Makala

KAULI YA WALIBORA: Tasnia ya uandishi itazidi kupiga hatua tu iwapo waandishi chipukizi na wale wabobezi wataandika sambamba, kwa sawia

March 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PROF KEN WALIBORA

Mwanafunzi aitwaye Boniface wa Shule ya Upili ya St Peter’s Mumias alinidokezea hivi karibuni kuhusu mawanio yake ya kuwa mwandishi. Si aghalabu kukutana na mwanafunzi ambaye mawanio yake si taaluma tamanifu kama uhandisi au uanasheria.

Boniface ni miongoni mwa wale wanaowania kujitosa katika ulingo wa uandishi, watuandikie vitabu tuvisome kwa lazima au kwa raha zetu. Hawa ndio William Shakespeare, Milton, Chaucer, Victor Hugo, K.W. Wamitila, Jeff Mandilla, John Habwe, na Euphrase Kezilahabi watarajiwa.

Nilikutana na Euphrase Kezilahabi kwa mara ya kwanza nilipozuru Botswana mwaka 2010 kwa kongomano la kiakademia.

Huyu ndiye mwandishi ambaye Bitugi Matundura alijasiria kusema amewapiku wote katika ulingo wa bunilizi za Kiswahili. Kaandika Rosta Mistika, Dunia Uwanja wa Fujo, Kichwani Maji, Kichomi, Kaptula la Karl Marx mbali ya hadithi ya “Mayai Waziri wa Maradhi.”

Ilikuwa fahari yangu kukutana na mkongwe huyu wa tasnia ya uandishi wa Kiswahili. Nikamuuliza alikuwa anaandika nini tukitarajie. Akaniambia kachoka, haandiki tena.

Nililikumbuka jibu lake nilipokutana na mwandishi mtarajiwa Boniface. Boniface aliniambia kwamba alitaka kuwa mwandishi maana anaona waandishi wakongwe kama vile Said A. Mohamed na mimi Ken Walibora tumekonga na karibu tufe.

Kwa hiyo, bora yeye na waandishi wengine chipukizi waanze kuandika, yaani tuwapishe wao sisi wakongwe au vikongwe. Naam, kauli ya Kezilahabi, ambaye nilivisoma vitabu vyake tangu nikiwa mwanafunzi wa shule ya sekondari, ilinijia akilini: je ina maana kuwa kuchoka na kustaafu katika kuandika bunilizi? Je, sharti tuwapishe waandishi wengine ndipo tasnia ikue?

Je, uandishi ni kama mbio za kupokezana vijiti ambapo huanzia hadi pale unapopokezwa kijiti? Au inawezekana waandishi chipukizi na wabobezi kuandika kwa sawia, kuandika sambamba, pamoja?

Huenda ikawa ni kweli baadhi ya waandishi huridhika na kuandika idadi fulani ya vitabu kisha wakaacha kabisa.

Mohammed Suleiman Mohammed aliandika Kiu, Nyota ya Rehema na Kicheko cha Ushindi akaridhika. Abdilatif Abdalla aliandika Utenzi wa Adamu na Hawaa na Sauti ya Dhiki akaridhika.

Lakini sio wote wanaoridhika na vitabu viwili vitatu au wanaosema kama Kezilahabi wamechoka hawaandiki tena.

Kuna waandishi walioandika vitabu kocho lakini ambao bado wana mawanio ya kuendelea kuandika zaidi kuchangia tasnia hii ya uandishi wa vitabu vya Kiswahili. Je, tuwashikie mtutu wa bunduki na kuwaambia kachokeni msiandike, staafuni msiandike?

Kwa waandishi kama hao kuandika ndio uhai wao, ndio pumzi ya uhai wao.

Huwezi kuwatakia kufa ili nawe uishi. Ukitaka kuishi katika ulimwengu wa uandishi lililopo ni kusema “jamani nami naja ulingoni, niachie niishi pamoja nanyi nichangie.” Kwa waandishi wa mawanio kama haya ya kuandika mpaka siku ya kufa, kuandika kwao ni kama karamu.

Usiwaambie, “acheni kula ili nami nile.’ Unajuzu kusema, “niachie nami nile pamoja nanyi.” Unapaswa kusema, “nisubiri naja” sio “ondokeni naja.” Karibu Boniface.