KAULI YA MATUNDURA: Tathmini ya ufaafu wa istilahi ‘runulishi’ kwa maana ya Smartphone – Sehemu ya 2
Na BITUGI MATUNDURA
KATIKA awamu ya kwanza ya makala yangu juma lililopita, niliangazia mdahalo wa wataalamu kuhusu istilahi ‘runulishi’ iliyopendekezwa na mwandishi na mhariri Geoffrey Mung’ou ili itumike kwa maana ya ‘smartphone’.
Nilidai kwamba maendeleo ya sayansi na teknolojia na taaluma nyingine zinahitaji istilahi mahsusi. Nilidai pia kwamba juhudi za watu binafsi kama vile Geoffrey Mung’ou katika kubuni istilahi hazipaswi kupingwa – bali kuungwa mkono.
Hata hivyo, nilitahadharisha kwamba shughuli ya kubuni istilahi ni nzito na inayofaa kufuata mchakato au mkondo fulani unaokubalika ili lugha iweze kuwa na istilahi faafu na kuepushwa kuvurugwa.
Baadhi ya wanaleksikoni wapevu nchini Kenya ambao wamekibunia Kiswahili istilahi zinazokubalika ni Mzee Sheikh Nabhany, Prof Rocha Mzungu Chimerah na Prof Kyallo Wadi Wamitila wa Chuo Kikuu cha Nairobi.
Vyombo vya habari kama vile Shirika la Habari la Taifa la Kenya (KBC) na Taifa Leo pia vimetoa mchango wa kupigiwa mfano katika kubuni na kusambaza istilahi za nyanja maalum kama vile tiba, sheria na teknohama.
Baada ya kuichunguza kwa makini istilahi ‘runulishi’ aliyoibuni au kuipendekeza Bw Mung’ou, nilihisi kwamba ilikuwa ni istilahi nzuri ambayo ilipaswa kupigwa msasa, ikaboreshwa na labda kuingizwa katika matumizi ya kila siku ya Kiswahili. Kwa hiyo, mimi nilipendekeza kwamba Bw Mung’ou aibadilishe istilahi yake iwe ‘rununulishi’ badala ya ‘runulishi’. Sababu zangu ni pamoja na zifuatazo: Kinadharia, istilahi ‘runulishi’ inatokana na uhulutishaji au uunganishaji wa maneno ‘rununu’ na ‘tarakilishi’.
Kiunzi
Fikra za mwandishi Mung’ou hivyo basi zilijikita kwenye kiunzi alichokiegemea Prof Rocha Chimerah katika kubuni istilahi ‘tarakilishi (tarakimu + akili + mashine). Mung’ou alifafanua kwamba umbo na utendakazi wa ‘smartphone’ unakurubiana mno na tarakilishi. Kwamba ‘smartphone’ ina uwezo wa kufanya na kutekeleza mambo ambayo tarakilishi au kompyuta inaweza kufanya. Kwa hiyo, mumo kwa mumo ni simu na tena ni tarakilishi.
Tatizo la istilahi ya Bw Mung’ou (runulishi) ni kwamba lugha ya Kiingereza inategemea sana unominishaji kuzalisha au kupanua leksikoni yake huku lugha nyingi za Kibantu (Kiswahili kikiwemo) zikiwa ni lugha ambishibainishi (agglutinative languages).
Aidha, Kiingereza kimeegemea mno Kigiriki na Kilatini na lugha nyingine kuu ulimwenguni kupanua leksikoni yake.
Mojawapo wa sifa za istilahi nzuri kinadharia ni kwamba sharti istilahi hiyo iweze kuzashisha istilahi nyingine kwa urahisi.
Pili, Kiingereza kina mgao mpana zaidi wa maneno yanayoelezea dhana ile ile moja huku Kiswahili kikiwa na mgao finyu wa msamiati ambao huzieleza zile dhana za Kiingereza kijumla. Kwa mfano katika Kiingereza tuna dhana kama vile: mansion, castle, hut, cottage, house na kadhalika ambazo ni aina mbalimbali za nyuma.
Hata hivyo, mtu anaporejelea aina hizo za nyumba katika Kiswahili kwa neno ‘nyumba’, bado ataeleweka anachokizungumzia.
Vivyo hivyo, dhana ‘simu’/ ‘rununu’ inapotajwa, mawazo ya simu huelekezwa moja kwa moja kwenye simu jinsi tunavyoifahamu pasi na kujali iwapo ni ‘smartphone’ au aina yoyote ile ya simu.
Kwa hiyo kwa maoni yangu, ingawa juhudi za kutafuta neno la Kiswahili la ‘smartphone’ hazipaswi kupingwa, itakuwa vigumu sana kuwadara wasemaji wa Kiswahili waitumie istilahi hiyo kwa sababu hizo ambazo nimekwisha kuzitaja.
Vilevile ni muhimu kukumbuka kwamba lugha haipati hasara pale inapokuwa na leksikoni au maneno yasiyotumika. Katika makala yangu juma lijalo, nitaangazia zaidi changamoto za upanuzi wa leksikoni ya Kiswahili.
Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka.