Kilimo cha matunda ya dragon champa tuzo
IKIWA kuna maamuzi asiyojutia, ni kuzamia kilimo cha matunda ya joka (dragon) ambayo hatimaye mwaka huu, 2024, yalimpa shime.
Si mwingine, bali ni Dkt Monicah Waiganjo ambaye kando na kuwa mkulima, ni mtafiti aliyewahi kuhudumu katika Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (Kalro).
Ana uzoefu wa muda mrefu katika kilimo cha matunda, hususan yenye thamani – kuteka soko lenye ushindani mkuu.
Dragon ni mojawapo wa matunda anayolima, akijituma pakubwa kuzalisha miche.
Katika Maonyesho ya Kimataifa ya Kibiashara Nairobi 2024, yaliyoandaliwa na Chama cha Kilimo cha Kenya (ASK), Monicah alitambuliwa kama mmoja wa watafiti hodari wa joka.
Utambuzi huo, mama huyu hauchukulii kama ushindi wake pekee, ila ni wa washirika wote wanaohamasisha ukuzaji wa dragon nchini.
“Tuzo niliyopata kama mmoja wa watafiti guru wa dragon ni ishara kuwa kuna kazi tunayofanya nyanjani. Sitasema ilikuwa bidii yangu pekee, ila pia Kalro imenifaa pakubwa,” akaambia Akilimali kwenye mahojiano ya kipekee.
Hata ingawa hakufichua endapo zawadi ya ASK ilijiri na minofu ya hela, Dkt Monicah alisema dragon ni kati ya matunda ambayo yakikumbatiwa kikamilifu hasa na vijana, kero ya ukosefu wa ajira itapungua kwa kiasi kikubwa.
Akitumia mfano wake, anasema alipostaafu kinyume na wengi ambao huhangaika kusukuma gurudumu la maisha, amepangwa na kilimo cha joka.
“Dragon ndiye mwajiri wangu,” anasema.
Mbali na matunda hayo, Dkt Monicah pia hulima maparachichi, maarufu kama avokado, ndizi, mapapai na machungwa maalum aina ya pixie.
Ndiye mwasisi wa Sungreen Harvest, kampuni yenye kiunga cha matunda eneo la Kithimani, Yatta, Kaunti ya Machakos kinachojishughulisha na uzalishaji wa miche, kilichoidhinishwa na taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea nchini (Kephis).
Dkt Monicah anataja dragon kama aina ya matunda ambayo kila Mkenya anapaswa kuwa nayo kwenye mazingira yake, kwa sababu ya tija zake anuwai.
“Hata ikiwa si kwa minajili ya biashara, kuza joka itakufaa kiafya,” anasema.
Matunda haya yamesheheni madini na virutubisho kama Carotenoids – pigmenti ya rangi nyekundu na manjano, pamoja na Lycopene (pigmenti nyekundu), ambazo ni muhimu sana kwa seli au chembechembe mwilini.
Dragon, hali kadhalika, ina Magnesium, Iron na mbegu zake Omega 3, madini ambayo Dkt Monicah anasisitiza husakwa sana kupitia matunda.
Akiwa na kiunga kingine katika Kaunti ya Kiambu ambacho pia huotesha mbegu na kuzalisha miche ya ndizi, avokado, pixie na mapapai, mtaalamu na mkulima huyu amejituma kuvumisha kilimo cha dragon.
Ni kutokana na mapenzi yake ya dhati kwa aina hiyo ya matunda ya thamani, kwa ushirikiano na wakulima ameanzisha chama cha ushirika, kinachojulikana kama Sun Yatta Sacco.
“Hutoa mafunzo kitaalamu jinsi ya kukuza dragon, na pia kusaidia wanachama kutafuta soko la mazao,” anaelezea.
Aidha, Dkt Monicah hushirikiana kwa karibu na mwajiri wake wa zamani, Kalro katika kutafiti na kuendeleza ari yake.
Dragon ni matunda yanayoweza kukua mahali popote nchini, ikizingatiwa kuwa Kenya ina udongo bora na hali nzuri ya hewa.
Maeneo yenye joto, yanakomaa kwa muda wa mwaka mmoja pekee, huku yenye baridi yakichukua miaka miwili, Dkt Monicah anadokeza.
Mtaalamu huyu hukuza dragon za rangi nyekundu, manjano na nyeupe.
Ni matunda ghali sokoni, hasa yale ya manjano akisema; “Yanauzwa mithili ya dhahabu”.
“Kulingana na aina, ndio maana kilo inachezea hadi Sh1, 000,” anasema Dkt Monicah.
Kwa mujibu wa takwimu za Idara ya Kilimo, Kenya, ekari moja inazalisha wastani wa tani sita kwa mwaka.
Kiwango hicho hata hivyo, Monicah anaamini kinaweza kuongezeka hadi tani nane, sawa na mataifa mengine Barani Afrika na ulimwenguni yanayolima dragon, endapo wakulima watakumbatia ukuzaji wa matunda haya.
Upanzi, kitaalamu inapendekezwa kila shimo liwe na mbegu – matawi manne, nafasi kutoka shimo moja hadi lingine ikipaswa kuwa mita mbili na nusu (between plants).
“Nafasi ya mistari ya mashimo hadi mingine (between rows), aghalabu huhimiza wakulima iwe mita tatu,” anashauri Dkt Monicah.
Matawi ya upanzi husitiriwa kwa kutumia vikingi, na ekari moja inahitaji vikingi 500 ukizidisha na matawi manne kwa kila shimo, ina maana kuwa yatakuwa matawi 2, 000.
Mbegu, Monicah anasema kila tawi lililo tayari kupandwa huuza Sh300.
Muhimu kupata mazao ya kuridhisha, mkulima atunze dragon kwa kutumia mbolea na fatalaiza zenye madini ya Magnesium, Calcium na Boron kuyaboresha.
Kenya, inakadiriwa kuwa na wakulima wapatao 10, 000 wanaokuza dragon.