• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
KILIMO: Anasifika kukuza nyanya licha ya ndoto yake kusomea kilimo kuzima

KILIMO: Anasifika kukuza nyanya licha ya ndoto yake kusomea kilimo kuzima

Na SAMMY WAWERU

KATIKA kijiji cha Karii, wadi ya Kangai, Kirinyaga na karibu kilomita tisa kutoka Kagio, shamba la Erastus Muriuki ni uga wa mafunzo ya ukulima bora na wa kisasa wa nyanya kwa wakazi kaunti hiyo.

Ni ufanisi ambao umejiri licha ya kupitia changamoto tele, ikizingatiwa kuwa ukosefu wa fedha ulimnyima fursa ya kuendelea na masomo.

Safari yake kunoa bongo ilifikia kikomo 1987 baada ya kuhitimu shule ya msingi.

Anasema alilelewa na mama mzazi pekee ambapo alifanya vibarua vya kijungu jiko kukimu wanawe. Hakuwa na budi ila kujiunga naye katika vibarua almuradi nduguze wasome.

Anasimulia kwamba matamanio yake kuendelea na masomo ya upili na hadi taasisi ya juu ya elimu ambapo alimezea mate taaluma inayohusiana na masuala ya kilimo, yalifikia kikomo. “Nilitamani kusomea kozi ya kilimo, niwe afisa, ili nigeuze eneo nilikozaliwa likumbatie mfumo wa kisasa kukuza mimea,” asema.

Bw Muriuki ambaye kwa sasa ni mkulima tajika Kirinyaga hususan katika uzalishaji wa nyanya, anasema alipata ajira katika boma la afisa mmoja wa kilimo kaunti hiyo kama shambaboi.

Hata ingawa alipokea kipato cha Sh20 kwa siku, lilikuwa jukwaa lililomnoa sambamba katika masuala ya kilimo ikikumbukwa bosi wake alikuwa mtaalamu na gwiji wa zaraa.

Kulingana na Muriuki 48, kufikia 1994 alikuwa ameweka akiba ya Sh3, 000, ambazo alitumia kuanzisha shughuli za kilimo. Anasema nyanya yake, anayemtaja kama nguzo kuu maishani mwake, alimpa kipande cha shamba chenye ukubwa wa robo ekari.

Akiwa amejihami kwa ujuzi na maarifa aliyopokea kama shambaboi awali, Muriuki alizamia ukuzaji wa nyanya, anazozalisha hadi kufikia sasa. “Mwajiri wangu alinifunza mengi, kuanzia pembejeo bora; mbegu, mbolea na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa, na kufanya kilimo bora. Niliiga mafunzo hayo,” aeleza mkulima huyo.

Muriuki ambaye ni baba wa watoto watatu, anasimulia kwamba aliimarika kiasi cha kuweza kukodi hadi ekari 20.

Licha ya ufanisi aliopiga mbele, mkulima huyu anasema 1998 alikadiria hasara ya nyanya zenye thamani ya Sh240, 000 na 2005 pigo lingine la zaidi ya Sh1.6 milioni kwa sababu ya ukame, mabadiliko ya hali ya anga na minyanya kuathiriwa na magonjwa.

“Hasara ya mwaka 2005 nililazimika kuuza lori langu, kwa kuwa mazao niliyovuna yalinipa chini ya Sh100, 000,” asema.

Hata hivyo, changamoto hizo hazikuzima ndoto zake. Mkulima huyo amewekeza pakubwa katika kilimo cha nyanya.

Kwenye ekari moja na nusu, anayomiliki, tunampata akikagua minyanya inavyoendelea.

Pia, ana ekari zingine sita anazokodi, na zote ‘amezirembesha’ kwa nyanya. “Kwa mwaka hufanya misimu miwili. Shamba la kukodi, ekari moja ni Sh5, 000 kwa msimu,” afichua, akiongeza kuwa ana wafanyakazi wanane.

Hukuza nyanya aina ya Bolgan F1na Perseo F1, kutoka kwa HM. Clause Kenya Ltd.

Mbali na nyanya, kampuni hiyo pia hutafiti na kuzalisha mbegu za mboga, matikitimaji na pilipili mboga.

Ekari moja inasitiri mbegu 10, 000. Sacheti ya punje 5, 000 za mbegu ya Bolgan inagharimu Sh14, 850, kipimo sawa na hicho cha Perseo kikiwa Sh13, 000. H.M Clause pia inauza kipimo cha punje 1, 000 za Perseo Sh3, 000.

Ikizingatiwa kuwa soko limesheheni mbegu bandia, wataalamu wanahimiza wakulima wa nyanya kuwa makini kwani hilo ni mojawapo ya vichangio vya mazao duni na changamoto ibuka.

“Ufanisi katika kilimo cha nyanya unategemea msingi wa mbegu, ambazo zinapaswa kuwa bora. Wakulima wawe makini wanaponunua mbegu iwapo wanataka mazao mengi na bora kwa sababu kuna nyingi duni na bandia sokoni,” ashauri Bw Sébastian Alix, mtaalamu na mkurugenzi wa HM. Clause hapa nchini.

Kauli yake kuhusu uhalisia wa mbegu pia inakaririwa na Benoit Montalegre, ambaye ni meneja wa mauzo katika kampuni hiyo, Ukanda wa Afrika Mashariki.

Bw Montalegre anashauri wakulima wa nyanya kununua mbegu zilizoidhinishwa na taasisi husika za kiserikali kama vile ya Utafiti wa Ubora wa Mimea, KEPHIS.

Miche ya nyanya huandaliwa kwenye kitalu kwa muda wa karibu mwezi mmoja.

Minyanya ina mizizi inayopenyeza ardhini, hivyo basi inahitaji udongo tifutifu ambao ni mwepesi na usiotuamisha maji.

Erastus Muriuki hutumia mfumo asilia wa ng’ombe katika kulima, maarufu kama Ox-plough kwa Kiingereza.

Jembe maalum hufungiwa kwa ng’ombe dume, analivuta likilima inchi nne kuenda chini. Pia, hutumia trekta, ambalo hulima inchi sita.

Kwa usaidizi wa dume, Muriuki huandaa mitaro kisha mashimo au makoongo yenye urefu wa inchi mbili.

Kitaalamu, nafasi ya mstari mmoja hadi mwingine iwe sentimita 145 na mashimo sentimita 25. Mbolea ichanganywe sawasawa na udongo, na pia unaweza kuongeza fatalaiza.

Katika uzalishaji wa nyanya, maji ni kiungo muhimu.

Masuala mengine kutilia maanani ni matunzo ya minyanya kupitia palizi na mbolea yenye madini yanayoimarisha mazao.

Nyanya ni miongoni mwa mazao yaliyovamiwa na mawakala.

Muriuki anasema wafanyabiashara hawa wanaendelea kukandamiza wakuzaji wa nyanya nchini kwani kreti inaborongwa hadi kufikia kilo 180.

“Wameibuka na mbinu ya kupakia kreti inazidi kipimo chake, kutoka kilo 130 hadi 180. Bei bado ni ileile ya kuumiza mkulima, ikikumbukwa kuwa yeye ndiye amebeba gharama ya kuzalisha,” akalalama wakati wa mahojiano.

You can share this post!

Wanyoa nywele kupinga kuteuliwa kwa Cho Kuk kuwa waziri

ULIMBWENDE: Jinsi ya kuifanya mikono, viganja na vidole...

adminleo