• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
KAULI YA WALIBORA: Namshukuru Jagina Shamte kwa sahihisho kuhusu uwanja wa michezo wa Sheikh Abeid

KAULI YA WALIBORA: Namshukuru Jagina Shamte kwa sahihisho kuhusu uwanja wa michezo wa Sheikh Abeid

Na PROF KEN WALIBORA

MANMO wiki iliyopita nilipokea mwitiko kutoka kwa wasomaji maarufu wa makala yangu katika safu ya “Kina cha Fikira.” 

Edson Wanga aliniletea arifa kupitia kwa simu yangu ya kiganjani kuhusu sahihisho la kosa langu.

Sahihisho lenyewe lilitoka mwa mshairi maarufu Abdallah Shamte ambaye alinikosoa kwa kuchanganya jina la uwanja wa michezo wa mjini Arusha.

Punde baada ya kupokea ujumbe wa Shamte kupitia kwa Wanga, Shamte mwenyewe pia aliniletea risala hiyo hiyo kama arifa.

Kimsingi Mzee Shamte alisema uwanja wa mjini Arusha unaitwa Sheikh Abeid ambaye alikuwa meya wa Dar es Salaam.

Uwanja ulioitwa kwa heshima ya rais wa kwanza wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar na makamu wa rais wa kwanza wa Tanzania, Sheikh Aman Karume, upo Zanzibar nao huitwa uwanja wa michezo wa Aman.

Nashukuru sana kwa masahihisho hayo mzee wangu Shamte na ndugu yangu Wanga kwa kuwasilisha ujumbe.

Kile kilichonishangaza katika ujumbe huo ni kwamba Mzee Shamte alitaja kwamba aliwahi kucheza mpira katika viwanja hivyo siku za ujana wake.

Waswahili husema kila mwacha sambaye huenda ali mwanamaji. Maana yake ni kwamba usimwone mtu ukamdharau kama huna habari nini alitimiza katika maisha yake zamani.

Unaweza ukamwona mtu ukampuuza au ukakosa kumwamini kwa yale anayosema alishayafanya ilhali kwa hakika katimiza mengi. Kamwe nilikuwa sijui Mzee Shamte alikuwa mchezaji wa mpira zamani.

Ni Edson Wanga ndiye aliyenipeleka kwake Mzee Shamte nilipokuwa nimezuru Mombasa, nafikiri mwaka 2014.

Alikuwa ameketi barazani, mtu mzima pale alipo, kachangamka, mbaraza na mcheshi si haba.

Ilikuwa ndio mwanzo nilimbuke kumwona mzee huyu ambaye nikisoma tungo zake tangu uraibu wa kusoma nudhuma ulipoingia nikiwa shule ya sekondari.

Nakumbuka hasa malumbano ya kishairi yaliyoshamiri kati yake na hayati Khamisi Abdallah Chombo na pia Hassan Mwalim Mbega, malumbano yaliyonogesha ulingo wa mashairi katika kurusa za gazeti la Taifa Leo.

Sasa kusikia kwamba alikuwa pia mchezaji wa soka, sijui kama mfungaji mabao, kiungo wa kati au beki, au golikipa, kwa kweli nilipata hamu ya kutaka kujua zaidi kumhusu.

Nini zaidi nisiyoyajua kumhusu jagina huyu wa ushairi? Je, ni mambo gani hatukuwahi kuyajua kuwahusu Khamisi Abdallah Chombo na Hassan Mwalim Mbega?

Nini hatuyajui kuwahusu Abdilahi Nassir, Mwinyihatibu Mohammed, Said Zakwanyi, na washairi wengineo?

Wasifu wa Haji Gora ulioandikwa na Ally Sale ni hatua muhimu katika kutuhifadhia historia ya mtunzi huyu maarufu mwenye usuli wa Zanzibar.

Labda ni muhimu kwa waandishi kama Edson Wanga kuanza kutunga mkufu wa historia ya Shamte katika Wasifu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Au Mzee Shamte mwenyewe atuandikie tawasifu yake, ili tuelewe kwa kina heri na shari alizopitia maishani.

Na vivyo hivyo, watunzi wengine watunge tawasifu au watungie wasifu ili kutajirisha tasnia ya fasihi ya Kiswahili.

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Ni muhimu kuitafitia kazi yoyote ya...

Wabunge wa Ruto Mlima Kenya wakaangwa mitandaoni

adminleo