Kilimo mseto ni siri ya mapato ya juu
WAKULIMA mbalimbali wamejua siri ya kuzidisha mapato ya mazao shambani ni kuongeza uwezo wa shamba kuwa na mimea zaidi ya moja.
Katika shamba lake lililoko kitongojini Mwarano, eneobunge la Kigumo, Kaunti ya Murang’a, Eunice Wanjiru anachanganya miparachichi na mahindi.
Aliamua kukumbatia mtindo huu shambani mwake baada ya kupata shamba kubwa kiasi ambalo sasa ni angalau ekari moja.
Anakiri kuwa, awali alikuwa anajishughulisha sana na mboga kabla ya kukuza mahindi na avokado.
Angali anakuza mboga kama vile kabeji, sukumawiki na spinach katika sehemu zingine za shamba.
“Parachichi zangu hununuliwa sana na wauzaji wanaosambaza mazao haya nje ya nchi,” anatanguliza Wanjiru. “Mazao ya mahindi aghalabu huwa chakula cha mifugo huku mengine yakinunuliwa na watumiaji masokoni.”
Amejishughulisha na kilimo cha miparachichi kwa zaidi ya miaka mitano.
Hapo awali alikuwa mkuzaji wa mboga tu. Lakini baada ya miti hii ya matunda kupata soko kubwa nje ya nchi, aliamua pia kuikumbatia.
Akisubiri miparachichi ikomae tayari kuuzwa sokoni, Wanjiru huendeleza kilimo cha mazao ambayo hukomaa baada ya muda mfupi.
“Nikisubiri avokado zikuwe tayari, mimi ninaendelea kupata pesa kutokana na sukumawiki, kabeji, maharagwe na spinach,” anaeleza. “Nimeongeza mahindi pia ambayo hukomaa baada ya kati ya miezi mitatu na minne.”
Wanjiru ni mmoja wa wakulima katika eneo hili ambao wanapendelea mazao ambayo yananawiri haraka.
“Hatutaki mahindi ambayo yanakaa shambani sana kwa sababu tunataka mapato ya haraka,” anaendelea akisema maendeleo ya teknolojia ya kilimo yanawezesha wakulima kufurahia kazi zao shambani.
Aghalabu wakulima hawa wa Kangari huanza kuvuna kuanzia Oktoba hadi kuelekea Februari, miezi ambao anaeleza faida huwa kubwa.
Akiangazia miparachichi, Wanjiru anasimulia kuwa ndiyo hatua kubwa ambayo amewahi kuchukua katika kilimo.
Kufikia sasa ana zaidi ya miti 50 ya avokado.
“Uzuri wa avokado ni kuwa hazihitaji uangalizi mkubwa wa mara kwa mara kama mimea hii mingine shambani,” anakiri. “Baada ya kupanda, kupalilia na kunyunyizia dawa, avokado inastawi kisha kuzaa mapato makubwa zaidi.”
Mkulima huyu amepokea mafunzo na ushauri kutoka kwa wataalamu wa kilimo kutoka kaunti ya Murang’a pamoja na wataalamu wa kibinafsi.
Kwa hivyo, amejua umuhimu wa kilimo asilia na kutangamana na wataalamu ili kuimarisha stadi na maarifa yake ya masuala ya kilimo.
Reuben Chomba ni mmoja wa maafisa wa kilimo vitongojini ambao huwashika mkono wakulima wa ngazi za chini.
“Mimi ni mtaalamu wa kilimo asilia na pia mkulima wa mazao mseto,” anaambia Akilimali. “Nina mtandao wa wakulima angalau 100 katika kaunti ya Murang’a ambao wamenufaika na mafunzo ya kilimo asilia.”
Chomba pia hukuza viazi vitamu, mboga, mahindi na miparachichi.