Makala

KIKOLEZO: Ageuka lulu majuu

March 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na THOMAS MATIKO

NYOTA mwigizaji wa hapa nyumbani Lupita Nyong’o anazidi kuchachisha kule majuu Hollywood kwa mambo makubwa anayoendelea kufanya katika tasnia ya filamu.

Tangu alipopata umaarufu mwaka 2012 kwa kushinda tuzo ya hadhi ya Oscars baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye filamu yake ya kwanza katika levo ya kimataifa 12 Years A Slave, mtoto wa mama amegeuka kuwa lulu.

Kila kukicha anaitiwa kazi kubwa kubwa ambazo kando na kumzidishia umaarufu, zimeweza pia kuanza kumtengenezea kipato, tena kizuri.

Kwa sasa Lupita anapiga noti ya maana bila kubahatisha.

Mwigizaji Lupita Nyong’o. Picha/ Maktaba

Kila anachokigusa kinabadilika na kuwa lulu kama sio dhahabu.

Na kasi hii ndio kama vile haipungui huku tayari kukiwa na ripoti kuwa, kalipwa mamilioni ya pesa kuigiza kwenye filamu yake mpya kabisa Us ambayo ni ya kuogofya na ambayo yaingia sokoni rasmi leo.

Je, kipochi cha Lupita kwa sasa kimekaa vipi?

Thamani yake noma

Wanasema mambo mazuri hayahitaji pupa. Lupita alipotokea kwenye 12 Years A Slave, muda mfupi tu baada ya kufuzu kutoka Chuo cha Uigizaji cha Yale kule Marekani, pengine hakudhania angeishia kuwa bonge la staa jinsi ilivyo kwa sasa.

Filamu hiyo haikumlipa vizuri ila ilimtengenezea mazingira mazuri ya kuweza kuanza kuvutia dili nzito nzito.

Thamani kamili ya Lupita haijulikani ila ndani ya miaka mitano hiyo toka ageuke kuwa staa, imekadiriwa kuwa dola 8 milioni (Sh800 milioni) kwa mujibu wa Celebrity Worth.

Nalo Jarida la kimataifa la Insider limekadiria ukwasi wake kuwa unafikia dola 5 milioni (Sh500 milioni).

Chanzo kikubwa cha hesabu hizi ni malipo mazuri ambayo ameendelea kupata kadri anavyozidi kutokea kwenye filamu tofauti na zikaishia kufanya vyema sokoni.

Lakini pia amekuwa akipata dili kibao za kimatangazo kutoka kwa kampuni tofauti. Hizi hapa badhi ya filamu zilizomvutia mkwanja mnene na dili kali za kibiashara alizopiga.

Black Panther (2018)

Malipo: Dola dola 1 Milioni (Sh100 milioni)

Kwenye filamu hii ya Black Panther iliyotengeneza faida kubwa baada ya kupiga zaidi ya dola bilioni sokoni, Lupita alilipwa dola milioni moja kwa uhusika wake kama Nakia kwa mujibu wa tovuti ya Universal na All Hiphop.

Star Wars: The Force Awakens (2015)
Malipo: Dola 300,000 (Sh30 milioni)

Filamu hii ilitengeneza dola 2.7 bilioni sokoni. Lupita aliyeigiza kama Maz Kanata alikuwa miongoni mwa waigizaji waliolipwa mshahara mdogo akipata Sh30 milioni huku waigizaji wakuu wakipokea kati ya dola 2 milioni hadi dola 10 milioni.

Star Wars: The Last Jedi (2017)

Malipo: Dola 300,000 (Sh 30 milioni)

Malipo yake yalisalia kama yale ya The Force Awakens kwenye mwendelezo huo wa Star Wars.

Us 2019

Malipo: Bado siri kubwa

Licha ya kuwa bado haijulikani kiasi cha pesa alizolipwa kwenye filamu hii ilinayoingia sokoni leo, inaaminika Lupita alilambishwa mamilioni ya dola hasa ukizingatia kwamba ni mmoja wa wahusika wakuu. Filamu hii ilitengenezwa kwa bajeti ya dola 20 milioni na kulingana na wachanganuzi, inatarajiwa kuingiza dola 35 milioni wikendi hii na ikizidisha kasi hiyo, huenda ikamshindia tuzo ya Oscar ya mwigizaji bora mwaka ujao.

Dili za kimatangazo

Ukiweka mbali mkwanja kutokana na filamu, Lupita pia ameweza kupiga hela ndefu kupitia mikataba kibao ya matangazo ya kibiashara hasa kutoka kwenye kampuni za fasheni.
Kampuni ya vipodozi na marashi ya kule Ufaransa, Lancome iliripotiwa kumlipa zaidi ya dola 1 milioni kuwa balozi wake.
Mwaka 2018 alisaini mkataba na kampuni ya Calvin Klein kuwa balozi wa marashi yake mapya ‘Woman’. Dili hiyo vile vile iliripotiwa kuwa ya kiasi kisichopungua dola milioni.

Mwigizaji Lupita Nyong’o. Picha/ Maktaba