KIKOLEZO: Secular ila wanafanya Gospel fire!
Na THOMAS MATIKO
NIMEWAHOJI wasanii wengi wa hapa nchini na kila mara mimi hupata nikiwauliza swali moja; “Ni kwa nini wanamuziki wengi wa injili wa Kenya hawaonyeshi kuzingatia maadili na desturi stahili za muziki wa injili”?
Swali langu limetokana na kuona jinsi tasnia ya muziki wa injili ilivyobadilika baada ya kuja kwa wasanii kizazi kipya hichi cha kina Willy Paul.
Toka madogo hawa waibuke, ule mtindo wa kina Gloria Muliro, Eunice Njeri, Janet Otieno, Reuben Kigame, Esther Wahome, The Kasanga’s, marehemu Peter Kaberere miongoni mwa wengine, umepotea. Siku hizi nyimbo za injili hazina hoja wala vina vya kina. Ni mistari ya kawaida sana, wanalofanya wasanii hawa ni kumtaja Mungu tu kwenye mishororo michache. Nyimbo zenyewe zinatokana na midundo ya densi. Hawaeleweki!
Kinachoniumiza kichwa sasa ni pale ninapowaona wasanii wa muziki wa densi, wakiachia ngoma za injili zilizojifuma kwenye misingi ya kidini bila kukufuru. Zina hoja na mada toshelezi. Hawa ni baadhi ya walionijia kichwani. Kama leo wakiamua kugeukia injili, watatisha.
NYASHINSKI (Mungu Pekee)
Mara tu baada ya kurejea nchini kutoka Marekani alikokuwa ameishi kwa miaka 10, Nyash alijitambulisha kwa ngoma tatu, Letigo, Now You Know na Mungu Pekee.
Alipoachia Mungu Pekee, wengi walianza kuhoji ikiwa kaka kaokoka. Ni wimbo ulioibua hisia nzito na kuzua mjadala kuhusu ujumbe wake na namna alivyoimba kwa hisia na kumtukuza Mungu. Na japo hakutoa video, kufikia leo una ‘views’ zaidi ya milioni 7.5 pale YouTube.
Hii inakuonyesha kuwa kama leo Nyash akigeukia injili, basi anaweza kuchangia kurejesha heshima ya tasnia hiyo iliyopotea.
SAUTI SOL (Kuliko Jana)
Miaka minne iliyopita bendi ya Sauti Sol waliamua kukaa kwenye biti moja na bendi ya RedFourth Chorus na kazi waliyoishia kuipika ikawa ni ‘hit’ kubwa ya injili, Kuliko Jana.
Wimbo huu ni wa kumsifu Mungu na kumtukuza mwanzo mwisho. Mashairi yana ujumbe na hoja. Video ina maadili yake, haina mbwembwe na wasanii wametulia. Haina picha chafu wala matukio ya kukuacha na maswali. Kazi hiyo ni moja ya nyimbo zipatikanazo kwenye albamu yao ya Live & Die in Afrika. Video hiyo ina zaidi ya ‘views’ 9.9 milioni. Leo Sauti Sol wakiamua kuwa wasanii wa injili, ni dhahiri watatisha kuliko hao kina Pozee.
NADIA MUKAMI (Maombi)
Mwaka jana kuelekea ukingoni, msanii wa densi Nadia aliingia studio kama kawaida na kuachia wimbo Maombi.
Kazi hiyo ilipotoka, wengi wakauliza kama naye kavuka hadi ng’ambo ya pili. Lakini kwenye majibu yake, Nadia alisema ulikuwa ni wimbo wa kumshukuru Mungu baada ya kumwonekania sana mwaka huo.
Ngoma ni safi, hakika ina meseji ya shukrani na yenye unyenyekevu. Video nayo haina mbwembwe zisizostahili na hata kwa upande wa mavazi, Nadia anaonyesha kujisitiri vyema. Sio ajabu mpaka sasa ina zaidi ya ‘views’ 740,000.
JULIANI (Pages Za Bible & My Call)
Rapa Juliani alipokuwa akianza sanaa yake yapata miaka 10 iliyopita, wengi walimchukulia kuwa rapa wa injili kutokana na kazi alizoanza nazo.
My Call aliyoshirikishwa na kundi la injili lililosambaratika la MOG, Juliani anachana mishororo mizito ya kumsifu Mungu. Kwenye Pages Za Bible aliyoitoa kipindi akiwa anaanza shughuli, ikawa ni vile vile. Juliani anamsifu Mungu kwa fujo. Hii ni moja kati ya kazi zilizomfanya kuwa maarufu. Leo akiamua kuachana na nyimbo za kizalendo na akarudi huko, mbona bado atatisha tu.
DOGO RICHIE (Maombi)
Baada ya miaka 10 kwenye gemu, miezi michache iliyopita Dogo Richie msanii kutoka Mombasani alizua gumzo baada yake kuachia ngoma mbili za injili kwa kufululiza.
Moja kati ya kazi hizo ni Maombi alichoshirikishwa na msanii chipukizi wa injili Chrisleno. Hapa Dogo anabadilika kabisa na kama ni mara yako ya kwanza kumsikia, basi utasadiki kuwa ni msanii wa injili wa siku nyingi. Anaimba kwa hisia, anazingatia maandiko kwa kina na mashairi yanaridhia. Video vile vile nayo haina vishasha.