Makala

KAULI YA MATUNDURA: Yasikitisha wanafunzi wa kisasa vyuoni kustahabu njia za mkato katika maisha

April 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BITUGI MATUNDURA

KATIKA takriban kipindi cha mwongo mmoja ambacho nimefundisha fasihi katika chuo kikuu, nimeshuhudia matatizo mengi kuhusiana na kizazi cha sasa cha wanafunzi wasiopenda kusoma.

Hali hii imedhihirika kwa jinsi wanavyojibu maswali ya fasihi kwenye mitihani. Wengi wa wanafunzi hawana mengi ya kuandika kuhusu swali wanaloulizwa – na jambo hili limekuwa likinitia wasiwasi.

Kutokana na hali hii ya kusikitisha, niliamua kufanya utafiti kubaini liliko tatizo – na labda kuibuka na suluhisho la tatizo hilo.

La sivyo, tunapoteza kizazi kizima bila ya sisi kujua. Katika kipindi hicho cha takriban miaka kumi ambacho nimefundisha chuoni, sijawahi kukumbana na mwanafunzi hata mmoja anayejibu maswali kwa kina – kiasi cha kujaza kijitabu cha majibu ambacho kina kurasa 16 pekee.

Hili ni jambo la ajabu sana kwa sababu katika enzi yetu, ninakumbuka tulikuwa tukijibu maswali kwa namna ambayo majibu yetu yalijaza vijitabu hivyo – na haka itakulazimu kupewa nyongeza ya vijitabu vingine.

Iwapo majibu tuliyotoa yalikuwa sahihi au la – ni suala la mjadala wa siku nyingine. Lakini ukweli ni kwamba tulikuwa na mengi ya kuandika kuhusiana na maswali tuliyoulizwa.

Kuwa na habari nyingi za kuandika mtu unapoulizwa swali ni ushahidi wa kutosha kwamba angalau tulisoma kwa kina kipindi hicho.

Tatizo jingine linalowakumba wanafunzi wa vyuo vikuu ni kwamba hawana umilisi wa lugha – si Kiswahili si Kiingereza.
Hali hii huwafanya washindwe kujieleza katika kujibu maswali yao ambayo mengi yao ni ya mjadala.

Aidha kizazi cha sasa kimeingiza mzaha katika kila jambo kinacholifanya.

Wengi hawaendi maktabani kusoma.

Wao hunyofoa taarifa kutoka kwenye intaneti na kuzirundika pamoja bila hata kujali iwapo taarifa hizo zinajibu swali waliloulizwa au la.

Kusoma ili kupata maarifa ni mchakato wa kimakusudi unaohusu kuketi chini, kusoma matini, kutafakari na hatimaye kuyameng’enya maarifa hayo na kuyaandika kwa njia sahili kwa kuyahusisha na tajriba na uhalisia wa maisha.

Vilevile wanafunzi wa kizazi cha sasa katika vyuo vikuu hakitilii maanani mwandiko mzuri na mpango wa kazi yao kwa namna inayoonyesha kuwa wamemakinika katika masomo yao.

Aidha wengi wao husoma kwa kubugia mambo bila kujali kuyaelewa.

Wengine hufanya ima fa ima kuendeleza udanganyifu katika mitihani. Ili kudhibiti tatizo hili, maswali yangu mengi huwa ya kiutekelezaji.

Katika enzi ya sasa ambapo taarifa na maarifa ‘yametapakaa’ kila mahali, wahadhiri katika vyuo vikuu hawana budu kulazimika kuibuka na mbinu mpya za kiubunifu za kufundisha na kuwapa mwelekeo wanafunzi kufuata mkondo na mikabala itakayowasaidia kuona muumano uliopo baina ya nadharia na uhalisia wa maisha ya kila siku.

Kukosa kuifaa jamii

Bila kufanya hivyo, tutakuwa tunatoa wanafunzi ambao hawataifaa jamii na wakati huo huo kutojifaa wao wenyewe.

Ni matarajio yangu kwamba wanafunzi wa vyuo vikuu watahimizwa kusoma kwa marefu na mapana – si tu katika maeneo yao ya masomo – bali taarifa kwenye taaluma nyingine.

Inasikitisha kwamba mwanafunzi wa fasihi ya Kiswahili kwa mfano anamaliza chuo masomo ya chuo kikuu bila kusoma hata riwaya moja ya Euphrase Kezilahabi au tamthilia yoyote ya Ebrahim Hussein na Chacha Nyaigotti Chacha.

Huu ni uzembe wa hali ya juu na wa kushangaza sana ambao haupaswi kuchangamkiwa kwa vyovyote karne hii. Katika enzi hii ambapo kila mtu anataka afe akiwa na shahada, tutakuwa na shahada za jabu mno ambazo haziakisi uwezo alio nao mtu.

[email protected]