KIKOLEZO: Rihanna hatari faya!
Na THOMAS MATIKO
UTAKUWA tayari unazo taarifa kuwa staa wa RnB Robyn Rihanna Fenty yupo kwenye ligi tofauti kabisa.
Anaishi maisha yasiyo ya kawaida. Usafiri wake wa angani ni wa ndege za kibinafsi. Akiwa majini, anatumia yoti za kukodisha yeye na wapambe wake.
Juzi karipotiwa kukodisha kisiwa kizima kule Uingereza kwa ajili ya kurekodi albamu yake.
Kisiwa hicho ni cha ukubwa wa ekari 380 anakoishi kwa sasa na familia yake tu, wengine hamruhusiwi hata kama mna uwezo huo.
Rihana haogopi kutumia pesa; anajua kuonyesha ujeuri wa noti. Mavazi yake ndio usiseme. Unaambiwa kila aendako huongozana na msusi wake kibinafsi pamoja na mrembaji anaowalipa hadi kufikia Sh20 milioni kwa mwezi. Na haiishi hapo tu, hata mpenzi wake sio mtu wa kubabaisha. Ni bilionea Hassan Jamal.
Kama akiamua leo, Rihanna anaweza kuchemsha ‘githeri’ kikatokota na kuiva kwa noti alizonazo na bado zibaki kibao.
Ndiye mwanaburudani wa kike anayeongoza kwa utajiri duniani kwa sasa.
Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya jarida la Forbes iliyotolewa wiki iliyopita.
Akiwa na umri wa miaka 31 tu, kisura hiyo kafanikiwa kujitengenezea himaya kubwa ya utajiri unaokadiriwa kufikia dola 600 milioni.
Kipato hiki kimemfanya kuwafunika manguli wengine wa kike aliowakuta tayari wakiwa wapo kwenye gemu.
Tunawazungumzia kina Madonna aliyeanza muziki hata kabla Rihanna hajazaliwa. Bibi huyo mwenye umri wa miaka 60, ndiye anayemfuata kwa kuwa na kipato cha dola 570 milioni.
Kisha mkongwe mwingine aliyepata umaarufu mkubwa miaka ya tisini Celine Dion, 51, akiwa na ukwasi unaofikia dola 450 milioni huku mke wa mtumbuizaji tajiri zaidi duniani Jay Z, Beyonce 38, akihitimisha nne bora na kipato cha dola 400 milioni.
Kuwafunika wakali hawa licha naye kuwa mkali utakubaliana nami haikuwa kitu rahisi. Na hata zaidi ukizingatia kuwa wakati Riri anaanza muziki akiwa hafahamiki, hawa tayari walikuwa ni watu maarufu.
Hii ina maana kuwa, ili kufikia upeo huu, alihitaji kucheza na hesabu zake vizuri. Lakini kivipi?
Mauzo ya muziki
Kulingana na lebo ya Roc Nation inayomilikiwa na Jay Z, Riri kauza zaidi ya nakala 60 milioni za albamu zake kote duniani.
Na kwenye mitandao ya kupakia muziki, nyimbo zake zimepakuliwa zaidi ya mara 215 milioni. Anakuwa msanii wa pili katika historia ya burudani kufikia levo hizi.
Imekuwa kawaida kwake kupiga pesa za maana kupitia mauzo ya muziki na shoo zake. Kwa mfano 2016, alitengeneza dola 22.3 milioni kupitia muziki pekee. Kisha baadaye alipofanya ziara yake ya ‘Diamond’, ilitengeneza kipato cha zaidi ya dola 137 milioni kabla ya makato ya kodi.
Mkwanja wa vipodozi
Pamoja na kuwa anavuta hela za maana kupitia muziki, ripoti ya Forbes imebaini kuwa sehemu kubwa ya utajiri wake umetokana na biashara anazojihusisha nazo.
2017, aliungana na kampuni ya vipodozi ya Ufaransa LVMH inayomilikiwa na bilionea Bernard Arnault. Kwa ushirikiano na bilionea huyo, Riri alianzisha kampuni yake ya vipodozi Fenty Beauty Septemba mwaka huo.
Takwimu zinaarifu kuwa Fenty Beauty ilitengeneza zaidi ya dola 100 milioni kimauzo kwenye wiki kadhaa za kwanza. Riri alichangia pakubwa mauzo hayo kwa kutumia nguvu zake za Instagramu aliko na zaidi ya wafuasi 71 milioni, kutangaza bidhaa hizo.
Kikubwa zaidi kilichomwezesha kuvutia wateja wengi ni uwezo wa Fenty Beauty kutengeneza aina 40 tofauti ya vipodozi ikilinganishwa na 10 au 12 za kampuni zingine.
Mwaka jana, kipato cha Fenty Beauty kilizidi zaidi ya mara tano ya kile cha mwaka wa kwanza kwa kuingiza dola 570 milioni.
Noti za fasheni
Baada ya vipodozi, Riri alizamia fasheni na kufungua kampuni nyingine ya Fenty kwa ushirikiano bado na LVMH.
Fenty hii inahusika na masuala ya uuzaji wa kivazi cha ndani cha wanawake ‘Lingerie’, na manukato.
Nayo pia iliingia sokoni na ni mojawapo ya mitindo inayokimbiliwa na kina dada. Hili limetia homa lebo zingine Dior, Louis Vuitton, Gucci kati ya zinginezo.
Kushindana nao, Fenty imehakikisha bidhaa zake zinakuwa za nafuu kidogo ikilinganishwa na lebo hizo.
Rihanna aliwekeza dola 34 milioni kuanzisha lebo ya Fenty kwa ushirikiano na LVMH na sasa thamani ya kampuni hiyo ni zaidi ya dola 100 milioni.
Noti za mjengo
Miaka michache iliyopita, alinunua mjengo kule Los Angeles kwa dola 6.8 milioni na baada ya kuufanyia ukarabati mdogo akauingiza sokoni tena na kuuza kwa dola 7.4 milioni.
Anamiliki majumba kadhaa Marekani ambayo kayakodisha.