KAULI YA WALIBORA: Mbona twaogopa kukiuka haki za wauaji wa lugha?
NA PROF KEN WALIBORA
HII ni enzi ya uhuru na haki. Katika enzi hii nimeona watoto wa shule za msingi wakiandamana na mabango yenye maneno yanayosema, “Haki yetu” na wakipiga mayowe sawia na maneno hayo.
Hii haki inafungamana na ung’amuzi wa uhuru wa msingi. Watu wanawania kuwa huru kwa lolote lile. Na hivi uhuru na haki haina mipaka?
Nahofia kwamba wimbi hili la uhuru ndilo linalodumaza maendeleo ya Kiswahili. Yaani watu wanadai haki yao ya kukitumia Kiswahili vibaya.
Wanadai uhuru wa kutumia Kiswahili wapendavyo, wakiandike au wakiseme kivoloya. Mtu asiseme lolote baya kuwahusu. Wao ni watu huru, watu na haki zao za kukiuka kanuni zote za lugha.
Tufani ya uhuru wa kukifisha Kiswahili imeingia kila pembe kunakozungumzwa Kiswahili. Kiswahili kinaendelea kuuawa na kimbunga hiki cha uhuru.
Kwa hiyo, si ajabu kwamba siku hizi maneno kama vile, “saa hizi” na “haki,” yanaandikwa *“saizi” na *“aki” wala hupaswi kulalamika. Ukiyaona au ukiyasikia makosa kama haya unyamaze tu, usiseme kitu. Usiseme kitu kweli? Yaani tulifikaje hapa pa kusema kuharibu lugha ya watu ni haki ya kibinadamu?
Zamani nilikuwa nafikiria kwamba kukiwepo vyombo mahsusi vya kudhibiti matumizi ya Kiswahili basi mambo yatakuwa nafuu. Nilitamani kila nchi ambayo kwayo Kiswahili ni muhimu katika mawasiliano, iwe na baraza la Kiswahili.
Matamanio yangu hayo yakiwiana na yale ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA). Nilisahau kwamba hata kabla ya KAKAMA kuundwa takriban miaka mitano iliyopita, kuna nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo tayari zilikuwa na mabaraza. Nchi hizi ni Tanganyika yanye (Baraza la Kiswahili la Taifa-BAKITA) na Zanzibar yenye (Baraza la Kiswahili la Zanzibar-BAKIZA).
Hizi kwa kweli ni nchi mbili zilizoungana na kuunda nchi moja ya Tanzania katika ndoa yenye vuta n’kuvute. Mitihani ya ndoa hii si lengo la makala haya.
Nimezitaja nchi hizi au nchi hii, kwa sababu humo mna vyombo vya dola vyenye dhamana ya kuelekeza watu namna ya kukitumia Kiswahili. Swali muhimu kwetu hapa ni: Je, vyombo hivyo vimefanikiwaje au vimefanikiwa kwa kiwango gani?
Nilitangulia kwa kusema hii ni enzi ya uhuru, enzi ya kudai haki hata zile zisizoeleweka. Sasa nasema kwamba hata katika nchi zenye vyombo mahususi vinavyohusika na lugha ya Kiswahili, bado kuna watu wengi tu wanaodai uhuru wao wa kuivuruga lugha hiyo.
Nao wanautumia uhuru wao huo kwa idili isiyosemeka. Mathalan, mnamo Jumatatu nilipotazama mahojiano kwenye runinga ya Clouds TV inayopeperusha matangazo yake kutoka Dar es Salaam, nilisikia wageni katika kipindi wakizungumza Kiswahili na kulitumia neno “serious” mara nyingi kana kwamba hilo nalo ni neno la Kiswahili. “Watanzania wanapaswa kuwa serious ili kuzuia maambukizi ya korona.”
Mbona BAKITA haijazuia unyongwaji wa Kiswahili Tanzania bara? Mbona tunaogopa kukiuka haki za wauaji wa lugha?