza Kiswahili na pindi kilipotia fora, wanasiasa kama Nyerere ‘wakakinyakua’ na kudai kwamba wao ndio watetezi sugu wa lugha hiyo.

Ni kwa nini suala la Nyerere na ‘wizi’ wa tafsiri za Shakespeare ni muhimu? Kwanza, kuna halaiki kubwa ya watu kote duniani waliokwisha kuzisoma tafsiri za Shakespeare kwa Kiswahili zinazodaiwa kuwa za Nyerere.

Wasomaji hao wamekwisha kumwonea fahari Nyerere kwa kazi hiyo. Sijui iwapo wachapishaji wa tungo hizo wanaweza kutoa taswira na habari kamili kuhusu suala hili.

Kuna uwezekano pia kwamba wachapishaji walifanya hivyo kimakusudi kama mbinu ya kisiasa ya kuimarisha mauzo ya vitabu vyao.

Prof Sengo si msomi hivi hivi na hivyo basi madai yake hayawezi kupuuzwa. Lakini pia ni muhimu kukumbuka kwamba, Sengo alipaswa kutoa madai hayo Mwalimu Nyerere akiwa angali hai ili aweze kujitetea. Prof Sengo alizaliwa Morogoro mnamo mwaka 1945.

Alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Idara ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Amendika kazi nyingi zikiwemo Ndimi Zetu, Hisi Zetu, History of Kiswahili Poetry (kwa ushirikiano na Mugyabuso Mulokozi, Fasihi Simulizi ya Mtanzania miongoni mwa tungo nyingine.

 

[email protected]