KIKOLEZO: Walivyoacha mashabiki hoi
Na THOMAS MATIKO
YAPATA wiki mbili zilizopita, mwanamuziki wa kike Ivlyn Mutua aliitikisa tasnia ya injili kwa kuchukua hatua isiyo ya kawaida.
Ivlyn aliwaacha wengi hoi alipotangaza kwamba alikuwa ameamua kuhamia ng’ambo ile ya pili.
Wengi walishindwa kumwelewa.
Wengine walimchamba kwa kumwambia kapagawa. Babake mzazi mwenye imani ya Kikristo alimuonya kwamba isitokee akasikia kwamba kaishia kuwa Illuminati.
Kwa walioshindwa kuelewa uamuzi wake anaosema ulimchukua miaka miwili, kichuna huyo alisema wakati alipokuwa akifanya muziki wa injili, hakujihisi akiwa huru.
Alisema alihisi ubunifu wake kama msanii ulikuwa ukibanwa kutokana na kuzingatia sana misingi ya kidini na ili kuwa huru, hakuwa na jingine ila kuikacha injili na kujitosa kwenye muziki wa kidunia.
Wakati Ivlyn akitoa sababu zake za hatua hiyo, pia tumeshuhudia wasanii wengine (hasa wa kike) waliotesa sana kwenye muziki wa densi, walioamua kuokoka kila mtu akitoa sababu zake. Kwa nini hawa waliamua kuokoka?
Wahu
Mwaka juzi, mwanamuziki Wahu ambaye ni mkewe Nameless, naye aliamua kuutosa muziki wa densi na kuokoka. Mume wake wa zaidi ya miaka 15 bado kagandia ‘Misri’.
Wahu ambaye amekuwa bize akiachia muziki wa injili japo haujaonekana kuwa na mashiko ikilinganishwa na ule wa densi aliofanya awali, naye alikuwa na sababu zake za kufuata nyayo za wenzake.
Kulingana naye, alikuwa amepitia kipindi kigumu sana katika maisha yake na kufikia hatua hakuwa na amani kabisa. Muziki wa densi ukamshinda na ndio sababu akaamua kusaka pa kuituliza nafsi yake na ndivyo alivyoishia kuokoka.
Japo hakufafanua magumu hayo, wapo wale waliojijazia kwamba pengine ilitokana na presha kubwa ya ile skendo aliyodaiwa kumchepukia Nameless na kuzaa mtoto wao wa pili na mchepuko huyo.
Ilikuwa skendo nzito ambayo ilidai kuwa Nameless aliishia kuitisha vipimo vya DNA kuthibitisha hilo.
Size 8 Reborn
Ilitokea 2013 kipindi ambacho mashabiki wake wengi hawakutarajia tangazo lake. Size 8 alikuwa amevuruga chati sana na muziki wa kisasa tangazo lake la kuokoka lilipotoka. Hiki ni kipindi ambacho alikuwa na ‘hits’ kama ‘Vidonge‘, ‘Silali‘, ‘Shamba boy‘, ‘Fire‘ kati ya nyinginezo.
Size 8 alipotangaza kuokoka wengi walishindwa kama ataweza kuendelea kuachia muziki mnene. Ila hakika alijitahidi na kuachia kete kama Moto na Mateke.
Lakini pia wengi walishindwa kuelewa ni kwa nini alichukua uamuzi ule. Ila katika maelezo yake, Size 8 alisema uamuzi wake ulitokana na sababu kwamba ilifikia hatua hakuwa na amani kabisa. Licha ya kwamba alikuwa akitengeneza pesa kwenye muziki wa densi, hakuwa akiyafurahia yale maisha aliyokuwa akiishi kipindi hicho.
Lakini pia ilikuwa ni aweze kutimiza ndoto ya marehemu mamake aliyetamani sana kumwona mtoto wake akiokoka na kuacha kunengua mauno.
Hata hivyo kilichofuatia baada yake kuokoka ni kufanyika ndoa ya kisiri kati yake na DJ Mo ambaye walikuwa wameonyesha ukaribu sana kama marafiki tu na hakuna aliyetegemea wangeishia kuwa kitu kimoja.
Wapo wanaoamini kuwa sababu hasa ya Size 8 kuokoka ilikuwa ni kwa ajili ya kuweza kuingia kwenye ndoa na Mo ambaye ni DJ wa injili. Lakini pia zipo tetesi kwamba Size 8 alikuwa tayari ameshanasa ujauzito na ili kuepuka dhihaka na skendo, wakaamua kuoana.
Amani
Kwa zaidi ya mwongo, Amani alivuruga chati sana za muziki wa densi.
Kwenye mahojiano yangu naye nyuma kidogo, Amani alisema hakuwahi kukosa shoo kutokana na kuwa wasanii wa kike walikuwa wachache sana na akawa mmoja wa wale waliokuwa wakifanya muziki mzuri.
Hata hivyo baada ya zaidi ya miaka 10 akifanya muziki wa densi, alianza kufifia na kupotea. Akapunguza kasi ya kufanya muziki wake akawa anaachia kwa kusitasita.
Mei 2018 kwenye mahojiano na Daily Nation, Amani alifungukia sababu zake za kuukacha muziki wa densi na kuingia kwenye injili.
“Nilichoka tu na maisha yale. Kila mara nipo safarini kupiga shoo, narudi nyumbani kuchelewa. Sikuwa napata muda wangu binafsi au hata wa kutangamana na familia yangu sababu safari hizi hazikuwa zinaisha,” akasema.
Aliamua kuokoka 2015 kipindi ambacho pia alikuwa tayari ameshaanzisha uhusiano wa kimapenzi na mpenzi wake Mnigeria ambaye kwa sasa ni mume wake. Wapo wanaoamini kuwa hatua yake kuokoka haikuwa kuchoshwa na shoo sababu kama msanii wa injili, kusafiri kwa ajili ya kupiga shoo ni kitu ambacho kipo. Wanasisitiza alichukua uamuzi huo ili aweze kutulia na kujitengenezea maisha ya ndoa.
Cece Sagini
Cece alitangaza kuokoka Oktoba 2017.
Kulingana naye sababu kuu ilichochewa na yeye kutoka kwenye familia ya Kikristo na kulelewa katika mazingira kama hayo.
Na licha yake kuufanya muziki wa densi kwa muda, nafsi yake iliishia kumsukuma sana arejee kwenye laini.
Toka alipotangaza kuokoka na kisha baadaye kufunga ndoa na mchumba wake mpiga picha Victor Peace, Cece kawa kimya sana kwenye gemu.