KINA CHA FIKIRA: Kusomasoma ni hazina kuu ya maarifa maishani
Na WALLAH BIN WALLAH
KATIKA maisha ukitaka uwe na maarifa mengi, busara, elimu na ujuzi mpevu kichwani kuhusu mambo mengi, soma sana vitabu, magazeti, majarida na machapisho mengineyo ainati.
Kusoma mara kwa mara kunamsaidia mtu kujiboresha, kujielimisha, kujifurahisha na kujifanyia utafiti ili ayafahamu mambo mengi maishani.
Mtu yeyote asipojisomea kwa mapana na marefu anapokuwa shuleni au baada ya kutoka shuleni ama chuoni atabakia hivyo hivyo na maarifa aliyoyapata katika nyakati hizo alipokuwa masomoni. Kisichonolewa huwa butu.
Masikitiko ni kwamba watu wengi wanataka kuwa wenye elimu bora na maarifa mengi lakini wanaogopa kusomasoma vitabu, magazeti na majarida ili kujiongezea maarifa! Mathalani, wapo wanafunzi waliosoma wakiwa shuleni au vyuoni kwa ajili ya kupita mtihani tu! Tena walivisoma vitabu vile vile vilivyoidhinishwa na kupendekezwa kutahiniwa masomoni tu basi! Ni kama waligombana na vitabu au walitalikiana! Hasara iliyoje?
Hali ni hiyo hiyo kwa wazazi, wafanyakazi na ndugu zetu wengine waliokamilisha masomo zama zao hizo! Baada ya masomo yao, hawakusoma na hawasomi tena chochote cha kuwaongezea maarifa!
Kutosomasoma ni kujinyima fursa na uwezo wa kujiongezea maarifa, elimu, busara, ujuzi, burudani na mambo mengi yanayosaidia kujenga ubongo na akili za mwanadamu kuimarika na kupevuka zaidi. Hapo tuwapongeze sana nyinyi nyote mnaopenda kusomasoma ili muerevuke na kuburudika maishani! Heko kwenu!
Tabia na desturi ya kusomasoma ndiyo mbinu muhimu ya kumwezesha mtu kujielimisha na kujifahamisha mambo na masuala yanayoibuka katika jamii ili kuenda na wakati.
Mfano, mwanafunzi mwenye mazoea ya kusomasoma vitabu vingi, majarida, magazeti na machapisho mengineyo huwa mwerevu sana na mwepesi wa kuyajibu maswali mbalimbali darasani. Naye mwalimu anayesomasoma kwa mapana na marefu hapa na pale huwa bora na mahiri zaidi katika kufundisha darasani.
Tija
Vivyo hivyo, mtu yeyote aliye na mazoea ya kusomasoma vitabu, majarida au magazeti ya Kiswahili ama ya Kiingereza kama Taifa Leo, Taifa Jumapili, Daily Nation, Sunday Nation na kadhalika, hujipatia mambo mengi yanayohusu elimu, ufundi, ujuzi, kilimo, ufugaji, uvuvi, lugha, ujasiriamali, michezo, chemshabongo, burudani na mawaidha mengi ya busara maishani. Kwa hakika kusoma kwingi ni kujifunza mengi!
Ndugu wapenzi tusome! Vijana someni! Shime wananchi wote, someni! Tusome kila mara tujiongezee maarifa na kujiburidisha ili kupunguza misongo ya mioyo wakati huu wa gonjwa la Korona! Usikubali kubakia hivyo hivyo ulivyo! Kusomasoma ni hazina kuu ya maarifa katika maisha! Soma!!