KIJIWENI: Mwanamume kamili
Na DKT CHARLES OBENE
IJE mvua lije jua, kamwe sitathubutu kudunisha juhudi za mamangu mzazi!
Daima nitajizatiti na kujikaza kisabuni kutimiza malengo aliyokusudia mamangu kunikopoa mimi mwana asiye usuli.
Lau kwa uvumilivu na ucha Mungu wake, labda ningalitemwa kama mate ya asubuhi ama ningalibururwa na majibwa kutoka majaa ya taka au ningalimenywa vijipande kutoka kizazi chake na kutupwa pipani.
Hakufanya hivyo mama!
Vimwana wangapi kati ya wazembe wa leo wanaoweza kukaidi shinikizo za jamii wakabeba himila na mwishowe kujifungua mwana?
Afadhali hata nzi ana ujasiri na akili razini.
Hakuna cha thamani kinachoweza kulipa ujasiri wa mamangu ila kumtendea wema na mema.
Alikuwa na uwezo kufanya yote wanayofanya vimwana wa leo.
Angalitaka angaliavya katika zahanati yoyote ile!
Angalikunywa sumu na vidonge vya kuzima taa ya maisha na mwanga wa roho yangu. Angalikoroga majani na mitishamba. Angalikwenda kwa wakunga kutaka msaada ili kuondoa kero ya mimba.
Angalizaa na kuniacha ufuoni mwa mto. Angalilipwa vichele vya pesa ili kunitupa chakani!
Mwanamke mwema anajua mwisho wa mzaha.
Hivyo ndivyo alivyofanya mama.
Alihakikisha kwamba mzaha upo mfundani. Alisimama kidete akahimili vishawishi vya marafiki waliomshinikiza kutungua kitu kilichotungwa ndani yake.
Alikaidi vitisho na ahadi zote zilizonuia kumshikisha damu ya mauti.
Huo ndio ujasiri wa mwanamke mwema.
Huo ndio moyo wa mwanamke kamili.
Haja gani kuhimilika katika raha na mwishowe kufa mfano wa nzi?
Mimi ni mtu mzima tena mwenye akili timamu.
Licha ya utu uzima huu, bado nazongwa akili tena kwa ghadhabu mno kwa sababu ya tabia za wanawake kwa wanaume wa leo kula raha na mwishowe kuafikiana, kushirikiana na kufurahia kutekeleza uavyaji.
Damu ya nani isiyoganda kwa ukatili unaotekelezwa kisiri katika miji na vijiji vyetu?
Vilikosa nini vijusi hivi vinavyokatwa vipande vingali kizazini? Yaani pesa zina thamani kuliko roho? Visa vya wanawake kuavya na kutupa vijusi vimekuwepo tangu jadi.
Wengi walioavya walifanya hivyo kisiri ili kuzuia fadhaa na kukwepa hadaa za gumegume waliopachika mimba hizo kabla ya kukwepa mlio wa ngoma.
Mwanamume wa leo
Kweli, ndio kwanza dunia inatambua mwanamume wa leo. Haja yake kula vya kuliwa. Hana haja kusubiri mabuyu kudondoka mbuyuni!
Ole nyinyi vichuna na vimwana wa leo mnaofukuzana na magumegume katika baa, vilabu, vijia vya kiza, mabweni ya vyuo na nyanja za mahaba hadaa!
Mwasubiri kimbunga gani kuwajuza dunia wakati wenzenu wanafia zahanatini kwa amri na ufadhili wa mwanamume wa leo?
Sikitiko langu ni kwamba wanaume wa kisasa hawana haya wala soni kutoa amri ama kufadhili uavyaji wa mimba – hasa hizi mimba za wanaharamu.
Mwanamke wa kale sawa na mwanamke wa leo. Wote wangali ndani mwa vitanga vya desturi kandamizi na mila potovu.
Isitoshe, jamii inavulia kofia wanaume wanaofadhili ukatili dhidi ya vijusi.
Mbona hatuna huruma kwa masikini wanawake wa leo? Jamani wanaume wa leo mbona mkawa sikio la kufa lisilosikia dawa?
Linalochukiza zaidi ni kwamba walioathirika mno na visa vya uavyaji ni wanawake waliosoma wakahitimu katika taaluma tofauti.
Yaani wasomi wangali ndani mwa kiza cha maisha. Watoto wa maskini wako mumo humo wakifuata pesa za matajiri ambao mwishowe huwakwepa kana kwamba wanaugua ukoma.
Kama maisha mema ni mume hamna budi kuthathmini kwa kina tabia za gumegume wa leo. Tahadharini msijeavya mkawa mzigo ndani ya mapande ya mbao!
Ndio kwanza dunia inatambua mwanamume wa leo! Hana haja kusubiri mabuyu kudondoka mbuyuni!