KAULI YA MATUNDURA: Wataalamu wa Kiswahili wajadili ufaafu wa ‘runulishi’ kwa maana ya smartphone
Na BITUGI MATUNDURA
WIKI iliyopita, mwandishi na mwanahabari Geoffrey Mung’ou alizua mjadala wa kuchangamsha kuhusu upanuzi wa leksikoni ya Kiswahili kwa kuibunia lugha hii istilahi mpya.
“ Jina ‘smartphone’ lina dhana ya uwezo wa kiutendakazi sawa na tarakilishi; rununu yenyewe hutumiwa kutekelezea majukumu yote yanayotekelezwa na tarakilishi,” akasema Bw Mungou.
Aliongeza: “Ninajua kwamba yapo majina mengine yaliyobuniwa kwa maana ya ‘smartphone’ ila neno ‘rununulishi’ linaziba sawasawa pengo na mapungufu yote kuhusu tafsiri faafu ya ‘smartphone’.”
Katika makala haya, ninayahakiki maoni ya Bw Mung’ou kuwili. Kwanza, ninayatathmini kinadharia. Pili, nitayapima kwenye mizani ya kiutekelezaji. Maoni ya Bw Mung’ou yalinielekeza katika ukuzaji na upanuzi wa leksikoni ya lugha – hususan Kiswahili. Lugha huhitaji istilahi au msamiati pale inapolazimika kushughulikia mawasiliano katika nyanja maalum ambazo hapo awali ilikuwa haiushughulikii. Baadhi ya nyanja maalum ni pamoja na tiba, sheria, kilimo, fasihi, isimu , teknolojia ya habari na mawasiliano (teknohama) n.k.
Kwa hiyo, dhana ya ‘smartphone’ imejikita katika uwanja wa teknohama. Wakati mwingine, lugha huhitaji kubuniwa leksikoni inapotwikwa jukumu la mawasiliano hasa katika nchi ambazo hapo awali zilikuwa zinatumia lugha za kigeni.
Kwa bahati mbaya, lugha za madola makubwa kama vile, Kijerumani, Kiingereza, Kichina, Kijapani n.k ndizo zinatumika sana aghalabu kuelezea maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kwa hiyo, ili Kiswahili kiingie katika usemezano wa maendeleo hayo na lugha nyingine za kiulimwengu, lazima kikabiliane na matatizo ya upanuzi wa leksikoni zao.
Ikumbukwe kwamba shughuli ya kubuni istilahi ni nzito – kwa sababu kila istilahi inayobuniwa lazima iwe na mantiki ili iweze kukubalika. Shughuli hii ama inafanywa na watu binafsi, mashirika au vyombo vya habari. Nchini Kenya, baadhi ya wanaleksikolojia wapevu ambao wametoa mchango muhimu katika uwanja huu ni pamoja na Mzee Ahmad Sheikh Nabhany, Prof Rocha Mzungu Chimerah na Kyallo Wadi Wamitila.
Istilahi ‘runulishi’ kwa maana ya ‘smartphone’ Iliyopendekezwa na mwandishi Geoffrey Mung’ou iliibua mwengo wa istilahi ‘runinga’ ambayo ilibuniwa na Mzee Sheikh Ahmad Nabhany kwa maana ya ‘television’ au ‘televisheni’.
Istilahi ‘runinga’ imetokana na uhulutishaji au uunganishaji wa maneno matatu; (1) ‘rununu’ (habari/taarifa), (2) ‘yakuenga’ (kutazama) (3) ‘kwa maninga’ (kwa macho). Kwa Waswahili, neno ‘rununu’ lina maana ya habari zinazotoka mbali na mijini.
Kwa hiyo, chambacho Mzee Sheikh Nabhany, habari hizi huletwa na jinni kulingana na imani ya Waswahili. Kwa hiyo, mtaalamu huyu anadai kwamba taarifa hizo kutoka mbali ni habari (‘rununu’) za kuonwa kwa macho.
Habari za kuonwa
Kwa hiyo, Mzee Nabhany anasema kwamba ‘televisheni’ ni kifaa kinachosambaza habari za kuonwa kwa macho.
Kwa hiyo, alihulutisha maneno haya: rununu + maninga. Katika kubuni istilahi ‘runulishi’, ninafikiri kwamba Bw Mung’ou alikuwa anafuata mchakato aliouanzisha Mzee Sheikh Nabhaby.
Nadharia ya Mzee Nabhany katika kubuni istilahi mpya za Kiswahili ni kuwa, kwanza sharti umbo la kifaa au dhana inayotafutiwa au kubuniwa istilahi izingatiwe’ Pili, sharti utendakazi au uamilifu (function) wa kifaa au dhana utiliwe maanani.
Jambo la mwisho ni kuwa sharti mwanaleksikoni azingatie sauti au mlio wa kifaa cha dhana husika. Baada ya kuikagua istilahi ‘runulishi’ aliyoipendekeza Bw Mung’ou, nilihisi kwamba ingekuwa bora zaidi iwapo angeibadilisha istihahi hiyo iwe ‘rununulishi.
Sehemu ya pili ya makala haya juma lijalo itaangazia sababu za kupendelea ‘rununulishi’ badala ya ‘runulishi’.