Makala

Kazi au Kashfa? Walioahidiwa kazi ng’ambo na serikali sasa walia kuhadaiwa

Na NYABOGA KIAGE April 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA kadhaa waliolipa maajenti wa ajira waliodaiwa kuungwa mkono na serikali ili kupata kazi nje ya nchi wamelalamikia kudhulumiwa, baada ya kusubiri kwa miezi mingi bila ajira wala kurudishiwa pesa walizolipa.

Takriban watu 48 walijitokeza kulalamika kuhusu kampuni kama Global Face Human Resources Ltd, Monisa Company Ltd na Mallow SmartHires Ltd wakisema walilipa pesa kwa matumaini ya kupata kazi nje ya nchi lakini wameachwa kwenye njiapanda.

Wengi hawajarejeshewa fedha licha ya ahadi kuwa kampuni husika zingefanya hivyo.

Wizara ya Leba pamoja na Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira (NEA) zimekuwa zikishirikiana na mashirika ya kibinafsi kuwatafutia Wakenya ajira nje ya nchi kwa malipo fulani.

Baadhi ya mashirika yaliyoshirikishwa na serikali ni pamoja na Bluewave Agency, DRA Agency, Epic Manpower, Global Face Human Resource, Iceberg Agency, Mallow Smart Hires, Monisa Agency, Shakale Agency na Workstar Agency.

Wizara ilimteua Moses Mbithi kuwa mratibu wa mashirika haya ya ajira, ingawa haijabainika wazi vigezo vilivyotumiwa kumpa jukumu hilo, ikizingatiwa kuwa si mfanyakazi wa serikali.

“Mbithi amekuwa akifanya mikutano ndani ya wizara kuhusiana na suala hili la kazi nje ya nchi,” alisema afisa wa wizara aliyeomba jina lake libanwe.

Jumapili, Aprili 6, 2025 Mbithi aliahidi kusaidia wanahabari kumpata mtu wa kujibu maswali, lakini siku ya Jumanne hakupatikana kupitia simu wala arafa.

Waziri wa Leba Dkt Alfred Mutua, alisema Jumanne kuwa waliokata tamaa ya kusafiri kuenda nje ya nchi wamekuwa wakirejeshewa pesa zao.

“Hakuna aliyedanganywa. Waliolipa na hawajasafiri lakini hawataki kusubiri, wameambiwa wachukue fedha zao,” alisema.

Aidha, alisema yeyote anayehisi kudhulumiwa anafaa kupiga ripoti kwa polisi na atahakikisha haki inatendeka.

Hata hivyo, alionya kuwa wale watakaotoa madai ya uongo pia watachukuliwa hatua za kisheria.

Dennis Moberu, mwenye umri wa miaka 30, alilipa Sh15, 000 kwa Global Face Human Resources Ltd mwaka jana kwa matumaini ya kupata kazi ya ujenzi Milki ya Ufalme wa Kiarabu (UAE).

Pamoja na wengine 40, walifanyiwa vipimo vya afya lakini miezi sita baadaye, hakuna kazi wala pesa zilizorudishwa.

“Tuliambiwa tutasafiri baada ya wiki mbili, lakini hadi sasa mawasiliano yamesitishwa,” alisema Moberu, ambaye ni yatima anayesaidia ndugu zake.

Taarifa za polisi zinaonyesha kuwa Festus Omwamba, mwakilishi wa kampuni hiyo, alikamatwa Machi 27 baada ya malalamishi kuwasilishwa, lakini aliachiliwa kwa dhamana ya Sh200, 000.

Hata hivyo, Omwamba amekana madai hayo akisema kucheleweshwa kwa visa ndicho kinachowazuia waliosajiliwa kusafiri.

Wengine sita waliolipa Monisa Company Ltd wanasema bado hawajasafiri kuwahi kazi walizoahidiwa.

Kati yao ni Severin Osoro, Joshua Choti, Cliff Nyakundi, Vincent Moroga, Enock Sambura, Kevin Kingi na Alex Kondo.

Wanasema mwakilishi wa kampuni hiyo, Titus Kaloki, alidai Sh150, 000 zaidi katikati ya Novemba.

“Simu yake huwa haipatikani. Tunataka Wizara ya Leba iingilie kati,” alisema Osoro.

Dkt Kaloki hakujibu simu wala ujumbe wa wanahabari kuhusu malalamishi hayo.Kwa upande mwingine, baadhi ya waombaji kazi waliolipa Mallow SmartHires walirejeshewa sehemu ya pesa zao, huku wengi wakilalamika kwamba hawajafidiwa kikamilifu.

“Mimi nililipa Sh55,000, lakini nilirudishiwa Sh37,000 tu baada ya kulalamika,” alisema mwombaji mmoja ambaye alisema anaogopa kusutwa na jamaa waliomuonya mapema.

Seneta mteule Gloria Orwoba, Machi 26, alitoa wito kwa Seneti kuchunguza mashirika haya ya uajiri yanayodaiwa kuungwa mkono na wizara, na kubaini iwapo baadhi yanamilikiwa na watu wenye uhusiano wa karibu na maafisa wa serikali.