KILIMO: Manufaa ya mbegu za ndizi zilizoimarishwa 'tissue culture banana'
Na SAMMY WAWERU
HADI kufikia sasa baadhi ya wakulima wanaendelea kukuza ndizi kupitia mfumo wa machipukizi (suckers). Huu ni mkondo wa zamani ambapo migomba michanga inayojitokeza kandokando mwa migomba mama hutolewa na kutumika kama mbegu. Inatumika kwa msingi kuwa inapunguza gharama, ikiwa ni pamoja na kupandwa moja kwa moja.
Baadhi ya wadau wa masuala ya kilimo wanasema kwamba mfumo huo una changamoto zake kwani migomba na mazao huathiriwa upesi na wadudu na magonjwa kama Fusarium wilt, Sigatoka na Bacterial wilt.
Magonjwa ya virusi kama banana streak na bunchy top, yanasambazwa na machipukizi.
Fukusi na Nematodes, ni wadudu wanaoshuhudiwa mara kwa mara kwa migomba iliyopandwa kutoka kwa machipukizi.
Migomba inayoepuka na kustahimili changamoto hizo, huchukua muda mrefu kukomaa.
“Mazao ya mbegu za aina hiyo, machipukizi, huwa haba,” anasema James Macharia, mtaalamu kutoka Green Oasis Plants Centre, Murang’a.
Ukuaji wa teknolojia, pia umekuwa wenye tija chungu nzima katika sekta ya kilimo. Uzalishaji wa ndizi ni mojawapo ya inayojivunia kwa hatua hii.
Kujiri kwa mbegu zilizoimarika, maarufu kama ‘tissue culture bananas’ kumekuwa kwa manufaa kwa wakulima wa ndizi nchini.
Ni mfumo mpya, uliotafitiwa na kuidhinishwa, ambapo changamoto zinazoshuhudiwa kutokana na upanzi wa machipukizi kama mbegu zimetatuliwa.
Aidha, watafiti wameweza kuibuka na uzalishaji wa mbegu za hadhi ya juu na zinazowiana na uwezo wa ‘mmea mzazi’ au mother plant.
Kuwa salama
Kupitia mfumo huu mpya, Bw Macharia anasema miche mingi inazalishwa kwa wakati mfupi na huwa salama dhidi ya wadudu na magonjwa.
Migomba michanga hupelekwa katika maabara ili kuzalishwa mbegu-miche, kupitia taratibu zilizowekwa.
Baadaye huhamishiwa katika kifungulio, greenhouse, ili kutunzwa kwa wiki kadhaa kabla kupandwa.
Ndizi hukua vyema maeneo yanayopokea kiwango cha mvua zaidi ya milimita 1,000 kwa mwaka. Yasiyoafikia kigezo hiki, wakulima wanahimizwa kutumia mfumo wa kunyunyuzia maji mashamba kwa mifereji.
Mtaalamu James Macharia anasema udongo unapaswa kuwa wenye rutuba.
“Usiwe unatuamisha maji,” anashauri Bw Macharia.
Maji mengi husababisha mimea na mazao kuoza.
Miche ya ndizi hupandwa kwenye mashimo, moja likipendekezwa kuwa na upana-diameter, wa futi 3 na urefu wa futi 2 kuenda chini.
“Kipimo cha nafasi kati ya mashimo kiwe mita 3 mraba,” asema Bi Lucy Muriithi, mkuzaji wa ndizi zilizoimarishwa kaunti ya Kirinyaga.
Kulingana na mkulima huyu udongo wa juu huchanganywa na mbolea ya mifugo na ya kisasa pamoja na dawa dhidi ya wadudu.
Mchanganyiko huo hurejeshwa shimoni, linamwagiliwa maji kisha mche unapandwa kimo cha karibu sentimita 40.
Mtaalamu Macharia anashauri wakulima kupanda miche iliyoidhinishwa na taasisi husika za kilimo nchini kama vile Karlo.
Chuo Kikuu cha Masuala ya Kilimo na Teknolojia (JKUAT) pia huzalisha tissue culture bananas.
Baada ya upanzi, unahimizwa kutumia nyasi za boji-mulching, zilizokauka ili kuzuia uvukuzi wa maji.
“Maji ni kiungo muhimu katika kilimo cha ndizi. Mazao bora na mengi yanapatikana ukiwa na chanzo cha maji ya kutosha,” anaeleza mkulima Lucy, akidokeza kwamba hutegemea maji ya Mto Thiba ambapo ameelekeza mtaro shambani mwake.
Ndizi zilizoimarishwa huanza kuzalisha baada ya mwaka mmoja na miezi mitatu, kinyume na machipukizi yanayoanza baada ya miaka miwili.
Ekari moja ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 25 sawa na kilo 25,000.
Hata hivyo Lucy anasema ndizi huuzwa kwa vifungu vinavyozalishwa ambapo kimoja hugharimu kati ya Sh400 na Sh800.