Makala

Kimbunga Melissa chapiga Cuba baada ya kuleta uharibifu mkubwa Jamaica

Na MASHIRIKA, WINNIE ONYANDO October 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

JAMAICA imekumbwa na Kimbunga kikali zaidi cha Melissa kilichoambatana na upepo mkali na mvua kubwa na kuleta uharibifu katika taifa hilo kabla ya kuelekea Cuba.

Waziri Mkuu wa Jamaica, Andrew Holness alitangaza kisiwa hicho kuwa eneo la maafa huku mamlaka zikitoa tahadhari kwa wakazi kubaki mahali salama.

Mafuriko na maporomoko ya ardhi yameshuhudiwa huku hali ya hewa ikiendelea kuwa hatari.

Waziri wa serikali, Desmond McKenzie, alisema hospitali kadhaa zimeharibiwa, ikiwa ni pamoja na katika wilaya ya kusini-magharibi ya Saint Elizabeth, eneo la pwani ambalo alisema limefunikwa na maji.

Kimbunga hicho ni kibaya zaidi kuwahi kuikumba Jamaica.

Kwa upande wmingine, takriban watu 735,000 walihamishwa kutoka kwa nyumba zao mashariki mwa Cuba.

Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel alionya kwamba kimbunga hicho kitasababisha ‘uharibifu mkubwa’ na kuwataka watu kutii maagizo ya kuhama.

Kusini-magharibi mwa Jamaika, parokia ya St. Elizabeth ilizama majini afisa mmoja alisema, na zaidi ya wakazi 500,000 kubaki bila makazi.

‘Ripoti ambazo tumekuwa nazo hadi sasa zinajumuisha uharibifu wa hospitali, uharibifu mkubwa wa mali ya makazi, nyumba na mali ya biashara, miundombinu na barabara zetu,’ Waziri Mkuu wa Jamaika Andrew Holness alisema.

Holness alisema kuwa serikali haijapokea taarifa za vifo vilivyothibitishwa kutokana na dhoruba hiyo, lakini kutokana na nguvu ya kimbunga hicho na ukubwa wa uharibifu huo, ‘tunatarajia kwamba kutakuwa na kupoteza maisha.’

Wataalamu wa hali ya hewa katika AccuWeather walisema Melissa iliorodheshwa kama kimbunga cha tatu kwa nguvu zaidi kushuhudiwa katika Visiwa vya Caribbean baada ya Wilma mwaka wa 2005 na Gilbert mwaka wa 1988.