Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Haya si maendeleo ya usasa wa Kiswahili

September 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA PROF KEN WALIBORA

Bwana mmoja aitwaye Nassoro Mwinyi niliyekutana naye Mombasa alinipa mambo mengi ya kutafakuri kuhusu taaluma za Kiswahili. Nilikuwa nimezuru eneo la Mji wa Kale kuwasabahi marafiki zangu.

Nilishangazwa na jinsi jiji la kale la Mombasa linavyobadilika kila uchao na kuwa jiji jipya. Usasa na uasilia unajongeajongea. Nahofia kwamba hatimaye utakuja kutafuta nyumba zilizosanifiwa kwa usanifu majengo ya kale isiione hata moja katika huu uitwao Mji wa Kale.

Zile chache zilizosalia zinalia machozi ya kusema niangalie nilivyotelekezwa nakaribia kufa au kuuawa. Bwana mmoja aitwaye Yahya aliniona nikipiga picha akaniuliza “Unalipiga jengo hilo picha kwa nini?”

Niliwazia mawili, ama ananitafuta ushari na kunituhumu kwa uhalifu wa aina yoyote ukiwemo ugaidi au anatania tu. Na kama ananidhania uhalifu basi mambo ndiyo hayo tena. Umati wa watu wema wa mji wa ukale upo hapa kumsaidia kwa lolote.

Hata hivyo, nilitabasamu na kutabaradi. Nikamwambia nyumba hiyo imenipendeza. Ndipo aliponijibu. “Kama imekupendeza inunue maana inauzwa na mimi ndiye mwenyewe.” Yahya alinipeleka kwake tukapanda vidato vya ghorofani na kuingia vyumba vyote na kuwapa “Asalaam Aleykum” watu wa kwake.

Yahya anasema atakayeinunua hiyo nyumba hiyo ana haki ya kujengua na kujenga nyingine ya kisasa. Akanipa nambari yake ya simu ya mkononi na kuagana kwa salama huku namwambia nikipata mnunuzi nitamwambia.

Hapa ndipo moyo wangu ulipokereketwa. Nyumba hizo zitabomelewa zote. Nyumba za kihistoria na ambazo ni urathi wa namna yake katika mwambao wa Pwani. Kile watu wanachokiongelea siku hizi ni “usasa na maendeleo,” hawataki tena kuhifadhi kumbukumbu ya jadi yao au mapisi yao.

Nilipokutana na Nassoro Mwinyi katika duka la muziki la Mzee Mbwana ndipo nilipogundua jambo jingine lililopuuzwa na watu hasa wale wajiitao wanataaluma za Kiswahili.

Kama watu wanaozitwaa nyumba za mji wa kale na kuzifyekelia mbali kwa sababu ya kuukimbilia usasa, wanataaluma wa Kiswahili wanakimbilia mambo makubwa makubwa.

Hiyo ndiyo fikra ya aliyoitoa Nassoro niliposema naye mbali na yeye na Mzee Mbwana kunifundisha mengi kuhusu historia na msamiati wa nyimbo za taarab.

Nassoro anasema wataalamu wa Kiswahili wanakimbilia mambo makubwa mazito huku wakiyapuuza mambo madogo yenye umuhimu mkubwa. Ndiyo maana utawasikia wakitumia maneno magumu kabisa, lakini hawajui kuyatumia maneno rahisi yenye umuhimu mkubwa.

Nikiwazia jinsi baadhi yetu tunavyosema “mtu amenona” badala ya “mtu amenenepa” au kondoo amenenepa” badala ya ‘kondoo amenona” au “kuna tetezi” badala ya “tetesi,” kwa maana ya uvumi. Yaani hatuna habari kwamba hapana uhusiano kati ya “utetezi” na “tetesi” na wala maneno hayo si visawe.

Baadhi ya wanunuzi nyumba katika mji wa Kale Mombasa wanafikiria usasa na maendeleo ni kubomoa nyumba za kale.

Baadhi ya wanataaluma wa Kiswahili wanafikiria kurusha makombora ya msamiati ndiyo maendeleo ya usasa wa taaluma.