• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
KILIMO CHA FAIDA: Karoti ina mazao mengi hata ikikuzwa kwenye kipande kidogo cha ardhi

KILIMO CHA FAIDA: Karoti ina mazao mengi hata ikikuzwa kwenye kipande kidogo cha ardhi

Na GRACE KARANJA

KAROTI ni zao la jamii ya mizizi na mojawapo ya mboga zinazokuzwa na kuliwa sana nchini Kenya.

Kwa kawaida hupatikana katika rangi tofauti lakini zinazokuzwa sana na zina umaarufu hapa nchini Kenya ni za rangi ya machungwa na nyekundu.

Karoti zina faida kubwa katika mwili wa mwanadamu kwani zina vitamini A na C pamoja na madini ya chuma.

Wakulima wengi wadogo wanajikimu kimaisha kupitia kilimo biashara cha karoti kwa sababu mavuno yake ni mengi hata ikiwa mkulima amelima katika kipande kidogo cha ardhi.

Karoti huchukua muda mfupi wa kukomaa ikilinganishwa na mazao mengine kama vile mahindi, pia karoti haihitaji muda mwingi wa uangalizi. Hapa nchini Kenya karoti huliwa kama mboga.

Mkulima anachofaa kuangazia wakati anaanzisha kilimo cha karoti ni aina ya mchanga na pia hali ya hewa iliyoko katika maeneo ya kukuza zao hili. Hata hivyo, kulingana na mtaalam wa kilimo Julius Nduati, zao la karoti halifanyi vizuri katika udongo wa ufinyanzi (clay) au ulie ulio na mawe mawe. Udongo wa mchanga tifutifu ndio unafaa katika kilimo cha karoti, na pia katika maeneo yaliyo na joto kiasi.

“Maeneo yaliyo na joto kali hayafai katika ukuzaji wa zao la karoti, kwani huhitaji kiwango cha joto cha nyuzi 15 na udongo ulio na virutubisho, na ambao unaweza kupitisha maji na mwanga kwa urahisi. Hii ni kwa sababu mwanga husaidia ukuaji wa matawi halikadhalika udongo hupenyeza maji vizuri na hufanya mizizi ya zao hili kuwa refu na nene,” mtaalam huyu anaeleza.

Ladha tamu

Walaji wengi hutofautiana kuhusu ladha ya mboga hii aina ya karoti wengine wakipendelea kula zile zinazopandwa katika mazingira ya baridi kwani wanasema kuwa zina ladha tamu.

Hata hivyo kuna wale husema zilizokuzwa maeneo ya joto la wastani ndio zina ladha ya sukari.

Tulipozuru maeneo ya Sulmack yaliyoko katika mpaka wa Kaunti ya Kinangop na Kiambu, vijana hapa wana bidii na wanasema wanategemea kilimo kujiinua kimaisha.

Licha ya changamototo wanazokumbana nazo katika kilimo kama vile ukosefu wa hela za kulima maeneo yenye ardhi kubwa, wanasema kuwa mapato wanayopata yanawasimamia kimaisha na hawana nafasi ya kujiunga na makundi ya kihalifu.

“Tunaweza kuwa hatuna mashamba makubwa lakini hili dogo tulilo nalo tunafaidika kwa sababu tuna kazi ya kilimo tunaendeleza,” mwenyekiti wa kikundi cha Sulmack Young Farmers anaeleza.

Wanachukua fursa hii kumshukuru mtaalam wa mbegu kutoka kampuni ya Starke Aryes ambaye amejitwika jukumu la kwenda mashambani na kuwapa mafunzo vijana kuhusu jinsi ya kulima karoti kwa faida. Aidha mkulima wa shamba hili lenye ukubwa wa ekari mbili unusu anawaomba wazazi ambao wamefanikiwa maishani na wana mashamba makubwa yaliyo wazi wasaidie vijana wao walio na ari ya kilimo ili wajikuze kimaisha.

“Langu tu ni kuwahimiza wazazi walio na mashamba huru wawasaidie vijana ambao wanataka kujiendeleza wakiwa wangali wachanga wachanga sio wakati wamezeeka. Vijana walime wapate pesa, kilimo kina faida,” anasema Gichia Ndung’u, mkulima maarufu wa karoti eneo la Sulmack.

You can share this post!

AKILIMALI: Alifanya hesabu; ndizi zamlipa kuliko mahindi

Wizara yasitisha kwa muda uteuzi wa wanaolenga kusomea kozi...

adminleo