KIKOLEZO: Vijiskendo kawapa jukwaa kuu showbiz
Na THOMAS MATIKO
KATIKA tasnia ya Showbiz wadau wengi ambao huchachisha ni wanamuziki, waigizaji na masoshiolaiti.
Kunapokosekana skendo, Showbiz hukwama kwa kukosa ladha. Ndio sababu skendo ya Jalang’o ilitrendi kwa zaidi ya siku tatu. Lakini pia kuna tabaka la watu ambalo halifai kabisa kuwa kwenye Showbiz lakini kutokana na vijiskendo vyao, limejikuta likiongezwa miongoni mwa wadau wa tasnia hii.
Tabaka hilo ni la wasomaji habari runingani. Japo wengi hujitahidi kuepuka vijiskendo, wapo wenzao waliochoma picha kabisa. Listi hii imewabeba baadhi yao.
BETTY KYALLO (K24)
Toka alipotalikiana na aliyekuwa mume wake Dennis Okari 2015 baada ya miezi sita pekee kwenye ndoa, amekuwa na vijiskendo vya kutosha. Talaka yenyewe hiyo ilizua gumzo kweli kweli. Mpaka leo Betty na Okari hawana uhusiano mzuri na mara kwa mara msupa huyo kadai kuwa anamlea mtoto wake solo. Hata hivyo Okari amekuwa akipinga kwa kusema Betty humwekea vikwazo kwenye suala la malezi.
Mwaka juzi alitibuana na mshikaji wake, Susan Keitany, kisa mwanamume.
Betty kutrendi kwa utata imekuwa kitu cha kawaida.
Aidha anapenda kutoa kauli tatanishi ambazo huwaacha wengi wakishindwa kumwelewa. Wengine huzichukulia kama kiki. Kwa sasa kuna tetesi kuwa kaishtaki kampuni anayoifanyia kazi baada ya kushurutishwa kuchukua punguzo la mshahara wake lakini kagoma.
Kwenye mapenzi, anasema anawinda jamaa aliyetaliki ili amzalishe mtoto wa pili. Kasheshe zake kama vile hazina mwisho.
ESTHER ARUNGA (KTN)
Miaka kumi iliyopita Arunga alifanikiwa kuziteka nafsi nyingi nchini kupitia usomaji wake wa habari katika runinga ya KTN.
Hakuwa msichana mrembo tu, ubongo pia ulijaa kisomo cha maana. Alikuwa na shahada ya sheria na utangazaji. Shughuli zake za kuwa mwanahabari alianzia kwenye redio ya Capital FM kabla ya kuhamia runingani KTN akiwa bado mchanga sana. 2008 alishinda tuzo za CHAT Award, kitengo cha mtangazaji bora chipukizi.
Miaka iliyofuata, taaluma yake ilikuwa ya kufana sana. Ghafla mapenzi yakaanza kumvuruga. Alifanikiwa kumpata mchumba promota wa tamasha Wilson Malaba na hata wakapanga ndoa. Lakini miezi miwili kabla ya harusi yao iliyokuwa imeratibiwa mwezi Aprili 2010, wakatemana. Malaba alimlaumu Quincy Timberlake, mumewe wa sasa kwa kuvuruga penzi lao kutokana na kuishi kumfuatilia akimtongoza.
Mwishowe waliachana na akaanza kutoka na Quincy aliyekuwa mume wa mtu wakati huo. Kilichofuatia ni yeye kuacha kazi na kutangaza kujitosa kwenye siasa, ndoto ambayo haikuwahi timia. Aliwahi pia kuwashtaki wazazi wake na kudai fidia ya Sh300 milioni akiwashtumu kwa kumnyima haki ya uhuru wake alipotangaza anamwoa Quincy ambaye wakati huo alikuwa katupwa seli kwa tuhuma za utapeli.
Baadaye walihamia Australia na kujaliwa kupata watoto lakini mwanao wa kwanza aliuawa na mumewe na Arunga akajaribu kumkingia. Alipogundua anaweza kutupwa jela kwa miaka 25, alimruka na kukiri ndiye muuaji. Maisha ya Arunga kwa sasa hakuna anayeyafahamu.
JACQUE MARIBE (Citizen TV)
Skendo zake za mapenzi ziliishia kumpotezea kazi katika runinga ya Citizen ambapo alikuwa kafanikiwa kupanda ngazi kutoka ripota wa nyanjani hadi msomaji habari.
Sakata yake ya kwanza iliyozua utata ni picha zilipoibuka akiwa anapigana denda na Erick Omondi. Wawili hao waliishia kukana kuwa kwenye mahusiano. Baadaye alipata ujauzito na kujifungua mtoto wa kiume. Mwaka 2019 Maribe na Erick wakajitokeza hadharani kuthibitisha kwamba waliwahi kuwa wapenzi na kujaliwa yule mtoto.
Baadaye alianza kutoka kimapenzi na Jowie Irungu aliyemwingiza kwenye sakata ya mauaji ya mfanyibiashara Monica Kimani. Jowie alitajwa kuwa mshukiwa mkuu huku gari la Maribe likichukuliwa na wapelelezi kusaka ushahidi. Naye alilala jela kwa siku kadhaa uchunguzi ulipokuwa ukiendelea. Alipofanikiwa kutoka jela, akatangaza kuondoka Citizen TV na pia kutemana na Jowie. Kumekuwepo na tetesi kuwa karejesha penzi lake kwa Erick.
WILLIS RABURU (Citizen TV)
Vimbwanga vya mtangazaji huyu kibonge vyote vimekuwa ni vya mapenzi. Raburu na ripota wa zamani wa Citizen TV Sally Mbilu, walikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa kipindi kirefu sana. Mwishowe Raburu aliishia kumchumbia na pete yenye thamani ya Sh100,000.
Januari 2016, Raburu alimtema Sally na mwaka mmoja baadaye akamwoa kichuna Mary Ngami baada ya miezi mitatu tu ya uchumba. Mwaka huu 2020 ndoa yao iliripotiwa kuvunjika tetesi zikidai kuwa Raburu alikuwa akimchepukia mkewe.
LOUIS OTIENO (KTN)
Enzi zake Louis alikuwa miongoni mwa wanahabari waliokuwa wakilipwa mshahara mkubwa zaidi nchini. Hata hivyo taaluma yake ya kufana ya utangazaji ilipiga breki jina lake lilipotajwa kwenye upelelezi wa kifo cha mwanafunzi wa chuo kikuu, Careen Kipchumba.
Kilichofuatia ni kazi yake kukatishwa na hapo akaachwa kusaka riziki kwingine. Kisha akapatwa na ugonjwa uliompooza. Uwezo wake wa kusikia ukapotea na hata kushindwa kutembea. Maisha anayoishi yamekuwa magumu. Miaka miwili iliyopita, aliitisha michango ya kumwezesha kupata Sh4 milioni kwa ajili ya kufanyiwa matibabu ili aweze kurudi sawa.