Makala

KINA CHA FIKIRA: Ishi ukienda mbele badala ya kurudi nyuma!

November 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WALLAH BIN WALLAH

MAISHA ni safari ya kuenda mbele moja kwa moja mpaka mwisho!

Kila mtu anapaswa kutimiza wajibu wake wakati huu anapoishi. Mwanafunzi anaposoma shuleni asiwe mzembe wala asiwe mtoro wa kutoroka kutoka shuleni kuacha masomo! Baada ya kuzeeka hatarudi shuleni kusoma tena! Kila kitu kina wakati wake. Chochote unachostahili kufanya leo usingojee kesho.

Tafadhali, mtu yeyote au mfanyakazi yeyote asiwe mvivu! Afanye kazi zake vizuri kwa wakati unaofaa ili maendeleo na mafanikio yapatikane! Ni vyema kutimiza wajibu bila ya kutarajia ati siku moja miaka itarudi nyuma upate muda mwingine wa kufanya shughuli ambazo hukuzifanya miaka iliyopita! Maisha ni kama maji ya mto yanayoelekea baharini. Hayarudi nyuma kamwe! Yanayowezekana uyatende leo!

Bwana Tupatupa mwenye umri wa miaka sitini alipatwa na ugonjwa wa kiharusi ghafla! Viungo vya mwili wake vikapooza na kukosa nguvu kabisa! Alipelekwa hospitalini akalazwa akiwa mahututi si hayati si mamati! Kila mtu alikata tamaa na kusema, “Huyu hatapona!”

Baada ya siku kadhaa, usiku mmoja Tupatupa aliota ndoto kuwa punde angekata roho! Akaomba ndotoni, “Mungu wangu, mimi ninaaga dunia na kuwaacha wanangu bila chochote! Sikujitahidi kufanya kazi yoyote ya kuwaletea maendeleo wala mafanikio ya kuwasaidia maishani! Sasa wanabaki katika shida!!!”

Mara Tupatupa akasikia Mungu au Malaika akimwambia, “Tupatupa, hufi leo! Una miaka mingine arubaini ya kuishi duniani!” Maneno hayo yalimpa nguvu akapata fahamu akawa mzima tena! Asubuhi daktari alimpata Tupatupa akiwa amepona kabisa! Lakini moyoni alibeba siri ya kuishi miaka arubaini zaidi. Aliamini maana yake ni kurudi kuanza maisha upya ili aende akafanye kazi na majukumu ambayo hakutimiza alipokuwa kijana!

Daktari alipomhakikishia Tupatupa kuwa alipona arudi nyumbani, Tupatupa alimwomba amtume nesi wake aende akamnunulie mavazi ya vijana, suruali ya kuteremsha, shati, kofia ya chepeo, miwani ya jua na viatu vya kisasa vya ujana avae aonekane kijana anapotaka hospitalini akienda nyumbani! Tupatupa aliacha mavazi na kila kitu cha kizee hospitalini! Alitembea kwa makeke na mikogo kama kijana huku bega moja ameliinamisha chini! Alipokuwa akivuka barabara, gari la ambulensi lilimgonga akakata roho pale pale! Tupatupa alipofika mbele ya kiti cha enzi alilalamika, “Mungu wangu, uliniambia ningeishi miaka mingine arubaini! Kulikoni?” Mwenyezi Mungu akamjibu akilini, “Samahani, Malaika wangu wanaokulinda hawakukutambua kwa jinsi ulivyojibadilisha!”

Ndugu wapenzi, maisha hayarudi nyuma hata ukifanya nini! Tekeleza wajibu na majukumu yako leo leo! Liishalo haliji tena!!!