Makala

Kilio sheria mpya kutokomeza ulevi zinaleta mianya ya hongo

March 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA MWANGI MUIRURI

TANGU serikali itoe amri kwamba maafisa wakuu wa usalama, wale wa ukadiriaji ubora wa bidhaa, na walio katika huduma ya kusajili baa wasijiingize katika biashara ya vileo, kuna vilio kwamba milango tele ya ufisadi imefunguliwa.

Pia maafisa wa ukusanyaji ushuru waliambiwa wasijiingize katika biashara hiyo.

Wamiliki wa baa ndio wanalia zaidi, wakitoa malalamiko kwamba amri hiyo imeiongeza nguvu mitandao ya makateli wa kuwafyonza faida zao kwa kiwango kikuu.

Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki mnamo Ijumaa alishikilia kwamba wote ndani ya serikali kama maafisa wa usalama ni lazima wajiondoe kutoka biashara ya pombe.

Tayari, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja ametoa ilani kwa wakuu wote wa usalama kuhakikisha kwamba amri hiyo ya maafisa kufunga biashara walizo nazo za pombe imetekelezwa, swali kuu likiwa ni nani ataamrisha hao wakubwa ikiwa wako na baa, wazifunge.

Aidha, inahofiwa kwamba maafisa wa polisi wameanza kuwa wabunifu ambapo wanaingia mitaani na kukamata vijana kiholela na kuwadai hongo ili wakwepe adhabu kali mahakamani.

Mwenyekiti wa makanisa asili Mlima Kenya Askofu Edward Nyutu aliteta kwamba vita dhidi ya ulevi na mihadarati vinageuzwa kuwa vya misako ya kiholela.

“Watu wengi wasio na makosa watajipata mahakamani na kisha kutupwa jela huku nao wasio na nguvu ya kuhonga wakifungiwa biashara zao pasipo haki,” akadai Bw Nyutu.

Alisema kwamba wanasiasa hasa walio katika mabunge ya Kitaifa, Seneti na yale ya Kaunti pia ni watunzi wa sheria na pia wao ndio hupiga serikali msasa hivyo basi kuwa katika biashara ya baa huenda isambaratishe haki kwa wawekezaji wote.

Bw Nyutu alisema kwamba “kwa madhabahu sisi ni wa haki ya kila mtu, hata watenda dhambi wanaofaa kupewa mwongozo maishani”.

“Hukumu kwa mujibu wa haki na imani inafaa kuwa ya kusawazisha wote chini ya sheria lakini hilo sio tunaloshuhudia katika vita hivi,” akalalama.

Wamiliki wa baa katika eneo la Mlima Kenya ambako amri hiyo mpya inavumishwa kwa makali zaidi ndio wameteta kwa sauti kwamba “maafisa wa polisi wanavamia baa na kudai kwamba wanajua mwekezaji ni afisa wa serikali”.

Kujitetea na ukweli, wamiliki hao wakiongozwa na mshirikishi wa muungano wao Bi Stella Githua walisema Alhamisi kwamba anayeandamwa hutoa pesa kati ya Sh5,000 na Sh20,000 ndipo aachiliwe.

Aliongeza kwamba katika rekodi za leseni zinazotolewa na serikali za kaunti kumezuka mtandao mwingine ambao unabadilisha majina yaliyo katika leseni hizo kupitia hongo.

“Maafisa wote wa serikali ambao wamewekeza katika biashara ya vileo kwa sasa wanalipishwa kati ya Sh3,000 na Sh10,000 kubadilishiwa majina ya leseni. Maafisa hao wanaandikisha leseni mpya kwa majina ya wachumba wao au watoto wao huku wengine wakiunda kampuni au vyama vya ushirika na kutoa hongo ndipo idhini ya kibiashara iwe na majina mbadala,” akasema.

Haya yalijiri huku wamiliki wa baa wakiteta kwamba amri ya serikali kupitia Naibu Rais Rigathi Gachagua na waziri Kindiki kwamba maafisa wa serikali wajitoe kwa biashara ya uuzaji pombe ilihepa kuwajibisha wanasiasa.

“Wanasiasa ndio hatari zaidi katika uuzaji pombe. Katika Mji wa Murang’a kwa mfano, kuna wanasiasa kadha ambao ndio washirikishi hata wa usambazaji pombe zisizokadiriwa ubora. Huwezi ukaandama mtandao huo wa wanasiasa kisheria kwa kuwa wao hukutisha na kuandaa maandamano,” akasema afisa mmoja wa usalama wa eneo la Murang’a Mashariki.

Alisema baa zinazomilikiwa na washirika wa wanasiasa hupigia majirani kelele usiku kucha kupitia muziki wa sauti ya juu, kuuza pombe za vipimo kinyume na sheria na kupinda sheria ili kuhudumu kwa muda wa saa 24.

Afisa huyo alisema kwamba wanasiasa hao huficha pombe haramu ndani ya nyumba zao na kwa kuwa wameungana na kuwa na mizizi ya kisiasa na hata ndani ya vitengo vya usalama, wao ni serikali, katiba na sheria kivyao.

“Kila afisa ambaye hutumwa kufanya kazi hapo nyumbani kwa mwanasiasa ni lazima wajuane kwanza ambapo onyo hutolewa kuhusu kutatiza mpangilio huo wa kibiashara,” akafichua.

Maafisa kadha wameripoti kuhamishwa kupitia ushawishi wa wanasiasa na washirika wao wa biashara ya pombe.

Katika amri mpya ambayo imetolewa, baa zote zilizo katika makazi ya watu, karibu na shule na maeneo ya ibada na pia zilizopewa idhini kinyume na sheria, inaagiza zifungwe mara moja.

Wamiliki wa baa wanateta kwamba amri hiyo inalenga tu wanyonge wa uwekezaji huku wanasiasa, wafadhili na wanaowapigia kampeni, maafisa wastaafu wa polisi na marafiki wa serikali, baa zao zikizidi kuhudumu pasipo vikwazo.

[email protected]