Makala

KILIMO: Faida za 'greenhouses'

July 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMMY WAWERU

ILI kupata mazao bora na ya kuridhisha mkulima hakosi kupitia changamoto za hapa na pale katika jitihada zake.

Ni muhimu kukumbusha kuwa kilimo ndicho uti wa mgongo wa Kenya, na mataifa kadhaa duniani hususan yaliyo na udongo wenye rotuba na hali bora ya hewa.

Sekta ya kilimo hapa nchini huchangia pakubwa katika ushuru, pamoja na kuletea wakulima mapato.

Kwa jumla, ni kitega uchumi ambacho pia kimebuni nafasi tele za ajira katika mashamba na kampuni zinazoongeza thamani kwa mazao.

Mbali na kudorora kwa soko na bei duni ya mazao, changamoto za wadudu na magonjwa ndizo kizingiti kikuu kwa wakulima.

Ni gharama ambayo mkulima huibeba mwenyewe, ikizingatiwa kuwa bei ya pembejeo; mbegu, mbolea na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa, inaendelea kupanda kila uchao.

Ili kupunguza gharama ya uzalishaji wa mazao, ukuaji wa teknolojia unaendelea kuibuka na mifumo mbalimbali kuzinduliwa angaa kuokoa mkulima.

Kujiri kwa kilimo cha vifungulio, maarufu hema au greenhouse, kumesaidia kuangazia suala la wadudu na magonjwa.

Usambaaji wa wadudu na magonjwa katika eneo tambarare (open field) ni wa kasi ukilinganishwa na kwenye hema.

Hili linachangiwa na upepo.

Ukulima kwenye kifungulio unadhibiti changamoto hiyo, kwani huwa kimeezekwa kwa karatasi ngumu ya nailoni juu na kandokando.

Ili kuruhusu hewa kuingia, kuna wanaotumia chandarua chenye mashimo madogo kandokando.

Brian Kimani ni mkulima wa nyanya na pilipili mboga eneo la Tigoni, Limuru kaunti ya Kiambu kwenye hema, na anasema teknolojia hii imemsaidia pakubwa kupunguza gharama ya kudhibiti wadudu na magonjwa.

“Ni rahisi kukabili wadudu na magonjwa kwenye kifungulio kwa sababu upepo umedhibitiwa. Isitoshe, wanaoruhusiwa kuingia humo ni wachache, hivyo basi mimea na mazao ni salama,” anaeleza Bw Kimani.

Kupanda kwa bei ya dawa za kuangamiza wadudu na magonjwa ni jambo linalohangaisha mkulima, hivyo basi anahitaji mbinu za kushusha gharama hiyo.

Mkulima huyu alianza kilimo cha hema 2015, ambapo ilimgharimu mtaji wa Sh600,000 kukianzisha.

Ana mahema mawili yaliyokalia kipande cha ardhi anachomiliki chenye ukubwa wa ekari mbili, ambayo ameyagawanya ili kusitiri mimea anayokuza.

Hata hivyo, anasema mkulima chipukizi akiwa na mtaji wa Sh50, 000 anaweza kuanzisha kilimo cha hema.

“Unachohitaji ni karatasi ngumu ya nailoni, chandarua, miti na nyaya,” anadokeza.

Anasema la kutia moyo katika kilimo hiki, mkulima hahitaji kuwa na shamba kubwa.

Reuben Kimuhu, ni mkulima mwingine wa nyanya na pilipili mboga kwenye hema, na anasema iligharimu Sh70,000 pekee kung’oa nanga 2013.

“Nilianza kilimo cha hema jijini Nairobi, japo nikahamia kaunti ya Meru ili kukipanua,” anasema Bw Kimuhu.

Tija nyingine itokanayo na kilimo hiki ni kuwa si lazima mimea ipandwe kwa miche, kwani mkulima anaweza kupanda mbegu moja kwa moja kwenye mashimo au mitaro aliyoandaa.

“Mmea haupitii breki yoyote kama inavyoshuhudiwa wakati miche inapohamishwa kutoka kitaluni hadi shambani.

“Mkondo wa kupanda mbegu moja kwa moja huwezesha mmea kuwa na nguvu na hata kustahimili changamoto za magonjwa ibuka,” afafanua David Karira, mkulima wa pilipili mboga kwenye kifungulio kaunti ya Nyeri.

Taratibu za upanzi hufuatwa katika hema, na ambapo mfumo wa kutumia mifereji kunyunyizia mimea maji ni rahisi kutumia.

Aidha, mifereji husindikiwa kwenye shina la mimea.

Kulingana na wakulima hawa, mmea unaoonekana kuwa na dalili za ugonjwa ama magonjwa, hutambulika upesi na kung’olewa mara moja. “Magonjwa yanayoshuhudiwa ni yale yanayosababishwa na udongo, hasa kwa ajili ya kutumia kemikali,” anasema Bw Brian Kimani.

Bacterial wilt ndio ugonjwa sugu katika mimea, ingawa David Karira ameibuka na mbinu ya kuudhibiti. Mkulima huyu, baada ya kuvuna pilipili mboga zote, hung’oa mimea na kufunika eneo lote kwa karatasi ya nailoni hususan nyeusi.

“Hulifunika kwa muda wa miezi sita mfululizo ili kuua wadudu waliomo na kuondoa magonjwa ibuka,” anafichua Bw Karira.

Kwa sababu ya kukosa nafasi ya kutorokea, wadudu huweza kuangamia upesi kwenye hema. Eneo tambarare, dawa zikitumika upepo unachangia kurejesha wadudu wengine na hata kusambaza magonjwa.

Wataalamu wa kilimo hata hivyo wanahimiza haja ya kufanya mzunguko wa mimea (crop rotation) ili kusaidia kukabili magonjwa yanayosambazwa mimea.

“Kuna magonjwa yanayoathiri familia moja ya mimea, hivyo basi mzunguko kwa familia tofauti ya mimea utasaidia kuyaondoa,” ashauri Bw Benoit Montalegre, mtaalamu kutoka H.M Clause; kampuni ya kuunda mbegu.

Pia, anahimiza umuhimu wa kupanda mbegu bora.

Mzunguko pia husaidia kuimarisha rutuba ya udongo. Mimea iliyoko kwenye familia ya legumes kama vile maharagwe huaminika kuongeza Nitrojini katika udongo.